Kama Bwana anawajua walio wake tangu asili kwanini tunahubiri injili? (Warumi 8:29).

Kama Bwana anawajua walio wake tangu asili kwanini tunahubiri injili? (Warumi 8:29).

Jibu: Tusome,

Warumi 8:29 “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza”.

Ni kweli maandiko hapo yanasema Bwana anawajua walio wake tangu asili.

Ili Mungu awe Mungu ni lazima ajue mambo yote, ni lazima aujue mwisho katika mwanzo. Vinginevyo asipojua hivyo, huyo sio Mungu.

Lakini pamoja na kujua hatima zetu wote, bado hajatuambia ni nani ataokolewa na nani hataokolewa. Nafasi ya kuokolewa ipo kwa wote, kadhalika nafasi ya kupotea ipo kwa wote, ni jukumu letu sisi kupambana ili tusijikute tumeingia katika hilo kundi la ambao hawataokoka na kuingia katika ziwa la moto.

Bwana Yesu alijua tangu mwanzo ni Nani atakayemsaliti, na akawaambia mapema wanafunzi wake kwamba mmoja wenu atanisaliti, Lakini hakutaja jina kwamba ni Yuda!. Aliachia hapo katikati, kila mtu ajihisi kama ni yeye, ili lengo kila mtu ajitathmini mienendo yake na ajihadhari na roho ya usaliti.

Lakini Bwana kwa kusema hivyo, hakuacha kuendelea kuwahubiria wanafunzi wake, au hata Yuda na wanafunzi pia waliendelea kuhubiri, kwasababu siri ya atakayemsaliti alikuwa nayo Bwana na sio wao..Hivyo kazi waliyokuwa nayo ni kuendelea na kuhubiri injili, na kujitahidi wasitimize huo unabii…

Marko 14:18 “Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.

19 Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi?

20 Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe”.

Na hata sasa Mungu anatuambia lipo kundi litakalomsaliti, lipo litakaloingia katika ziwa la moto, lakini hajataja majina, hivyo ni wajibu wetu sisi kupambana tusiwe mojawapo ya hao.

Sasa swali tunalopaswa tujiulize kila mmoja wetu ni hili:

Utajuaje kama wewe utaangukia katika kundi la watu ambao wataingia jehanamu ya moto?..

Hautajua kwa tafsiri ya jina lako, wala kwa rangi ya uso wako, wala kwa kimo chako, wala kwa jinsia yako wala kwa kabila ulilotokea au familia uliyotokea.

Bali utajijua kwa tabia zako!. Kama maisha yako bado ni ya dhambi, ya anasa, ya kiulimwengu na uzinzi na uasherati, ya kuabudu sanamu, ya kutokujali mambo ya Ki-Mungu kama Yuda, ingawa unaonywa mara nyingi..basi fahamu kuwa upo miongoni mwa lile kundi lililotabiriwa kutourithi uzima wa milele.

Kadhalika kama upo ndani ya Kristo, na umepokea Roho Mtakatifu, na unayafanya mapenzi yake basi fahamu kuwa upo katika kundi la watu waliotabiriwa uzima wa milele.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba injili tunapaswa tuendelee kuihubiri kama mitume walivyoendelea na kazi hata baada ya kujua kuwa miongoni mwao yupo atakayemsaliti Bwana..zaidi sana tujihadhari na dhambi ili tusiwe miongoni mwa watakaotupwa katika ziwa la moto.

2 Timotheo 2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii,
Bwana awajua walio wake.
Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Patrick Ndabila
Patrick Ndabila
1 year ago

Ahsante ujumbe mzuri