Wakati mwingine Mungu anatumia njia za dhahiri kabisa kufunua yale yanayoendelea rohoni. Kwamfano utaona wakati ule Yesu anakutana na yule kichaa, na kuyaamuru yale mapepo yamtoke, tukio lililofuata baada ya pale ni wale nguruwe kupelekwa moja kwa moja ziwani na yale mapepo na kuuliwa huko. Hiyo ni kufunua kuwa mapepo hayana malengo mengine zaidi ya kuua tu na kuangamiza, wala hakuna pepo zuri au jini zuri kama watu wa dini nyingine wanavyodhani, maadamu una pepo ndani yako, basi ujue lengo lao ni moja, kukuangamiza tu.
Na ndio maana utaona lile pepo ambalo wanafunzi wa Yesu walishindwa kulitoa, baba wa yule kijana alisema, mara nyingi linamtupa mwanangu kwenye maji..mara nyingine kwenye moto(Marko 9:22)..Fikiria wewe unadhani lengo lake lilikuwa ni nini kama sio kumwangamiza. Hivyo hata leo hii, ukiwa na pepo la uzinzi, ujue kuwa shabaha ni wewe ukutane na ukimwi, ufe kabla ya wakati wako, au hata ukumbane na mabalaa mengi mengi yasiyoeleweka,ili tu uondoke katika hali ya dhambi ujikute kuzimu.
Sasa, tukirudi katika habari ya mwanzo, tulisema Mungu huwa anaruhusu wakati mwingine mambo Fulani yaonekane kwa dhahiri ili kufunua hali halisi ya mtu ilivyo rohoni.
Sehemu nyingine tena utaona ni pale mtume Paulo, alipokutana na Yesu alipokuwa anaelekea Dameski kufanya kazi yake ya kuliharibu kanisa la Mungu, Na Bwana alipomtokea kama tunavyojua habari, ni kuwa nuru ya Yesu ilimwangazia pande zote, sasa kutokana na kuwa nuru ile ilikuwa kali, ilimfanya awe kipofu wa muda. Mpaka alipokwenda kuombewa na mtu mmoja aliyeitwa Anania baada ya siku tatu ndipo akaona tena.
Lakini baada ya kuombewa kwake, biblia inatuambia, vitu kama magamba vilidondoka machoni pake. Tusome.
Matendo 9:17 “Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
18 MARA VIKAANGUKA MACHONI PAKE VITU KAMA MAGAMBA, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;
19 akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.
haya magamba yalikuwa kwenye macho ya Paulo sikuzote lakini hakuwahi kuyajua, mpaka siku anaombewa na kudondoka ndipo anajua kitu hicho kilikuwa
Hiyo ilikuwa inafunua hali halisi ya Paulo ilivyokuwa rohoni. Alikuwa amepofushwa kikweli kweli na shetani, kwa kuwekewa haya magamba ya adui, bila hata ya yeye maskini kujijua.
Sasa haya magamba ya adui yapoje?
Haya, hayana malengo ya kuziba kila mahali katika maisha ya mtu hapana, haya yapo mahususi kukuziba lile eneo linalohusiana na kumjua Mungu. Unaweza ukawa na elimu yako nzuri, unaweza ukawa na hata na fedha nyingi, lakini unaweza ukashindwa kuiona njia Ya wokovu wa Mungu.
Pengine utakuwa mwepesi hata katika kufanya mambo mengine yote, utakuwa mwepesi kuelewa hata kanuni nyingine za maisha ya kila siku, lakini utakosa wepesi wa kuifahamu njia ya wokovu.
Ukihubiriwa habari za msalaba, kwako zinakuwa kama ni habari za kishamba vile, hata ukielezwa habari za kuzimu hazikushtui tena, haijalishi utatolewa na shuhuda nyingi kiasi gani, kwako ni kawaida tu, na ndio maana unaendelea na ulevi wako na uzinzi wako badi leo hii, sasa ukiona upo katika hali hiyo basi ufahamu magamba hayo ya rohoni yameshawekwa kwenye macho yako pasipo wewe kujijua. Pengine ulichobakiwa nacho ni kuisifia tu dini yako.
Na hali hiyo inaweza kuwa mbaya kiasi kwamba ukawa hata unaupinga wokovu, na kufanya vita nao kama ilivyokuwa kwa Paulo…Lakini jiulize unadhani Paulo alikuwa amekusudiwa kuwa mtu wa namna ile, ? Jibu ni hapana, ndio maana baada ya kuondolewa magamba hayo, akaupenda wokovu kwa namna isiyo ya kawaida, akawa mhubiri nambari moja wa njia ya wokovu.
Hii ni kazi ambayo shetani anaifanya kila kukicha, watu wanapofushwa macho yao ya rohoni, wasimjue Mungu, au wasione umuhimu wa wokovu, angali wakiwa bado hapa duniani.
2Wakorintho 4:3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.
Magamba haya ukiyaendekeza ndani ya maisha yako, madhara yake utakuja kuyaona baada ya kifo. Kwasababu siku utakapokufa moja kwa moja utajikuta kule kuzimu, Na wewe huko utakuwa katika majuto yasiyokoma, kama ya yule tajiri wa Lazaro(Luka 16:19-31)… Mahali ambapo aliomba sana ndugu zake wasifike huko..
Ndugu yangu watu wanaoshuka kuzimu kila siku idadi yake haihesabiki, na wote huko laiti tungeonyeshwa hali zao zilivyo, jinsi wanavyojuta, jinsi wanavyosema tulipofushwa kiasi gani mpaka tukaudharau msalaba, na leo tupo hapa, tusingeuchukulia wokovu wetu juu juu tu. Hivyo tubu dhambi zako, mgeukie Kristo, na yeye atakuokoa. Epuka magamba haya ya ibilisi.
Kwasababu siku hizi ni za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine:
Mada Nyinginezo:
About the author