WAKATI WA KRISTO KUSIMAMA,UMEKARIBIA SANA.

WAKATI WA KRISTO KUSIMAMA,UMEKARIBIA SANA.

Tunapaswa tujue, hichi kipindi tulichopo sasa ni kipindi gani, na hicho kinachokuja mbele yetu pia kitakuwa ni kipindi gani. Kwa ufupi ni kwamba Kristo sasa yupo mbinguni ameketi katika kiti chake cha neema, ikiwa na maana kuwa mlango wa neema upo wazi wakati wowote wa mtu yeyote kuingia muda wowote.

Lakini cha kuogopesha ni kuwa biblia ilishatabiri tangu zamani hata kabla Bwana Yesu mwenyewe hajazaliwa kuwa upo wakati wa yeye kusimama kutoka katika hicho kiti chake, na kama tunavyofahamu akisimama ni tendo gani linafuata..Jibu ni kuwa anakwenda kuufunga huo mlango ambao ulikuwa wazi kwa muda mrefu..

Zekaria 2:13 “Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za Bwana; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu”.

Biblia inasema hapo, Nyamazeni, maana yake wakati huo wakati utakapofika, Mungu atafumba vinywa hata vya watumishi wake, yaani kwa ufupi yatakuwa ni majira mengine, wakati huo kama mtu atakuwa bado yupo nje ya wokovu, basi hataweza kuupata tena wokovu, kwa jinsi mambo yatakavyokuwa yamebadilika wengi watatamani walau wautafute uso wa Mungu, lakini hawataupata kwasababu yule Roho Mtakatifu ambaye alikuwa ameachiliwa kushawishi mioyo ya watu wamwamini Yesu, ameshaondolewa.

2Wathesalonike 2:7 “ Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa”.

Na ndio maana Bwana Yesu mwenyewe alisema..

Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25 WAKATİ MWENYE NYUMBA ATAKAPOSİMAMA NA KUUFUNGA MLANGO, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; 26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje”.

Ndugu yangu ambaye upo nje ya mlango, wakati huo usidhani upo mbali sana, kumbuka siku moja inapopita ndivyo tunavyoikaribia siku yenyewe. Yaani jana ilikuwa ni mbali kuliko leo, Na cha kuogopesha zaidi Bwana Yesu alisema itakuja kwa ghafla sana kwa wasio amini.. Sasa kwanini mimi na wewe yatukute hayo yote, wakati sasa njia ipo wazi?..na inapatikana bure!, hutozwi chochote wala hulipishwi chochote??… Kumbuka Lengo la Kristo sikuzote ni kutuokoa sisi tuliopotea dhambini, hana lengo la kutuhukumu sisi, kinyume chake anataka atutengeneze maisha mema angali tukiwa bado hai muda huu, ili tuweze kuyarithi vizuri yale aliyotuandalia baada ya maisha haya. Anajua kuwa maisha ya hapa duniani ni mafupi, na yamejaa ubatili, na upotofu na ndio maana katuandalia maisha ya umilele baada ya kifo.

Hivyo ndugu yangu..kama hujaupokea wokovu basi huu ni wakati wako wa kufanya maamuzi, unachopaswa kufanya ni kwanza kudhamiria kwa moyo wako wote kumfuata Yesu, pasipo kusita-sita. Na hiyo inaambatana na kuacha dhambi. Hapa ndipo wengi wetu tunapokosea, kwasababu tunamtaka Yesu lakini hatutaki kuacha dhambi..Lakini tukiwa tayari kusema Ulimwengu nyuma yangu, na Kristo mbele yangu, kuanzia leo mimi na dhambi basii!.

Mungu akishaona tu moyo wako huo, moja kwa moja Kristo anaingia maishani mwako,..Hivyo dhamiria kwanza kufanya hivyo, kisha wewe mwenyewe piga magoti, mweleze Yesu makosa yako yote, na baada ya hapo mwombe msamaha kwa moyo wa kuugua kabisa.. Na kama utakuwa umefanya hivyo kwa kumaanisha, basi ipo amani ataileta katika maisha yako ambayo ndio itakuwa uthibitisho wa toba yako, sasa hiyo ni hatua ya kwanza,,

Hatua ya pili ni ubatizo, tafuta kanisa la kiroho karibu na wewe linaloamini ubatizo sahihi wa kimaandiko (yaani ule wa kuzamishwa kwenye maji tele na kwa jina la YESU Matendo 2:38)..Kisha nenda kabatizwe haraka iwezekanavyo, (Ubatizo ni bure hauhitaji gharama zozote, wala hauna tozo la fedha zozote, gharama zako ni toba yako na kujitoa kwako kwenda kuutafuta kwa bidii), Sasa ukishakamilisha vigezo hivyo, basi Kristo atamtuma Roho wake moyoni mwako kukuongoza katika safari yako ya wokovu tangu huo wakati hata milele.(Utaona ufahamu wako anaubadilisha kwa kiwango cha ajabu kwasababu umekubali kumtii).

Na mwisho ni jukumu lako kutafuta ndugu wa kikristo, na kuhudhuria ibadani, ili ukulie wokovu na kujifunza siri za Mungu, huku ukiingojea ile siku ya shangwe ya furaha ya kumlaki Bwana wetu Yesu mawinguni kama itakukuta ukiwa bado hai..Lakini kama utakuwa umelala basi, siku hiyo ikifika utafufuliwa wewe kwanza kisha utaungana na walio hai na kwa pamoja tutaanza safari ya kwenda kula karamu ya mwana kondoo aliyotuandalia mbinguni.

Lakini maadamu bado neema tunayo, tukumbuke tu Neno hili kuwa “siku ya mwenye nyumba kusimama imekaribia”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MPINGA-KRISTO

VUKA UJE MAKEDONIA UTUSAIDIE.

TUWATAFAKARI NZIGE WA JANGWANI.

FANYIKA SIPORA WA KRISTO, UNYAKUO UPO KARIBU.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments