SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kumwambia mama yake, “Saa yangu haijawadia”?
Yohana 2:1 “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.
2 Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
3 Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.
4 Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia”.
JIBU: Saa anayoizungumzia hapo ni saa ya Yesu kutukuzwa duniani, lakini sio kutukuzwa tu peke yake, bali pia na siku ya mateso yake,
Sasa katika habari hiyo, Mama yake, alitazamia Yesu awasaidie wale watu kwenye shughuli yao waliyoiandaa, na bila shaka tarajio lake halikuwa Yesu atoe fedha au nguvu kazi, hapana tarajio lake lilikuwa ni Yesu afanye muujiza, na kwa tukio hilo Yesu atatukuzwa..Lakini Yesu kwa kulijua hilo alimkatiza mama yake, ni sawa na alimwambia mama unataka nitukuzwe kwa tendo hili?, Nina nini mimi nawe?, Saa yangu ya kutukuzwa haijafika, ikifika ni lazima nitukuzwe tu, lakini haitakuwa kutukuzwa kwa njia hii tu peke yake, bali itakuwa na mateso pia, kwasababu Hiyo nayo ni saa yangu.
Na ndio maana utaona katika matukio ya aina hizi mbili, Yesu alilisema neno hilo.
Tukio la kwanza ni pale walipotaka kumkamata ili kumuua , na alipokaribia kwenda msalabani alisema Neno hilo,
Yohana 7:30 “Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado”.
Akimaanisha saa yake ya mateso yenyewe haijaja..
Yohana 13:1 “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo”.
Kote huku akimaanisha saa ya mateso..
Yohana 12:27 “Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena”.
Unaona? Na sehemu ya pili ni pale, watu walipomtukuza sana, aliita ni saa yake, ambayo ndio hiyo mama yake alikuwa anaitazamia wakati ule, utaona baada ya kumfufua Lazaro, na watu wengi kutoka mataifa mbalimbali wakawa wanataka kuja kumuona, na watu wakamtandikia nguo zao, na miti ya mitende wakimwimbia Hosana kwa sauti kuu mpaka mji ukataharuki.. ndipo hapo alisema tena maneno hayo;
Yohana 12:21 “Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.
22 Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.
23 Naye Yesu akawajibu, akasema, SAA IMEFIKA ATUKUZWE MWANA WA ADAMU”.
Hivyo popote unapoona Yesu anasema SAA YANGU, jua anamaanisha saa ya kutukuzwa kwake, na saa ya mateso yake.
Amen.
Nasi pia tuna saa zetu hapa duniani, Mungu akitaka kututukuza, ni lazima kicheko na huzuni viambatane nasi, Yesu alitumia mfano wa SAA ya mwanamke azaapo kufananisha na saa zetu.
Yohana 16:21 “Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni.
22 Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye”.
Mhubiri 3: 1 Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.…..4 Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza”.
Bwana atusaidie, tuyatuambue majira yetu.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Je! mabalasi Bwana Yesu aliyoyatumia kugeuzia maji kuwa divai, yalitumika tu kwa kazi hiyo?
About the author