Usikimbilie tarshishi hakuna uzima
Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio mwanga wa njia yetu na Taa iongozayo miguu yetu.
Kama ni msomaji wa biblia utakumbuka habari za Nabii Yona jinsi alivyoukimbia uso wa Bwana na kuelekea Tarshishi. Lakini umewahi kujiuliza TARSHISHI ulikuwa ni mji wa namna gani?…Ninawi tunaujua ndio uliokuwa mji mkuu wa Ashuru..lakini Tarshishi je!
Hebu kwa ufupi tujifunze juu ya huu mji na kisha tutapata jambo jipya ambalo linaweza kutusaidia katika nyakati hizi za hatari tunazoishi.
Mji wa Tarshishi ni mji ambao ulikuwa mahali panapoitwa Tiro..ambapo kwa sasa ni nchi ya Lebanoni…Nchi ya Lebanoni ni nchi iliyopo kaskazini mwa Israeli, kama vile Kenya ilivyo kaskazini mwa Tanzania (Na mpaka leo hiyo nchi inaitwa hivyo hivyo Lebanoni haijabadilika, inakaliwa na Waarabu sasahivi, lakini haina tena utajiri/ushupavu uliokuwa nao wakati ule)..
Sasa wakati wa vipindi vya wafalme wa Israeli nchi hii ya Tiro (Lebanoni) ambao mji wake mkuu ni Tarshishi ndio ulikuwa ni mji wa kibiashara mkubwa kuliko miji mingine yote. Ulikuwa unasifika kwa kuwa na MERIKEBU NYINGI ZA KIBIASHARA kuliko miji mingine yote. Na ulikuwa ni mji wenye uzoefu wa ki-biashara
Biblia inasema katika kitabu cha Ezekieli…
Ezekieli 27:12 “Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa”
Yeremia 10: 9 “Iko fedha iliyofuliwa ikawa mabamba, iliyoletwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi,….”.
Unaona? Vilevile Miti ya Mierezi ambayo ilitumika katika ujenzi wa hekalu la kwanza la Sulemani, ilitoka huko Lebanoni, kulikuwa hakuna mahali pengine ambapo miti hiyo ilikuwa inapatikana, na njia ya usafirishaji iliyokuwa inatumika kusafirishia miti hiyo ni bahari (Njia ya Maji). Kwa ufupi sehemu kubwa ya malighafi za ujenzi wa hekalu la kwanza la Sulemani zilitoka huko Tiro, ambao mji wake mkuu ni Tarshishi. Hata Dhahabu Sulemani alizozitumia kutengenezea vyombo vyake zilitoka huko Lebanoni..Sulemani alinunua dhahabu nyingi kutoka huko Lebanoni mpaka kufikia kiwango cha kuwa tajiri sana hata kuona kutumia madini ya fedha(silver) kutengenezea vito vyake ni kama kujishushia heshima..
1Wafalme 10: 21 “Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.
22 Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.
23 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.”
Huko Tarshishi walikuwepo pia manahodha waliobobea sana, na pia kulikuwa na watu wenye elimu ya ujenzi kubwa sana..baadhi ya wajenzi wa hekalu lile la mfalme Sulemani aliwatolea huko huko Lebanoni.
Hivyo ipo mistari mingi sana katika biblia inayoelezea ushupavu wa Tarshishi…ipo mingi sana unaweza kuipitia kwa muda wako upatapo nafasi…Kasome (Ezekieli 27: 25-27, Ezekieli 38:13, 1Wafalme 22: 48, ).
Sasa kwa kuielewa sifa ya Huu mji wa wa Tarshishi tunaweza kujua ni kwanini Yona alikimbilia huko…Na kwanini alipanda merikebu…Kumbuka kutoka Israeli mpaka Tarshishi(huko Lebanoni) kulikuwepo na njia ya nchi kavu nzuri tu..lakini yeye alikwenda kupanda merikebu. Ni sawa leo mtu atake kwenda Tanga..aache kupanda basi achague kutumia ferry/meli pale bandarini Dar es salaam aende Tanga. Ni lazima anayo sababu ya kufanya hivyo..
Na ni wazi kuwa sababu yenyewe si nyingine Zaidi ya biashara…Yona pengine alikuwa na mizigo yake anakwenda kufanya biashara.. Tarshishi haukuwa mji wa kitalii..ulikuwa ni mji wa kibiashara..hivyo alipoisikia sauti ya Mungu ikimwambia aende Ninawi kuhubiri yeye akaona njia pekee ya kuipotezea hiyo sauti ni kuzama kwenye biashara zake…wala hakuchagua kukimbilia miji mingine kama Misri, au Moabu ambayo angepata pumziko..yeye alikuwa na sababu ya kwenda Tarshishi.. Angalau apate riziki kidogo.
Lakini kama tunavyojua ni nini kilimtokea njiani. Biashara iliishia pale pale, wakapata hasara merikebuni kwa kutupa bidhaa zao majini kupunguza uzito.. na mtaji wote ukaishia palepale.
Sasa kitu cha muhimu cha kujifunza hapo ni nini?..Usiikimbie sauti ya Mungu leo inayokuambia fanya jambo fulani au tii jambo fulani, usiidharau sauti hiyo na kukimbilia kufanya biashara zako. Ni kama bahati tu Yona alipata neema mipango yake ilikatishwa katikati haikukamilika…..angeweza kuachwa aende huko anakokwenda na Mungu akamtafuta mtu mwingine wa kwenda Ninawi kuhubiri na watu wa Ninawi wakaokoka lakini Yona huko alikokimbilia akafanikiwa na utajiri wake lakini akafa na huku hajalitimiza kusudi la Mungu aliloletewa duniani, na mwisho wa siku kupotea katika ziwa la moto milele.
Hivyo leo isikie sauti ya Mungu lipo kusudi la wewe kuwepo hapa duniani la kufanya mapenzi ya Mungu.. usilikimbie kusudi hilo kwa kisingizio cha kufanya biashara, Hizo biashara ni za muhimu sawa..lakini kulitimiza kusudi la Mungu ni muhimu Zaidi..Una safari 5-6 za kwenda China kila mwezi lakini huna siku ya kukaa kufunga na kusali na kulitafakari Neno. Mwaka unapita hujawahi kufunga useme angalau nautafuta uso wa Mungu. Hujawahi kusema angalau mwezi huu wote sitasafiri nitajikita katika kutafuta kujua mapenzi ya Mungu kwangu…Unatengeneza pesa lakini hutengenezi hazina yako mbinguni..Nchi zinakujua, Benki zinakujua, lakini mbinguni hujulikani.
Watu wengi wananiambia, mtumishi ninatamani kujifunza Neno, wengine wanasema ninatamani kwenda kanisani lakini kazi zinanisonga, shughuli zinanifanya kuwa buzy,..Nataka nikuambie unayo hatari kubwa sana ya kuiokosa mbingu.
Unakimbilia Tarshishi unaiacha Ninawi?..Unakimbilia kufanya uwekezaji unasahau kutangaza habari za ufalme wa mbinguni..Kumbuka Neema aliyoipata Yona sio atakayoipata kila mtu. Simama katika nafasi yako muda ni mchache, usiruhusu mbegu yako kusongwa na kitu chochote.
Bwana atusaidie.
Ikiwa hujampa Kristo Maisha yako..na unakazana kuifuata njia ya Ninawi!..nakushauri geuka leo..Bwana Yesu alisema “Baba yetu wa mbinguni anajua kuwa tuna haja na hayo yote, bali tuutafute kwanza ufalme wake na haki yake, na hayo mengine yote tutazidishiwa”..Hivyo tubu leo kwa kukusudia kuacha dhambi, na kupunguza masumbufu ya Maisha haya ambayo yanakuvuta na kukusonga ukae mbali na Mungu wako.
Luka 21:34 “ Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, NA MASUMBUFU YA MAISHA HAYA; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.
36 Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu”.
Chukua hatua leo, na Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author