Ni kweli mizimu ipo?, Na tunawezaje kujihadhari nayo?.
Katika tafsiri inayojulikana na wengi ni kwamba Mzimu/Mizimu ni roho za watu waliokufa ambazo zinaweza kurudi na kuwatokea wengi.
Roho hizo zinaweza kurudi zenyewe au kurudishwa na mtu, kwa lengo fulani, aidha kutatua tatizo lililoshindikana katikati ya mtu au jamii ya watu, au kujilipiza kisasi kwa mambo aliyofanyiwa mtu huyo kabla ya kufa.
Lakini je! Kibiblia MIZIMU ni kweli ipo?
Jibu ni la! Hakuna roho yoyote ya mtu aliyekufa, inayoweza kurudi yenyewe au kurudishwa na mtu, na kisha kutatua jambo fulani la kimaisha.
Jambo hilo liliwezekana kwa sehemu katika agano la kale kabla ya Bwana Yesu kuja, shetani alikuwa na uwezo wa kuzipandisha juu za watu waliokufa. Utaona katika maandiko aliweza kumpandisha juu nabii Samweli (1Samweli 28:11-14).
Lakini katika agano jipya, baada ya Bwana Yesu kushuka kuzimu na kuzichukua zile funguo za mauti na kuzimu, ambazo mara ya kwanza zilikuwa mikononi mwa shetani, kukawa kuanzia huo wakati na kuendelea hakuna yeyote anayeweza kuzipandisha juu roho za watu waliokufa..
Hata shetani mwenyewe hawezi tena, kwasababu funguo za kuzimu na mauti anazo Kristo mwenyewe..yeye ndiye anayewamiliki wafu wote, wema na waovu.
Warumi 14:9 “Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia”.
Sasa swali linakuja, kama wafu hawawezi kurudi kama mizimu, hivyo tunavyoviona, au tunavyovisikia vikiwatokea watu vikiwa na sura za wapendwa wao waliowahi kuishi ni vitu gani?
Jibu rahisi ni MAPEPO yaliyojigeuza na kuvaa sura za watu waliokufa.
Maandiko yanasema shetani anaweza kujigeuza akawa kama Malaika wa Nuru, atashindwaje kujigeuza na kuvaa sura ya mtu fulani aliyekufa?. Ni kitu kirahisi sana kwake.
2 Wakorintho 11:14
“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.
Kwahiyo shetani na mapepo yake wanachokifanya ni kuvaa sura za watu waliokufa na sauti zao, na kuigiza kama ndio wale watu halisi, na watu wanapowaona au kuwasikia wanaamini ni wafu wao wamerudi (Mizimu).. lakini kiuhalisia kumbe sio, bali ni mapepo yaliyojigeuza.
Na kwasababu shetani ni yule yule, anapenda kukaa nyuma ya kitu na kutafuta kuabudiwa..anakaa nyuma ya wote wanaoabudu sanamu, wanaoabudu miti wakidhani ni Mungu, wanaoabudu mizimu, wanaoabudu jua n.k
Hivyo hatuna budi tuwe macho na tujihadhari na kumwabudu shetani bila kujua, kwa kukosa maarifa.
Kadhalika kama bado tupo nje ya wokovu, hakuna namna yoyote tunaweza kujiepusha na madhara ya roho hizo chafu, ambazo zinazunguka huku na huko, kuuharibu ulimwengu.
Bwana atubariki.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
About the author