SIKU ZA WATUMISHI WA MUNGU.

SIKU ZA WATUMISHI WA MUNGU.

Luka 17:26  “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. 

27  Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.

28  Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; 

29  lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote”.

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe. 

Unabii huo ulitolewa na Bwana wetu Yesu mwenyewe kupitia kinywa chake, haukutolewa kwa kutumia kinywa cha  Mtume Paulo, au Yohana, au Petro au hata Luka mwenyewe aliyekiandika hichi kitabu, bali ni Bwana mwenyewe ndiye aliyeutoa…akilelezea jinsi ujio wake unavyofananishwa.

Katika unabii huo aliufananisha na siku za Nuhu pamoja na za Lutu. Sasa pamoja na mengi aliyoyafananisha kwamba watu watakuwa wakioa na kuolewa (ndoa za jinsia moja), watu watakuwa wakila na kunywa (karamu za ulafi pamoja na ulevi)kama nyakati za Nuhu, pia katika siku za ujio wake watu watakuwa wakiuza na kununua (biashara haramu na za magendo) kama ilivyokuwa nyakati za Lutu

Lakini pamoja na hayo yote ambayo mengi ya hayo yameshatimia..kuna vipengele viwili ningependa tuvione katika mistari hiyo, ambavyo ukiisoma kwa haraka haraka ni rahisi kuvipita tu. Na vipengele hivyo ni 1) KAMA ZILIVYOKUWA SIKU ZA NUHU na 2) KAMA ZILIVYOKUWA SIKU ZA LUTU

Katika vipengele hivyo hakusema “kama zilivyokuwa siku za gharika, au kama zilivyokuwa siku za maangamizi ya moto ya Sodoma na Gomora”..Bali utaona anatumia siku za Nuhu na siku za Lutu…

Sasa Nuhu na Lutu walikuwa ni watumishi wa Mungu.. Kwasababu walionywa na Mungu juu ya maangamizi yanayokuja mbeleni na pia wakapewa nafasi ya kwenda kuwahubiria wengine.

Lutu kabla ya kutolewa Sodoma, alihubiriwa na wale malaika wawili mambo yatakayokwenda kutokea kipindi kifupi mbele na akapewa nafasi ya kwenda kuwahubiria wakwe zake, na ndugu zake pia, ikiwemo mke wake, wanawe wawili na ndugu zake.. Waliokubali ni mke wake pamoja na wanawe wawili, wengine walimwona kama kikaragosi tu kinacholeta habari za mababu.

Mwanzo 19:12 “Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; 

 13 maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za Bwana; naye Bwana ametupeleka tupaharibu. 

 14 Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu Bwana atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze”

Vivyo hivyo Nuhu kabla ya kuingia safinani alihubiriwa na Mungu juu ya hukumu itakayokwenda kutokea kipindi kifupi mbele, na pia akapewa nafasi ya kwenda kuwahubiria ndugu zake, lakini waliokubali kuambatana naye ni mke wake na wanawe watatu, pamoja na wake za wanawe, jumla watu 8 tu..wengine wote walimwona kama fundi mbao aliyerukwa na akili.

Hivyo utaona hapa Bwana Yesu anazitaja kama siku ni ZAO.. Na anazifananisha na siku za ujio wake.. Maana yake ni kwamba siku za ujio wake, atawanyanyua watumishi wake mfano wa Nuhu na Lutu kuonya ulimwengu juu ya hukumu ijayo.

Ndugu..hukumu ipo!.. Wakina Nuhu wapo wengi leo, katika kila Taifa na mkoa..(Watumishi wote wanaouonya ulimwengu juu ya siku za mwisho ni wakina Nuhu na Lutu), na hizi ndizo siku zao… “zinaitwa Siku za Hao watumishi” na sio “siku za kuangamizwa dunia”..Lutu alionekana anacheza mbele za wakwe zake.

Kibaya zaidi ni kwamba, watu wengi watakaokuwa wanasikia habari hizo wataoana kama wanacheza tu nao pia, wanapiga ngonjera, wamekosa kazi ya kufanya,.Lakini mwisho utakapowakuta kwa ghafla ndipo watakajuta majuto yasiyoelezeka…

Ukiona unasikia habari za mwisho wa dunia kwa nguvu, jua ndio injili ya kumalizia hiyo, baada ya hapo ni hukumu. Hizi ni siku za mwisho, siku za Watumishi wa Mungu..Na zitaisha!

Je umempokea Kristo? Kwa kutubu na kubatizwa?.. kama bado unasubiri nini?.. Yesu yu karibu kurudi, hivi karibuni hutasikia tena ukiombwa uingie ndani ya safina, hutasikia tena sauti ya Roho Mtakatifu ikikushawishi kutubu..kutakuwa na ukimya nje na ndani, mlango wa Neema utakuwa umeshafungwa, kitakachobakia ni hukumu..

Watu wa kipindi cha Nuhu walisubiri Mungu azungumze nao pengine kwa kutumia jua ndipo waamini, hivyo wakaishia kumdharau Nuhu, vivyo hivyo wa kipindi cha Lutu. Wakati huu ambao watu wanaidharau injili ya kurudi kwa Kristo, hatupaswi kufanana na  wao hata kidogo.

Hivyo ndugu mpokee Kristo leo kama hujafanya hivyo, kisha nenda katafute ubatizo sahihi wa maji mengi (Yohana 3:23) na kwa Jina la YESU, ambalo ndio jina la Baba, mwana na Roho Mtakatifu (Matendo 2:38, Mathayo 28:19), na kuanzia wakati huo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukuongoza na kukutia katika kweli yote ya maandiko.. Na utaiepuka hukumu ambayo ipo karibuni kuujilia ulimwengu wote.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

SIKU ZA MWISHO WA DUNIA.

Naomba kujua watakaoenda mbinguni je! ni wengi au wachache?

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

JINSI DHAMBI INAVYOMGHARIMU MTU SANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments