Kwanini ukate tamaa ya kumtafuta Mungu? Nataka nikuambie hata Mungu mwenyewe akikuambia sikutaki haunifai, bado hupaswi kukata tamaa…
Kuna mbegu Fulani ya uharibifu ambayo shetani ameipanda ndani ya mioyo ya wakristo wengi, ambayo kuna hatua wanafikia ya kujiona kuwa hawafai tena mbele za Mungu, ya kujiona kuwa Mungu hawezi kuwa nao tena, ya kujiona kama hawastahili kwenda mbele za Mungu tena,….Hivyo wanaishia kukata tamaa ya kuendelea mbele pale wanapoona hata majibu ya maombi yao yanachelewa, nimekutana na watu wa namna hiyo wengi.
Lakini nataka nikuambie hupaswi kukata tamaa, wapo ambao Mungu alikuwa hana mpango nao,wengine hawakuwa hata wakristo, na wengine walikuwa wamesha muudhi Mungu kupindukia kwa kiwango cha juu sana mpaka Mungu kuwatamkia vifo, lakini katika uovu wao hawakukata tamaa ya kumkimbilia Mungu awarehemu, si Zaidi wewe ambaye ulishaokoka? Kwanini ukate tamaa?
Zaburi 107:10 “Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,
11 Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu.
12 Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.
13 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
14 Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao.
15 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu”.
Kumbuka Biblia ni kitabu kilichoandikwa ili kutuonya sisi, na kwa sehemu nyingine ili kututia nguvu, na kutufariji..
Kwa mfano embu mwangalie huyu mama ambaye hata wakati wake neema ya wokovu ilikuwa haijamfikia, alikuwa na miungu yake huko Tiro, pengine alipata hilo tatizo kutokana na dhambi zake kwa Mungu, lakini ilipofika wakati wa kutaka msaada kutoka kwa Mungu, hakujali “kutokujali kwa Mungu“, hakujali majibu makali kutoka kwa Mungu, bali aling’ang’ania mpaka akapata alichokuwa anakitafuta, haijalishi kuwa angeendelea kwenda kuiabudu miungu yake.
Mathayo 15:22 “Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.
27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.
Unaona tabia ya huyo mwanamke?, Mfano mwingine ni Mfalme Ahabu..Ambaye tunajua alikuwa ni mume wa yule mwanamke mchawi Yezebeli, biblia inasema huyu Ahabu alikuwa mfalme mwovu, kuliko wafalme wote waliomtangulia na alishiriki kuwakosesha sana Israeli mbele za Mungu (1Wafalme 21:25), mpaka ikafikia wakati Mungu akamwambia inatosha sasa..kufa utakufa, na nyumba yako itakuwa jaa..
Lakini Habari hizo mbaya kutoka kwa Mungu zilipomfikia, haikumfanya akate tamaa, na kusema sasa ndio basi!, Mungu hawezi tena kunitazama, badala yake alikwenda kujinyenyekeza..
1Wafalme 21: 27 “Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.
28 Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema,
29 Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake”..
Yupo na mwingine aliyetokea baada ya Ahabu, aliyeitwa Manase, Huyu ndiye alifanya mabaya Zaidi kuliko hata Ahabu na ndio aliyesababisha hata Mungu asiwasemehe Israeli tena, huyu alikuwa anawatoa mpaka Watoto wake kafara kwa kuwapitisha kwenye moto, alikuwa anakwenda kufanya uganga na mambo maovu kweli kweli..Mungu akachukizwa naye sana Ikiafikia hatua ya kuchukuliwa mateka kwa minyororo na pingu, na waashuru mpaka Babeli.
Lakini akiwa huko akijijua kuwa yeye ni adui wa kwanza wa Mungu, alijinyenyekeza kwa Mungu akamlilia sana mpaka akasikiwa..
2Nyakati 33:12 “Hata alipokuwa katika taabu, akamsihi Bwana, Mungu wake, akajinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.
13 Akamwomba; naye akamtakabali, akayasikia maombi yake; akamrudisha tena Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akajua ya kwamba Bwana ndiye Mungu”.
Sasa hiyo ni mifano michache ya watu ambao walikuwa ni waovu na wenye dhambi, ambao tayari walikuwa wameshahukumiwa tayari na Mungu kutokana na makosa yao..Lakini hawakukata tamaa, kujinyenyekeza kwake (sasa wewe kwanini ukate tamaa?)..Lakini sikuambii hivi ili na wewe ukafanye dhambi umwombe Mungu halafu akusikie hapana, hilo ni kosa.
Naandika hivi kwa ajili yako, wewe ambaye umeokoka, halafu unaona kama Mungu hawezi kukusikia, au hakujali.. Jiulize! tu kama Mungu Yehova alivisikia vilio vya wenye dhambi kama wakina Ahahu na Manase ambao walimkasirisha kwa kiwango kile, ataachaje kukusikia wewe ambaye, tayari ulishampa Maisha yako?..Anakusikia sana. Na anakuhurumia kuliko wewe unavyodhani, na anakujali, na anayasikia maombi yako…Hivyo huna sababu ya kukata tamaa?..Endelea mbele kumwamini na kumwomba kwa bidii.
Hebu soma tena hapa..
Zaburi 107: 4 “Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa.
5 Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.
6 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
7 Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa”.
Zaburi 105:8 “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema”
Nataka nikuambie ukiwa umeokoka, Bwana anakupenda na yupo karibu sana na wewe kuliko hata wenye dhambi, ukiwa umeokoka kilio chako mbele zake kinasikika Zaidi kuliko kilio cha akina Ahabu na Manase.., Hivyo endelea tu kumtafuata Mungu kwa bidii zote kwasababu wewe ni wa thamani nyingi kwake, wenye dhambi wasikushinde, ng’ang’ana na Bwana, popote pale, atakuwa na wewe wakati wote..
Wanaomtegemea Mungu, mwisho wao huwa unakuwa mzuri kama wa Ayubu.
Yakobo 5:11 “Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma”.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Je kualikwa kwenye sherehe za watu ambao si wakristo ni dhambi?
About the author