MAGONJWA YAKUPATAYO MARA KWA MARA.

MAGONJWA YAKUPATAYO MARA KWA MARA.

1Timotheo 5:23  “Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara”

Haya ni maneno ya mtume Paulo kwa mtoto wake wa kiroho Timotheo, Ni rahisi kuyachukulia juu juu, lakini ukitazama kwa undani utaona jinsi watu wa kale walivyojitoa kwa Bwana,bila kuruhusu hali zao za mwilini kuwakwamisha.

Kama tunavyosoma, Timotheo alikuwa ni kijana mwenye bidii sana, aliyetumika na Mtume Paulo katika kuineza injili sehemu kubwa ya dunia, lakini kijana huyu hakuwa vizuri sana kiafya kama tunavyodhani, alikuwa anasumbuliwa na tumbo, lakini kama hilo halitoshi, alikuwa pia anapatwa na magonjwa ya MARA KWA MARA, tena katika ujana na sio uzee. Ni heri magonjwa hayo yangekuwa ni ya siku moja, bali ya mara kwa mara. Paulo aliishi naye kwa muda mrefu hivyo alikuwa anamwelewa sana, anashangaa leo yupo sawa, kesho, ni mgonjwa, wiki hii yupo sawa, wiki ijayo tumbo linamsumbua sana.

Lakini katika yote hayo, hakuwa kama Dema ambaye alimwacha Paulo, akaurudia ulimwengu, yeye aliendelea kuitenda kazi ya Bwana katika madhaifu yake ya mwili,  Ni mtu tu pekee ambaye Paulo alijiona amani kumwachia hata huduma yake aiendeleza duniani. Alikuwa kama Elisha kwa Eliya.

Hivyo mwishoni kabisa mwa huduma, tunaona hapa Paulo anamwandikia waraka huu na kumsisitiza, asinywe maji tu peke yake, bali na mvinyo kidogo kwa ajili ya magonjwa hayo ya mara kwa mara, Paulo hapa anampa ushauri wa kitabibu, zaidi ya ule wa kiroho, kwani zamani mvinyo , ulitumika kwa ajili ya baadhi ya magonjwa, lakini sasa kwa wakati wetu tunazo dawa za hospitalini. Unaweza kujiuliza Paulo ambaye Mungu alimtumia kwa ishara na miujiza ya kupita kawaida, angepaswa amweke, mikono, na kukemea magonjwa hayo ya mara kwa mara yamwachie, lakini alitambua kuwa si kila wakati hali itakuwa hivyo, mambo mengine Mungu anayaruhusu yatokee kwa sababu zake.

Ni kama Elisha, ambaye, alisumbuliwa na ugonjwa ambao ulikuja kumuua, lakini hakumwacha Bwana, na kusema Mungu gani huyu hanioni, aliendelea kuwa nabii wa Mungu,

2Wafalme 13:14 “Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake!”

Ni nini Bwana anataka tujifunze?

Katika madhaifu yetu, kamwe tusipunguze spidi ya kumtumikia Mungu, kwasababu mambo tunayoyapitia sisi walishayapitia watakatifu wengine waliotutangulia. Kijana Timotheo, alikuwa ni mdhaifu sana kimwili, lakini aliichapa injili ya Kristo, bila kujali yamsibuyo. Alisafiri huko na huko.

Yawezekana na wewe, ni mhubiri au mtumishi wa Bwana, lakini vidonda vya tumbo, haviishi ndani yako ijapokuwa umemwomba sana Bwana aviondoe lakini bado huoni matokeo yoyote, endelea hivyo hivyo kutumika usisubiri upone, una magonjwa Fulani ya kichwa ambayo yanakuja na kuondoka, yanakuja na kuondoka, yasikukwamishe, mkumbuke Timotheo, kunywa dawa za hospitalini, songa mbele, unasumbuliwa na saratani, unasumbuliwa na sukari, inapanda, inashuka, kila siku ni kuchoma sindani, Usingoje kwanza Bwana akuponye, endelea, kwani huzijui njia za Bwana, hujui ni kwanini leo upo hivyo, huwenda amekusudia, uishi maisha marefu kuliko zaidi ya wengine katika hali hiyo hiyo ili jina lake litukuzwe, na uwaponye wengi wanaosumbuliwa na maradhi kama hayo, Elisha baada ya kufa katika ule ugonjwa wake, tunaona bado mifupa yake ilifufua wafu, Hivyo kuugua si kikwazo cha Mungu kutokututumia sisi.

Tujipe moyo tusonge mbele, Bwana anatupenda, kwani yeye mwenyewe alisema, pale tuwapo dhaifu ndipo tulipo na nguvu.

2Wakorintho12:9  “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 12.10  Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu”.

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Nini maana ya..“wakiwazuia watu wasioe” (1Timotheo 4:1)

AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!

MAUMIVU  NYUMA-YA-HUDUMA.

NINI TOFAUTI KATI YA KARAMA, UTENDAJI KAZI NA HUDUMA.

KANSA/SARATANI INATIBIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments