VIJANA NA MAHUSIANO.

VIJANA NA MAHUSIANO.

Karibu katika darasa fupi, linalohusu vijana na mahusiano.

Yapo maswali kadhaa ya kujifunza kwa kijana kabla ya kuanza mahusiano ya aina yoyote ile, na mambo yenyewe ni haya;

 1. Je ni wakati gani ulio sahihi wa kuanza mahusiano?

 2. Je ni mtu gani sahihi wa kujiingiza naye katika mahusiano?

 3. Je mambo gani ninapaswa niyafanye na yapi sipaswi kuyafanya ninapoingia katika uhusiano?

Awali ya yote ni muhimu kufahamu kuwa darasa hili linawahusu/linawafaa zaidi vijana wa kiume na wa kike ambao tayari wameshaokoka!, yaani wametubu na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu na wanaitazamia mbingu mpya na nchi mpya. Kama bado hujampokea Bwana Yesu basi mafunzo haya yanaweza yasikusaidie, hivyo ni vyema kwanza ukampokea Bwana Yesu (ukaokoka), na ndipo mambo mengine yafuate baadaye.

Mahusiano yamegawanyika katika sehemu kuu (2),  Yapo Mahusiano kabla ya Ndoa, na Mahusiano baada ya Ndoa. Mahusiano kabla ya ndoa, yanaitwa Uchumba ambayo tutajikita sana kujifunza juu ya haya katika siku ya leo.


  1. Ni wakati gani ulio sahihi wa kuanza mahusiano Kwa kijana wa kiume:

Kama wewe ni kijana wa kiume na umeokoka, wakati sahihi wa kuanza mahusiano ni wakati ambao tayari unajitegemea mwenyewe. Maana yake una sehemu yako mwenyewe ya kuishi na una kipato chako mwenyewe, haumtegemei mzazi au ndugu!, kwasababu hatua ya uchumba ndio hatua ya awali kabla ya kuoa, na huwezi kuoa ukiwa bado hata wewe mwenyewe huwezi kujitunza, utamtuzaje huyo mke anayekuja?.

Kwasababu hiyo basi si wakati sahihi wa kuanza mahusiano yoyote ukiwa bado ni Mwanafunzi,  au ukiwa bado upo kwa wazazi wako, au ukiwa huna shughuli yoyote ya kukuingizia kipato!.

Ni umri gani sahihi wa kuanza Mahusiano, kwa kijana wa kiume?

Hapa inategemea na umri ulioanza kujitegemea mwenyewe, katika zama hizi vijana wengi wa kiume kuanzia miaka 25 na zaidi ndio wanaanza kujitegemeana hiyo ni kutokana na mifumo ya Elimu. Mtu atamaliza shule akiwa na zaidi ya miaka 20, na kujikuta kuanza kufanya kazi za mikono akiwa na zaidi ya miaka hata 25, wakati huo unaweza kuwa wakati sahihi wa kuanza uchumba.

Wapo wengine wanawahi kuanza kujitegemea wenyewe kabla ya umri huo!, hao wanaweza kuwahi kuanza mahusiano..lakini mahusiano ya mapema ni hatari sana, kwasababu akili ya kijana bado haijakomaa vizuri katika kujua mambo mengi ya kimaisha na wengi wanaingia huko kutokana na tamaa za kimwili tu!,.. Hivyo Ni vizuri kijana wa kiume akaanza mahusiano zaidi ya miaka 25.


Kwa kijana wa kike:

Wakati sahihi wa kuanza mahusiano kwa kijana wa kike, si wakati upo shule, bali wakati ambao umemaliza shule,

Vile vile umri sahihi wa kuanza mahusiano ni miaka 20 na zaidi!.. Zamani kidogo ilikuwa ni mapema, lakini zama hizi, shule zimewafanya watu wachelewe kuanza maisha yao kujitegemea. Lakini vijana wengi wa kike walio chini ya miaka 20 sasa wanaojiingiza kwenye mahusiano ya uchumba wengi wanaongozwa na tamaa tu!, aidha kwa kujua au kwa kutokujua. Na wengi wa hao wakifikisha miaka 30, akili zao zinapofika hatua ya kupevuka wanajigundua kuwa walikuwa wanafanya vitu vya kitoto na vya kipumbavu.


 2. Je ni mtu gani sahihi wa kujiingiza naye katika mahusiano?

Kwa kijana wa kiume:

Mtu sahihi wa kuanza naye mahusiano sio yule uliyeoneshwa na Nabii, au Mchungaji, au uliyechaguliwa na mtu. Kamwe usianze mahusiano na mtu yeyote ambaye umesaidiwa kuchaguliwa. Uchaguzi utachagua wewe!, Yule Bwana aliyekuchagulia atakuja kwako na wewe utajikuta unampenda, anakidhi vigezo vyako!..Hivyo ndivyo Bwana anavyowapa watu wenza wao na sio kuchaguliwa na mchungaji au Nabii, au kuoteshwa ndoto.

Vile  vile usianze mahusiano na msichana/ mwanamke yeyote ambaye yeye ndiye anayekuomba au kukulazimisha umwoe!.

Kwa kijana wa kike:

Kwa kijana wa kike mtu sahihi wa kuanza naye mahusiano si mwanafunzi,  haijalishi anaonesha kukupenda kiasi gani, bado sio mtu sahihi, hapa sizungumzii wale watu ambao ni wafanyakazi lakini wanajiongezea elimu ya juu (hili tayari ni kundi la watu wazima wanaojitambua), wanafunzi tunaowazungumzia hapa ni wale wa sekondari, na wale waliotoka sekondari na moja kwa moja chuo.


 4. Je mambo gani napaswa niyafanye na yapi sipaswi kuyafanya ninapoanza mahusiano?

Fanya mambo yafuatayo unapoanza mahusiano.

Kwa kijana wa kiume!

Mfahamu huyo mtu kwanza, na kama ameokoka anza naye urafiki kama wa dada na kaka tu Kama hajaokoka au si mtu wa imani moja nawe!, mhubirie kwanza aokoke, akimkubali Bwana Yesu, atakukubali na wewe, akimkataa Bwana Yesu hawezi kukukubali na wewe!. Usimwahidi kwamba utamwoa endapo akiokoka maana kwa kufanya hivyo atakukubali ilimradi tu aolewe na wewe!, hivyo mvute kwa Kristo kama unavyowavuta wengine wote.

Akikubali kumtii Kristo na kumpata Roho Mtakatifu ambaye umempokea wewe, na hata kushiriki kanisa moja nawe, hapo unaweza kuanza naye urafiki kama wa kaka na dada tu!, wa kuheshimiana, wakati huo unaweza kuongeza kumjali zaidi kuliko wengine wote wanaomzunguka, kwa kufanya hivyo atakuwa ameshaanza kujua kuwa unamjali, na hivyo atakupenda na hapo ni rahisi kuendelea na hatua nyingine.

Kwa kijana wa kike!

Kwasababu ni mwanaume ndiye anayemchagua mwanamke!, kijana wa kike hupaswi kujiweka au kujitangaza kwamba unatafuta mchumba.. Kaa katika hali yako ya asili, umri usikuogopeshe wala kukutatanisha, wapo wanaoolewa hata na miaka 60, na wanakuwa na furaha, hivyo usijitafutishe mchumba.. usijipendekeze sana kwa vijana wa kiume!, bali dumu katika usafi wa Rohoni na wa Mwilini, jiweke katika mazingira ya usafi na ya upole!, Bwana atakuletea mtu sahihi ambaye atakuheshimu, kwa wakati sahihi. (www wingulamashahidi org).

Hali kadhalika utakayemwona anakuja kwako kuwa naye makini, kwasababu Matunda mazuri si mtu tu anayeyapenda bali hata nyani, na ndege na popo na bundi wanayapenda!, (maana yake hata watu waovu wanawapenda wanawake wanaojiheshimu na watakatifu), hivyo kuwa makini, Kama hajaokoka mkaribishe kanisani, na jitahidi usimhubirie wewe, kwamaana ni rahisi kukubali kuokoka ili akupate!, bali mwunganishe na mchungaji wa kiume kanisani, au na mtu yeyote aliyesimama pale kanisani, kama akimsikiliza huyo na kumkubali Kristo, ni rahisi kuwa mtu sahihi Bwana aliyekukusudia, lakini kama hataki kujihusisha na mchungaji au mtu yeyote kanisani, jitenge naye, usitazame uzuri wake au fedha zake, ni pando la adui, anakutafuta kwa faida zake tu!

Mambo yafuatayo usiyafanye unapokuwa katika Mahusiano ya uchumba!


Kwa kijana wa kiume/kike.

1/ Usikutane kimwili na huyo uliyeanza naye mahusiano, wala msishikane wala kubusiana, (Kujaliana tayari ni ujumbe tosha kwamba kila mmoja anampenda mwenzie, na sio kufanya hayo mambo)

2/ Usimtembelee huyo kijana/binti nyumbani kwake akiwa peke yake, tafuta mwenzako muwe wawili ndipo umtembelee, hiyo itaongeza heshima yenu na vile vile shetani hatapata nafasi. Vile vile tafuta masomo mazuri yanayohusu mahusiano, yaliyofundishwa na watumishi wa Mungu wa kweli, mshirikishe mwenzio asikilize mafundisho hayo, au asome, au ahudhurie semina ili aanze kujiandaa na kuwa mume au mke.

Baada ya kuhakiki kuwa huyu mwenzangu ananifaa kimaisha na vile vile ananifaa kiroho, vile vile amekukubali uwe mwenza wake, basi hatua ya ndoa inaweza kufuata. Mambo yafuatayo yatakufaa baada ya mwenzako kukubali kufunga ndoa naye.

 1. Tangaza kwa wazazi: Kumbuka unapoenda kutangaza isiwe ni jambo la kushtusha kwa wazazi wako au walezi, ni vizuri wawe wanamjua huyu mwenza wako hata kabla ya hapo, ili wawe na amani naye.

2. Baada ya kutangaza kwa wazazi, Ndoa inapaswa utangazwe kanisani. Baada ya kanisa kujua na kupewa taratibu zote za ndoa, Mahari zitapangwa (Ni lazima kijana wa kiume ulipe mahari, ikiwa kubwa sana omba upunguziwe au kopa mahali ulipe), ni kinyume na maandiko kijana wa kiume kutolipa mahari, Kristo aliingia Gharama kutukomboa sisi (ndio damu yake) ambayo inafananishwa na mahari kwetu sisi bibiarusi wake, kwahiyo ni lazima kijana ulipe mahari.

 3. Baada ya Mahari na ndoa kutangazwa na kufungwa, kanisani. Hapo Mmekuwa Bwana arusi na Bibi-Arusi, mnaweza kufanya mambo yote yanayowahusu wana-ndoa. Hampaswi kuishi kama wachumba tena.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

JINSI YA KUUHARIBU UJANA WAKO.

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

kwanini yule kijana aliitupa ile nguo ya kitani chini na kukimbia uchi?

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

6 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Awey
Awey
2 years ago

Amina Bwana Mungu Awabariki watumishi wake Kwa mafundisho mazuri Mungu awalinde

Anonymous
Anonymous
2 years ago

Na Kama nna mahusiano Ila sifanyi mapenzi lakini mabusu tu unanishaurije Mana mapenzi pasipo hayo Mambo sidhani Kama yanawezekana?

Charles egbert
Charles egbert
2 years ago

Samahani mtumishi nashukuru kwa kunifumbua lakn kwa mtu ambae sjajitegemea na Nina mahusiano Ila sio ya kufanya uasherati hapo unanishaur nn?

MBONIMPA COSMAS
MBONIMPA COSMAS
2 years ago

Mungu azidi kuwabariki sana