Jina la Bwana wetu na Mwokozi wetu, Yesu Kristo libarikiwe…Karibu katika kuyatafakari maandiko, tumekwisha kuvipitia vitabu kadhaa vya Mwanzo, naomba kama hujavipitia na ungependa kuvipitia, basi fungua hapa >> VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1
Leo kwa neema za Bwana tutasonga mbele kitabu kingine kimoja, ambacho ni kitabu cha Zaburi.
Kitabu cha Zaburi ndio kitabu kirefu kuliko vitabu vyote katika biblia, na ndio kitabu ambacho kipo katikati ya Biblia. Sehemu kubwa ya kitabu hichi imeandikwa na Mfalme Daudi, mwana wa Yese. Lakini sio Milango yote imeandikwa na Daudi, la!..milango mingine imeandikwa na Sulemani, Mfalme Hezekia, Asafu,Musa, Ethani na Hemani.
Kitabu hichi kimeandikwa katika mfumo wa beti za nyimbo. Kwasababu maana tu ya neno lenyewe Zaburi ni “Nyimbo takatifu zilizoimbwa kwa vyombo vya muziki vya nyuzi nyuzi, kama vile santuri, kinubi na zeze”. Kama utapenda kuvijua vyombo hivyo vya nyuzi nyuzi vya muziki kwa urefu utatutumie ujumbe inbox.
Hivyo nyimbo hizi za Zaburi, ziliandikwa si kwa lengo la kuburudisha bali kwa lengo la kumshukuru Mungu, kumtukuza Mungu, kumwomba Mungu, kumsifu Mungu, kuomba ulinzi na haki .
Mfalme Daudi alizitunga nyimbo hizi katika kipindi chote cha maisha yake aliyoishi (yaani miaka 70). Hivyo hakikuandikwa kwa siku moja, au wiki moja. Kila hatua ya maisha Daudi aliyoipitia Roho ya Mungu ilishuka juu yake na kumsukuma kuandika beti za nyimbo hizo, ambazo leo tunazisoma katika biblia.
Sasa swali ni kwanini zimeandikwa katika mfumo wa Nyimbo?
Ikumbukwe kuwa Daudi tangu akiwa mdogo alikuwa na kipaji cha kupiga filimbi na kinubi..Hivyo alijifunza kumwimbia Mungu tangu akiwa mdogo, na kipaji chake hicho Mungu alichompa, kuna kipindi kilivuma mpaka hadi kikamfikia Mfalme Sauli..
1Samweli 16:14 “Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua.
15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona.
17 Basi Sauli akawaambia, VEMA, NITAFUTIENI MTU ALIYE STADI WA KUPIGA KINUBI, MKANILETEE.
18 Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, ALIYE STADI WA KUPIGA KINUBI, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye Bwana yu pamoja naye.
19 Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo……….
23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, NDIPO DAUDI AKAKISHIKA KINUBI, AKAKIPIGA KWA MKONO WAKE, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha”.
Hivyo kipaji hicho cha kupiga vinubi na kuimba, alichokuwa nacho Daudi, aliendelea kukitumia mpaka anaondoka Duniani.
Sasa ni Mazingira gani aliyokuwa mfalme Daudi wakati anaandika hizo Zaburi.
Daudi hakuwa anakaa tu ndani, na ghafla anaanza kujikuta anaandika nyimbo hizo. Hapana, mfano wa mazingira aliyokuwa anaandika beti hizo, ni wakati labda ametoka vitani na Mungu kampa ushindi dhidi ya maadui zake ambao pengine walikuwa ni hodari kupita wao, hivyo ile furaha anayoipata na huku anaona kama sio Mungu wasingeshinda, ile furaha inamsukuma kuandika nyimbo za kumshukuru Mungu.
Kwamfano hebu tuziangalie beti chache za Daudi katika Zaburi kasha tuzitafute ziliandikwa kipindi gani.
Tuanze na Zaburi ya 105, inasema hivi..
Zaburi 105:1 “Haleluya. Mshukuruni Bwana,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake.
2 Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.
3 Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
4 Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote ”
Je ni kwamba Daudi alikaa tu ndani?..na akachukua tu kalamu na karatasi kuandika ubeti huo?..Jibu ni la!..Ubeti huo uliandikwa kipindi Mfalme Daudi Analitoa sanduku la Agano kwa Obed-odemu kwenda mjini kwake yaani (Yerusalemu).. Hivyo kwa furaha kubwa wakati sanduku la agano linaingia tu mjini mwake, alicheza mpaka nguo zikamtoka, na alilisindikiza Sanduku hilo la agano, kwa nyimbo nyingi za santuri na vinubi…
Tusome…
1Nyakati 15:25 “ Basi Daudi, na wazee wa Israeli, na maakida wa maelfu, wakaenda, ili kulipandisha sanduku la agano la Bwana kutoka nyumbani mwa Obed-edomu kwa furaha kuu;
26 hata ikawa, Mungu alipowajalia Walawi waliolichukua sanduku la agano la Bwana, wakachinja ng’ombe saba, na kondoo waume saba.
27 Naye Daudi alikuwa amevaa joho ya kitani safi, na Walawi wote waliolichukua sanduku, na waimbaji, na Kenania msimamizi wa uchukuzi, na waimbaji; naye Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.
28 Ndivyo Israeli wote walivyolipandisha sanduku la agano la Bwana kwa shangwe na kwa sauti ya tarumbeta, na kwa baragumu, na kwa matoazi, wakipiga sauti kuu kwa vinanda na vinubi.
29 Hata ikawa, sanduku la agano la Bwana lilipofika mjini kwa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi, akicheza na kushangilia; akamdharau moyoni mwake”.
Sasa tukiendelea mlango wa 16 kuanzia mstari wa 9 ndiyo tunaiona Zaburi hiyo ya 105 ilipotokea.
Tusome..
1Nyakati 16:1 “Wakaliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu.
2 Na Daudi alipokwisha kuitoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani, akawabariki watu kwa jina la Bwana.
3 Kisha akawagawia kila mtu wa Israeli, waume kwa wake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu.
4 Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la Bwana, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, Bwana, Mungu wa Israeli;
5 Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Matithiya, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi;
6 nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la agano la Mungu. 7 Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru Bwana, kwa mkono wa Asafu na nduguze.
8 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake.
9 Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi; Zitafakarini ajabu zake zote.
10 Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
11 Mtakeni Bwana na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote.
12 Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake;
13 Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
14 Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake.
15 Likumbukeni agano lake milele, Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. 16 Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka;
17 Alilomthibitishia Yakobo kuwa amri, Na Israeli liwe agano la milele”
Umeona?..Kwahiyo Zaburi hazikutungwa tu pasipo sababu yoyote, bali zilitungwa kila baada ya tukio fulani la ki-Mungu lililotokea katika maisha ya Daudi. Zaburi zote 150, zilindikwa kwa msukumo wa Roho baada ya tukio fulani la ki-Mungu.
Zaburi nyingine Daudi aliziandika, baada ya kuokoka kimiujiza kwenye mikono ya Sauli aliyekuwa anatafuta kumuua, hivyo akaandika nyimbo hizo kumshukuru Mungu. Na sehemu kubwa ya Zaburi ya Daudi aliandika baada ya kupata ushindi dhidi ya Maadui zake (Yaani mataifa yaliyokuwa yanafanya vita dhidi ya Israeli)
Lakini pamoja na hayo nyimbo hizo za Zaburi, licha tu ni nyimbo katika mfumo wa maombi, shukrani, sifa n.k. kwa Mungu lakini pia zina unabii ndani yake.
Na unabii wa kwanza na Mkuu ziliobeba ni unabii wa kuja kwa Masihi, yaani Yesu Kristo, na unabii wa Wana wa Israeli kuchukuliwa mateka Babeli.
Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake”. Linganisha na maneno ya Bwana Yesu katika Yohana 13:18
Yohana 13:18 “Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate kutimizwa, Aliyekula chakula changu Ameniinulia kisigino chake”.
Zaburi 22:18 “Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura”…Linganisha na Mathayo 27:35
Hivyo kitabu hiki kwa sehemu kubwa kimebeba Ufunuo juu ya Yesu..Ndio maana Baada ya Yesu kufufuka alitaja kuwa yote aliyoandikiwa katika Zaburi na torati lazima yatimie..
Luka 24:44 “Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi”
Mbali na hayo, Kitabu cha Zaburi kinatufundisha Mambo yafuatayo.
Bwana akubariki.
Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata…
Maran atha!
Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author