Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lizidi kubarikiwa.
Karibu tujifunze Neno la Mungu wetu.
Kama ni msomaji mzuri wa Biblia utakuwa unayajua majaribu matatu ya Yesu aliyojaribiwa na Ibilisi kule jangwani. Jambo la ajabu ni kwamba shetani hakwenda kumjaribu Bwana Yesu kwa uchawi, au kwa magonjwa au kwa maneno yake, bali alikwenda kumjaribu kwa kutumia maandiko matakatifu.
Maana yake ni kwamba kitengo kikubwa cha Majaribu ya shetani kwa mkristo hakipo kwa wachawi, au kwa waganga wa kienyeji kama watu wengi wanavyofikiri, BALİ KİPO KATİKA NENO LA MUNGU. Na shetani hatumii nguvu nyingi kututumia majeshi ya wachawi wake kama unavyohubiriwa na watu, bali anatumia nguvu kubwa kuhakikisha kwamba hulielewi Neno la Mungu, na hapo akifanikiwa basi unakua umekwisha!.. Bwana wetu Yesu asingekuwa analijua Neno kweli kweli, basi asingemweza shetani kamwe..Lakini shetani hakumweza kwasababu yeye ndio aliyekuwa Neno mwenyewe.
Wengi wetu tunakosa shabaha hapo, Tukidhani uadui mkubwa wa shetani kwetu ni waganga wa kienyeji na wachawi wanaotuzunguka…jambo linalompelekea Mkristo kutwa kuchwa kupambana na wachawi katika maombi.. Na kusahau kuwa silaha yake kubwa ni Neno la Mungu (Ndio upanga) Waefeso 6:17. Na pasipo kujua kuwa asipokuwa na Neno la Mungu la kutosha ndani yake basi tayari anakuwa kalogwa na shetani siku nyingi (Wagalatia 3:1)..Hata kama atakuwa anasali na kupiga maombi ya vita kila siku.
Sasa hebu tusome kwa ufupi jinsi Bwana alivyomjibu shetani katika yale majaribu na kisha tutajifunza kitu cha muhimu sana. Usipite hata kama ulishasoma rudia tena.
Mathayo 4:1 “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. 2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. 4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. 5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu 6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. 7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. 8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, 9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. 10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. 11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia”
Mathayo 4:1 “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.
2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.
3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.
4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu
6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.
8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,
9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.
10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.
11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia”
Kama tunavyojua maneno yote shetani aliyomwambia Bwana Yesu hapo , hayakuwa ya UONGO! Yote yalikuwa ya kweli na yapo katika biblia, yalikuwa ni maneno ya Mungu yenye pumzi ya uhai (hivyo upo ukweli unaopotosha)…na yote shetani aliyatoa katika biblia..Kwamfano hilo Neno “Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua” Ni Neno la Zaburi 91:12.
Lakini shetani aliyapindisha yale maneno na kuyafanya yatumike mahali ambapo sio sahihi, na kwa wakati usio sahihi. Maneno ya Mungu yakitumika mahali ambapo sio sahihi na kwa wakati ambao sio sahihi yanakuwa ni sumu kubwa.
Kwamfano Neno la Mungu ni kweli linasema.. “waume waishi na wake zao kwa akili na kumpa mke heshima (1Petro 3:7)”..Sasa Neno hili linawahusu Wanaume waliooa ndoa halali ya kimaandiko…Na si mtu yeyote tu hata anayeishi na girlfriend wake. Nimewahi kukutana na watu wanaoishi pasipo kuonana na wanautumia huu mstari kwa madai kwamba Mungu amesema “tuishi na wake kwa akili”. Nimewahi kukutana na mwingine akiwashawishi wanawake kufanya nao uzinzi huku akitumia hichi kipengele cha maandiko.. 1Wakorintho 7:5 “Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”.
Hivyo mwanamke yeyote anayekutana naye anakimbilia kumwonyesha huu mstari, na kusema hata Mungu amesema “tusinyimane” na amefanikiwa kuwanasa mabinti wengi kwa andiko halo…Pasipo kufahamu kuwa hilo andiko linawahusu wana-ndoa tu!(watu ambao tayari wameoana) na sio kila mtu tu!.
Sasa shetani alimjia Yesu kwa njama hiyo hiyo, kuyaweka maneno ya Mungu mahali pasipopaswa na kwa wakati usiofaa.
Anamwambia Bwana ajitupe chini na Mungu atamwagizia malaika waje wamchukue asijikwae…Ni kweli hilo ni Neno la Mungu, lakini huo sio wakati wake..Neno hilo litafaa kutumika wakati ambao tumejikuta tumeingia majaribuni au hatarini pasipo hiari yetu, huo ndio wakati wa Bwana kuwaagiza malaika zake watuchukue. Lakini sio wakati ambao tupo salama halafu tunamjaribu Mungu tuone atafanya nini, tukifanya hivyo tunajitafutia laana badala ya baraka..
Na sisi tunapaswa tujifunze KULIGAWANYA VYEMA NENO LA MUNGU. Na hiyo inakuja kwa kulisoma Neno la Mungu kwa bidii. Ukisoma kijimstari kimoja tu na kwenda kulala! Ni rahisi kushindwa kuyagawanya Maneno ya Mungu ipasavyo..
Na pia usitumie nguvu kubwa kuchunguza mchawi wako ni nani?.. Tumia nguvu kubwa kuyachunguza maandiko!!…Je biblia inasema nini katika hali hiyo unayopitia?..Je katika biblia kuliwahi kutokea kisa kama hicho unachopitia na je kilitatuliwaje?.. Unapoona kuna kitu fulani hakipo sawa, tafuta kujua je! Biblia inasemaje kuhusu hiyo hali.. Usisubiri kufundishwa-fundishwa biblia, jifunze kuisoma mwenyewe..Utakutana na mambo mengi huko, ambayo hata mchungaji wako hawezi kukuhubiria, na pia utagundua ni vitu gani ulikuwa unapotoshwa na vitu gani ulikuwa unaambiwa ukweli.
Lakini ukisubiri tu kila somo unalokutana nalo mitandanoni, ni kulisoma tu, kwasababu mtumishi yule anaaminika na wengi!, au kila hubiri ni kusikiliza tu kwasababu mtumishi yule anasifiwa na wengi. Nataka nikuambie, utaishia kukosa mahali pa kusimamia, utakuwa ni mtu wa kupepesuka daima. Na kutufuta mchawi ni nani kwenye ukoo wako, kumbe uchawi ni kukosa kwako maarifa ya Neno la Mungu.
Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;..”
Soma Biblia mwenyewe huo ndio uthibitisho wa kwanza wa kwamba umeamua kuanza safari ya kumjua Mungu.
Na Bwana akubariki
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
JINSI YA KUSOMA BIBLIA.
KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?
UPONYAJI WA ASILI
JIOKOE WEWE NA NYUMBA YAKO.
MASOMO MBALIMBALI YA NENO LA MUNGU.
Je! Mwanamke anapaswa afunikwe kichwa anapokuwa ibadani?
UNYAKUO.
Rudi Nyumbani:
Print this post