Bwana Yesu asifiwe..karibu tujifunze Biblia. Leo tutajifunza kwa kifupi mojawapo ya njia Mungu anazotumia kutuharakisha kwenda kwenye mafanikio yetu.
Kitu kimoja kinachotuzuia wengi wetu kusonga mbele ni HOFU…Chochote kile mtu afanyacho katika Maisha, endapo akiondoa hofu asilimia 100, basi ni rahisi sana kufanikiwa na kupiga hatua kubwa kwa haraka sana. Hata wafanyabiashara wengi waliofanikiwa kwa namna moja au nyingine ukiwafuatilia utaona ni watu waliojaribu kuondoa hofu na kujiingiza katika kazi Fulani yenye hatari kubwa ya kupata hasara (risk takers)…Na siku zote kazi yenye hatari kubwa ya kupata hasara ikifanikiwa huwa ndio ina matokeo makubwa kuliko ile yenye hatari kidogo. Kwahiyo hofu ndio kikwazo cha watu wengi…
Hali kadhalika kwa upande wa kiroho…Tatizo ni hilo hilo…Hofu!, Leo hii Bwana akikuambia kafanye kitu fulani ambacho kinaonekana hakijawahi kufanywa na kinaonekana kina hatari nyingi, kwa hofu ni rahisi kutokwenda kukifanya…
Hebu kwa ufupi tujifunze jambo kwa wana wa Israeli wakati wa safari yao ya kutoka Misri kwenda Kaanani.
Kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia utafahamu kuwa wakati wana wa Israeli wanatoka Misri, njiani walikutana na kipingamizi cha Bahari…Na Mungu alipanga kuipasua ile bahari mbele yao ili waivuke…Lakini kama tunavyojua moyo wa binadamu ni mgumu kuamini…Hebu jiulize endapo bahari ingepasuka mbele yao…halafu waambiwe wapite katikati ya ile bahari, bila msukumo wowote nyuma yao unadhani wangevuka????
Hebu jiweke wewe katika hiyo nafasi, umekuta bahari imefunguka kutoka ferry Dar es salaam na kuna njia imejitengeneza inakwenda mpaka Zanzibar halafu unaambiwa upite katikati ya hiyo bahari, huku pembeni unaona maji yamesimama kama ukuta..je utapita??? Jibu ni la! Hata kwa dawa hutapita..kwasababu utahisi pengine utakapofika katikati maji yatarudi yote na utaangamia….au utaanza kujihisi hisi una dhambi nyingi na hivyo endapo ukipita ukifika katikati Mungu atakuua…Sasa hiyo hali ya hofu na kuwazawaza ingeweza kukufanya usivuke kwenda Zanzibar hata kwa dawa!…Lakini hebu jiulize umeona simba anakuja nyuma yako kukufuata na njia ya kuokoka ni kupita katikati ya hiyo bahari je utaacha kupita?…
Na Bwana alilijua hilo…kwamba wana wa Israeli katika hali ya kawaida hawatavuka katikati ya ile bahari…Hivyo ili kuwalazimisha wavuke…alilileta jeshi la Farao makusudi nyuma yao….Na wana wa Israeli walipoona kuna jeshi la Farao linakuja nyuma yao, lenye mapanga na mikuki na hasira nyingi…Wakaona ile bahari si kitu mbele yao… ni heri kuingia kwenye haya maji kuliko kuchinjwa kama kuku huku tunajiona…Waliwajua wa-Misri jinsi wanavyoua kikatili…Hivyo wote kwa hofu ya kuwaogopa waMisri walijikuta wanaingia baharini bila wao kupenda tena huku wanakimbia,…na ghafla wakajikuta wameshatokezea upande wa pili bila madhara yoyote…
Ni hivyo hivyo hata leo, wakati mwingine Bwana akitaka kukuvusha na kukupeleka katika hatua nyingine…anafungua njia mbele yako ambayo kwa macho ya kawaida unaona huwezi kuvuka….Na pengine wakati unajishauri shauri kwamba utapitaje pitaje hapo, na kwamba ukijaribu utakufa! Au utapata hasara kubwa….ghafla Bwana mwenyewe anakuleta jeshi la ADUI nyuma yako, sasa lengo la lile jeshi sio kukumeza wewe…bali kukulazimisha uvuke hicho kiunzi kilichopo mbele yako, ili akakupe mafanikio mbeleni.
Ndicho kilichotokea hata wakati wa Esta?…Mungu alipotaka kuwabariki Israeli…kulikuwa hakuna namna nyingine zaidi ya kumnyanyua Hamani bin Hamedatha adui wa wayahudi….Lengo la yeye kumnyanyua vile ni ili kuharakisha baraka za wana wa Israeli..
Hivyo kama wewe ni mkristo usiogope uonapo jeshi la Adui limejipanga nyuma yako…na mbele ukitazama unaona Bahari…..Hapo usipaniki…ila tazama kwa makini hiyo bahari utaona kanjia chembamba cha nchi kavu….hako hako ndio kafuatie, usiogope mafuriko, hayatakumeza..hayo yamewekwa mahususi kwa Adui shetani na majeshi yake, na si kwaajili yako. Lakini hiyo ni endapo tu, moyoni mwako unaouhakika kuwa upo ndani ya Kristo.
Unapoona shida zimekuzingira na hakuna kupona, wakati mwingine madeni,n.k.…basi fahamu kuwa hapo ndipo wokovu upo mkubwa…Jeshi la Adui nyuma yako lenye kila silaha lisikufadhaishe…ni Bwana kalileta ili kukulazimisha wewe kupita katika ile njia iliyo nyembamba na hatari mbele yako ili utokezee upande wa pili kwenye baraka zako, usianze kufikiri kupambana na jeshi la shetani wala usianze kunung’unika, utapoteza muda wako na kumuudhi Mungu…wewe endelea mbele na tumaini lako lote liweke kwa Bwana na utauona wokovu wa Bwana na utanyamaza kimya kama Musa alivyowaambia wana wa Israeli.
Kutoka 14:10 “Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?
12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.
13 Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.
14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya”.
Lakini kinyume chake ni kwamba mkono wa Bwana hutaweza kuuona kama utakuwa sio miongoni wa walioitwa…kumbuka si watu wote waliokuwa duniani kipindi hicho ndio waliokuwa wanaona matendo ya Mungu kama hayo bali ni wana wa Israeli peke yao..na hiyo ni kwasababu hao ndio wan a wa Ahadi walioitwa!…Hivyo na sisi kama hatutakuwa katikati ya kundi la waliomwamini Yesu..kamwe tusitazamie kuuona mkono wa Bwana ukituokoa katika majaribu…Jeshi la Adui shetani litatushambulia na kutushinda siku zote. Lakini ni matumaini yangu kuwa wewe na mimi tupo ndani ya neema ya Kristo, hivyo Bwana ni mwokozi wetu na mtetezi wetu.
Maran atha
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU:
TAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE.
WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.
USISUBIRI MPAKA MUNGU AKUAMBIE, NDIO UFANYE!
NEEMA YA MZALIWA WA PILI.
UCHAWI WA BALAAMU.
About the author