Jina la Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe daima.
Natumai u mzima, hivyo nakukaribisha tuyatafakari kwa pamoja maneno ya uzima ya Mungu wetu,.
Leo tutatazama tukio moja kati ya mengi yaliyokuwa yanaendelea kipindi kifupi kabla ya Kristo kuingia katika mateso makali ya kusulibiwa. Na tukio lenyewe ni lile na maadui wawili kukutana tena na kupatana…,Ambao ni Herode na Pilato.
Luka 23:11 “Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato.
12 Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao”.
Ulishawahi kujiuliza ni kwanini hawa watu wasipatanishwe na mambo mengine ya msingi mfano ya kidiplomasia, au ya kiuchumi, mpaka wapatanishwe na kukamatwa kwa mtu Fulani mwenye haki?. Utajiuliza Yesu alikuwa ana umuhimu gani kwao? Kwani ni yeye ndiye aliyewagombanisha? Kwanza wao walikuwa ni warumi Yesu ni myahudi, wao wapo Israeli kwa lengo la kutimiza mambo yao ya kiutawala na kuhakikisha nchi inastawi na kupeleka kodi nzuri kwa mkuu wao Kaisari aliyeko huko Rumi kwao, maelfu ya maili kutoka hapo walipo, Hivyo Yesu hakuwa na umuhimu wowote kwao, kwasababu yeye hakuwa mwanasiasa wala mfanyabiashara, au jasusi fulani..
Hivyo ukitazama kwa ukaribu utagundua kuwa muungano ule haukuwa wa kawaida, Bali ni muungano uliobuniwa na mamlaka tofauti na wanaoujua wao, na hiyo si nyingi zaidi ya ile ya mamlaka ya giza.
Na ndio maana kipindi kifupi kabla Bwana Yesu hajakamatwa kule Gethsemane, aliwaambia wale waliokuja kumkamata kuwa huu ndio WAKATI WA MAMLAKA YA GIZA kutenda kazi (soma Luka 22:52-53).
Mamlaka ya giza siku zote, ikitaka kuleta dhiki, huwa inafanya kazi ya kuwakutanisha na kuwapatanisha kwanza pamoja wakuu, hata wale maadui walioshindikana wa muda mrefu, inawapatanisha..Na inafanya hivyo ili kuongeza nguvu ya kutimiza azma yake ya maangamizi, na si kingine..
Na ndio maana, kipindi kile Kama Herode na Pilato wasingeungana, Bwana Yesu asingesulibiwa kwa namna yoyote ile, kwasababu amri ilipaswa iidhinishwe na pande zote mbili,. Na sio tu hao wafalme wawili waliungana, bali biblia inatuambia pia pamoja na mataifa, na watu wa Israeli ikiwemo waandishi na makuhani, waliungana pamoja ili kufanya shauri la kumwangamiza Kristo. Mpaka mafarisayo na Masadukayo ambao kutwa kuchwa walikuwa wakikinzana lakini waliungana kipindi hicho (Kasome Mathayo 22:34).
Matendo 4:25 “ nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili?
26 WAFALME WA DUNIA WAMEJIPANGA, NA WAKUU WAMEFANYA SHAURI PAMOJA Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.
27 MAANA NI KWELI, HERODE NA PONTIO PILATO PAMOJA NA MATAIFA NA WATU WA ISRAELI, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta”
Umeona hapo, timu ya kumwangamiza Yesu ilikuwa ni kubwa sana kuliko unavyoweza kudhani na sehemu kubwa ya hiyo ilikuja kwa kupatana kwa maadui.
Ndivyo itakavyokuwa katika dhiki kuu ndugu yangu. Roho ya mpinga-Kristo, itayakutanisha mataifa takribani yote ulimwenguni, na kitakachowakutanisha sio mikataba ya amani unayoiona leo hii inayosainiwa kila siku, sio makubaliano ya kiuchumi, wala sio mazungumzo ya kidiplomasia, hayo hayawezi kuipatanisha dunia hata kidogo, yameshafanyika mara nyingi huko nyuma, mpaka leo hii hakuna hata moja lililowezekana..
Kitakachokuja kuipatanisha dunia na kuwa na serikali moja ya makubaliano ambayo bila hiyo mtu hataweza, kuuza wala kununua, wala kuajiriwa itakuwa ni ya mamlaka ya giza, juu ya UKRISTO halisi ulimwenguni. Utajiuliza ukristo una nguvu gani mpaka uyasababishe mataifa yaungane?,
jibu ndio kama lile la Bwana Yesu, kwani yeye alikuwa na ushawishi gani mpaka Herode na Pilato maadui wa muda mrefu waungane,. Utagundua kuwa shetani ni lazima afanye hivyo ili atimize agenda yake vizuri.
Hapo ndipo wale ambao watakaokuwa wameukosa unyakuo, watayashuhudia haya, ghafla tu kutatokea visa visivyokuwa na mashiko ambavyo vitawalenga wakristo wale walioachwa kwenye unyakuo, na hivyo vitasababisha dunia nzima uinganishwe chini ya mfumo mmoja wa mpinga-kristo, Hapo ndipo kutakuwa na dhiki ambayo haijawahi kutokea tangu dunia iumbwe, na hiyo itawalenga wale wanawali vuguvugu waliokukosa unyakuo, ambao hawatakuwepo kwenye huo mfumo wao.
Mambo hayo ndugu yangu, yapo mlangoni kutokea, na yatakuja kwa ghafla sana, dalili karibia zote za mwisho wa dunia zimeshatimia, siku yoyote unyakuo utapita, na ndio maana Bwana Yesu anataka kutuepusha na huo wakati mbaya sana, wa kuharibiwa kwa ulimwengu.
Anasema,
Ufunuo 3:10 “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.
11 Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.
Je! tumejiwekaje tayari? Je na sisi tumelishika Neno la subira yake? Bwana Yesu akirudi usiku wa leo tunao uhakika wa kwenda naye mbinguni?. Kama hatuna uhakika huo, ni dhahiri kuwa tutababaki, hivyo ni heri tuyasalimishe maisha yetu kwa Bwana ayaokoe ndani ya hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho. Na yeye mwenyewe atahakikisha anatufikisha ng’ambo salama.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author