Biblia inatuambia kuwa viumbe vya Mungu navyo vinaugua, na vinapitia shida kama sisi tu tunavyopitia..
Warumi 8:22 “Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa”.
Hivyo kama vinaugua kama sisi, vinaumia kama sisi, ni kosa kuvipiga au kuviua bila sababu yoyote.
Biblia imetoa sababu kuu mbili ya kuviua au kuviadhibu.
Ya kwanza ni pale tunapovitumia kwa chakula, au kwa matumizi ya msingi: (Kumbukumbu 12:15). Utachinja kuku, au ng’ombe, au mnyama yoyote ikiwa ni kwa lengo la kula, au biashara,..Hiyo sio dhambi wala sio kosa.
Na sababu ya pili ni pale, vinapofanya makosa, au vitatusababishia madhara au hasara: Utalisoma hilo katika (Kutoka 21:28-29). Vilevile kuna viumbe kama nyoka, mende, nzi, mbu, kunguni, n.k. hivyo vikiuliwa hakuna shida, kwasababu havina kazi nyingine yoyote zaidi ya kutuletea magonjwa au kutudhuru.
Lakini kwasababu nyingine yoyote nje ya hizo ni dhambi.
Utalithibitisha hilo kwa Balaamu, siku ile alipokuwa anamfuata Balaki mfalme wa Moabu, Ili awalaani Israeli, utaona Mungu alipomfumbua macho punda yule na kumwona yule malaika, Balaamu alianza kumpiga, na yule punda akafumbuliwa kinywa na Mungu, akamwambia unanipigia nini? (Hesabu 22:21-39)
Na kama hiyo haitoshi yule malaika naye alikuja kumuuliza tena Balaamu kwanini alimpiga punda bila kosa lolote? Unaona, Mungu hapendi tuvitese viumbe vyake, bila sababu yoyote. Sio lazima ukimkuta mbwa barabarani ambaye kakaa tu bila kosa lolote, wala dhara lolote, uanze kumpiga kwa mawe.
Si vizuri ukamkuta kinyonga katulia zake pale mtini, uanze kumlenga kwa manati, Si vizuri ukamwona punda wako amechoka katulia, ukaanza kumpiga piga ovyo tu bila sababu..Hiyo ni dhambi.
Biblia sehemu nyingine inatoa thawabu nono sana kwa wanaowatenda fadhili wanyama..Soma hapa.
Kumbukumbu 22:6 “Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;
7 sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi”.
Unaona, kwa mambo madogo tu, mtu unajiongezea siku za kuishi.
Hivyo, ikiwa hatuna sababu zozote za msingi, tusivipige au kuviua viumbe vya Mungu.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Katika Warumi 8:18-25. Je! Viumbe vinatazamiaje kwa shauku kufunuliwa kwa Mwana wa MUNGU?
Je! ni kweli kuna viumbe vinavyoishi sayari nyingine (ALIENS)?
Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?
Fadhili ni nini? Nini maana ya “fadhili zake ni za milele” kibiblia?
About the author