EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.

EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.

Heshima na Baraka za mwanamke uliyeolewa zipo kwa wakwe zako (hususani mama mkwe wako).

Vitabu viwili vikuu vilivyoitwa kwa majina ya wanawake ni Esta, na Ruthu. Vimeitwa hivyo sio kwasababu tu Mungu anataka kupitisha ujumbe wake wa wokovu kwa kanisa, lakini pia upo ujumbe mahususi unaowahusu wanawake.

Leo tutamtazama Ruthu kwa maneno machache sana. Wanawake wengi wanapitia mikwaruzo katika ndoa zao, na kikubwa ni saikolojia wanayojijengea kabla na baada ya kuolewa kwao, kuhusu wakwe zao, hususani mama-mkwe..Na hapo ndipo panapokuwa chanzo cha matatizo yote…Wanawake wengi wanaoniuliza juu ya matatizo ya ndoa zao, nimegundua kuwa asilimia kubwa hawana mahusiano mazuri na wakwe zao.

Nataka nikuambie ulipokuwa hujaolewa Baraka zako zilikuwa kwa wazazi wako waliokuzaa, lakini unapoolewa ujue kuwa Baraka za ndoa na za uzao wako zinahamia kwa wakwe zako haijalishi ni wabaya kiasi gani..

Kama tunavyofahamu habari ya Ruthu, na Orpa, wote hawa wawili waliolewa na watoto wa Naomi mkwe wao, lakini kwa bahati mbaya, Naomi akafiwa na mume wake na watoto wake wote wawili akabakia kuwa mjane, hivyo akawa hana mume wala mtoto wala mjukuu,..Lakini Naomi kwa ukarimu wake akawatangazia uhuru wakwe zake, warudi makwao kila mmoja akaolewe tena kwasababu bado walikuwa ni vijana na pia bado hawajazaa..Orpa akakubali kuondoa kurudi kwao, lakini Ruthu hakukubali kwasababu alijua Baraka zake zipo wapi…

Hivyo akaamua kurudi na mkwe wake nchi ya Israeli, akajitoa tu kama wakfu kuwa kama mjakazi wake, walipofika wakaishi pamoja,Na Ruthu akawa anamtumika mkwe wake kama mtoto wake kwa amani tu..Ruthu aliipoteza nafsi yake, ili tu amrudhishe mama mkwe wake, lakini alijua ndani yake haitakuwa bure kuwa vile.

Lakini kama tunavyojua, ni nini kilifuata baadaye..Licha tu ya Ruthu kuolewa na Yule tajiri Boazi ndugu yake Naomi, lakini watu wote walimwona kuwa anastahili kuliko watoto 7 wa Naomi..

Ruthu 4: 13 “Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na Bwana akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume.

14 Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe Bwana, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli.

15 Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, NAYE ANAKUFAA KULIKO WATOTO SABA, ndiye aliyemzaa.

16 Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake”.

Embu jiulize wewe mwanamke uliyeolewa, Je, mkwe wako alishawahi kukuona unastahili kuliko watoto wake wote alionao?.. Alishawahi kujivunia kwako kwa namna hiyo? Kama hakuna chochote alichowahi kujivunia kwako, lipo tatizo.

Na kama hiyo haitoshi, Ruthu ambaye alikuwa ni mwanamke wa kimataifa, akahesabiwa katika uzao wa Kiyahudi kama vile Rahabu alivyohesabiwa kwa tendo lake tu hilo , na huko huko baadaye ndipo alipokuja kutokea Mfalme Daudi.. Uzao wa kifalme na uzao wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Jaribu kufikiria tena jinsi uzao wake ulivyobarikiwa zaidi hata ya wanawake wengi wa kiebrania waliozaliwa na Ibrahimu…Na hiyo yote siri ilikuwa kwa MAMA MKWE WAKE na si penginepo. Ni yeye tu na Esta ndio waliopata nafasi ya vitabu vyao kuandikwa majina yao.

Hata wewe mwanamke uliyeolewa au unayekwenda kuolewa.. Timiza jukumu lako la kuwapenda wakwe zako kwasababu huko ndipo uzao wako utakapobarikiwa na ndipo ndoa yako itakapokuwa na amani..

Wewe kama siku zote huna habari na wakwe zako, unawasengenya, huwahudumii, huwaheshimu, unagombana nao, unawapenda kinafki tu, unafanya ili kutimiza wajibu tu, lakini hujitoi kwao, unaifikiria familia yako tu na ndugu zako…usitazamie kuwa Utabarikiwa uzao wako.

Biblia inakupa fundisho, litii ulifuate , watu wengi wenye matatizo ya ndoa huwa chimbuko ni hapo, pasipo hata wao kujua. Ikiwa humpendi mama wa mume wako, na usimpende na mume wako pia, lakini kama unampenda mume wako basi mpende na mama yake na ndugu zake ndipo utakapoishi kwa rah ana amani katika familia yako. Unaweza ukasema mimi ninaishi kwa raha, hao wakwe wananihusu nini..ni kweli utaishi leo kwa raha, lakini uzao wako unaweza usiishi kwa raha huko mbeleni..Na vile vile Maisha yako pia yanaweza yasiwe ya baraka.

Hiyo ni sheria ya Mungu ambayo ipo katika maandiko, ikiwa utataka kuwazaa akina YESE na Mfalme Daudi basi ambata na wakwe zako bega kwa bega, na kanuni hiyo itakulipa..Epuka mafundisho na injili za kwenda kupiga maadui zako, na kuwalenga wakwe zako..hapo utakuwa unazipiga baraka zako mwenyewe, utakuwa unajimaliza mwenyewe, ukidhani unajihami kumbe unajimaliza…Ukiona kuna kasoro Fulani ipeleke kwenye sala ukimwomba Mungu azidi kukupatanisha na wakwe zako sana, maana milango ya baraka zako ndio ipo huko.. siku zote zingatia hilo

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Asante sana kabisa kwa manene mazuri kabisa,somo lina sema wazi kabisa.ila Mungu atu saidiye kwe,ina onekana tume kuwa na fujo yingi kwenye ndo.sababu ni kwamba hatueshimu wakwe zetu.Mungu ani saidiye niwe kabisa nikate hatua.niwapende wakwe zangu!