Yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake.

Yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake.

SWALI: Mstari huu una maana gani? “yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.(Mhu 7:15)”

JIBU: Shalom,Tukianza na mstari wa 15 anasema:

“Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.

Huyu ni Sulemani akizungumza maneno hayo, anasema akiwa katika siku za UBATILI wake, yaani akiwa katika siku za masumbuko yake ya kutafuata jumla ya mambo yote, alikutana na Fumbo moja ambalo lilimtatiza sana, na Fumbo lenyewe ndio hili “yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake”. Au kwa lugha nyingine iliyorahisi ni kusema wenye haki wengi hawaishi muda mrefu, lakini wale waovu ndio wanakuwa na maisha marefu. Aligundua Kumbe haki haipimwi kwa kipimo cha umri mrefu mtu anaoishi. Fumbo hili linafanana na lile lingine alilolisema katika:

Mhubiri 9: 11 “Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.”

Hata wewe mambo haya yatagonga kwenye kichwa chako lakini huo ndio uhalisi, Ni mara ngapi unasikia na kutazama wale watu ambao hawana elimu,wala hawana ujuzi tena kama wamefika mbali sana, wengine labda ni darasa la 7 lakini hao ndio wanaokuwa matajiri sana? . Hili ni funzo kwako ikiwa utatafuta ujuzi au elimu kwa kigezo cha kuwa bilionea, utavunjika moyo , vilevile ikiwa unautafuta ufalme wa mbinguni ili uje upate utajiri kwa sadaka, kadhalika utavunjika moyo sana! Au leo hii unaokoka ili mambo yako ya kiuchumi yakae vizuri, yaani hiyo ndio sababu ya wewe kuokoka.. unajeweka katika hatari kubwa ya kuvunjika moyo huko mbeleni…Hekima na wokovu havina ushirika na pesa kabisa.. Tukiendelea na mistari unaofuata anasema ..

Mhubiri 7: 16 “Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?

17 Usiwe mwovu kupita kiasi; Wala usiwe mpumbavu; Kwani ufe kabla ya wakati wako?

18 Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; kwa kuwa mtu yule amchaye Mungu atatoka katika hayo yote.”

Kuna mambo mawili hapo la kwanza usiwe na haki kupita kiasi na pili usiwe mwovu kupita kiasi, yote haya yanaweza kukusababishia kifo ambacho hakijafikia umri wake. Lakini nataka upigie mstari jambo moja hapo la msingi hasemi usiwe na haki au usiwe na hekima, hapana bali anasema usiwe na haki KUPITA KIASI wala usiwe na HEKIMA KUPITA KIASI, hii inafunua tabia ya kujikweza, kujionyesha kuwa wewe ni kitu Fulani, wewe ni mtakatifu kuliko wengine, mifano dhahiri ya matukio kama haya tunayo, tunaweza kuyaona si kwa wengine zaidi ya waandishi na mafarisayo.. Ukisoma Luka 18:10-14 utaona Bwana Yesu alitoa mfano huu….

“Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.

11 Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.

13 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.

14 Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

Unaona, walijihesabia haki kupita kiasi, kufunga kwao, kutoa kwao zaka,kutokuzini kwako, ndio kulikowapa kiburi wajione wao ni kundi fulani maalumu mbele za Mungu na hiyo iligeuka kuwa hasara kwao kwa kuupoteza wokovu ambao wao ndio wangetakiwa waupate wakwanza.. Hivyo kama tukiangalia maudhui ya huyu mhubiri hasaa yalikuwa ni kutaka kuonyesha kuwa, sio mwenye haki, sio mwovu, sio mwenye hekima kupita kiasi sio mpumbavu anaweza kujiongeza maisha kwasababu ya mwenendo wake. Na ndio maana anahitimisha kwa maneno haya “18 Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; KWA KUWA MTU YULE AMCHAYE MUNGU ATATOKA KATIKA HAYO YOTE.”” Unaona, ukimcha Bwana utaepukana na hayo yote, Kumcha Bwana ni kujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kuitii injili yake na maagizo yake yote anayokupa kwa kufanya hivyo basi utapata hekima iliyo sahihi ya kumwendea mbele zake..Ndio mhubiri maana huyo huyo anasema kumcha Bwana ndio chanzo cha hekima na maarifa, Na sio hekima ndio chanzo cha kumcha Bwana.

Hivyo leo hii mtu Yule atakayekubali kumtii Kristo na kuyaishi maneno yote aliyoyasema atakuwa na uhakika kuwa amesimama upande ulio salama. Lakini ukiwa mtu wa dini(kama mafarisayo na waandishi, ambao wao wanajiona wao tu ndio wanao Mungu wengine wote ni waovu, Na hiyo inawafanya hata hatawaki kusikia jambo lingine lolote, mfano tu leo, hata mtu umwelezeje kwamba biblia inasema hivi, maadamu tu dhehebu lake au dini yake halifundishi hivyo au haliamini hivyo basi hakusikilizi,..huko ni kujihesabia haki kupita kiasi biblia inakokukataza), Na ukiwa pia mwovu, mambo hayo mawili basi jua utakumbana na mauti (rohoni na mwilini).

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU.

MAANA YA HUU MSTARI NI IPI? MITHALI 14:4 ‘ZIZI NI SAFI AMBAPO HAPANA NGOMBE;BALI NGUVU ZA NGOMBE ZALETA FAIDA NYINGI’.

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

USIMFANYIE JEURI ROHO WA NEEMA.

KWANINI BWANA YESU ALISEMA PALE MSALABANI NAONA KIU?

KUCHEZA KARATA NI SAHIHI KWA MTU ALIYE MKRITO?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments