TABIA ZA NJIA YA MUNGU KWA MKRISTO

TABIA ZA NJIA YA MUNGU KWA MKRISTO

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo.

Biblia inatuambia Yesu ndiye njia na kweli na uzima. (Yohana 14:6)

Ni kweli wakristo wengi tunamtambua yeye kama njia, lakini hatujui tabia ya hii njia kwa undani jinsi ilivyo kwetu sisi wakristo.

Tofauti na hizi njia tuzijuazo, kwamfano ukitaka kutoka Dar es salaam kwenda Morogoro, ni rahisi kuifuata hiyo barabara, au kuielewa kwasababu daima ipo palepale haibadiliki, watu wote tunaipita hiyo kila siku, tumeshaikariri, tunajua vituo vyake vyote vya njiani,  tunaweza hata kukadiria ni muda gani tutakaoutumia kumaliza safari yetu.

Lakini vipi kuhusu njia ya Mungu kwa wakristo. Je na yenyewe inakaririka, au inazoeleka, au ipo palepale?

Maandiko yanatupa majibu; tusome;

Warumi 11:33

Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!

Hapo anasema “Njia zake hazitafutikani”

Ndugu Bwana alichotuhakikishia ni , usalama na mwisho mwema wa safari yetu ya wokovu endapo tutaamua kumfuata YESU kwa mioyo mikamilifu. Lakini hakutuhakikishia kuwa njia zetu sote kwa pamoja zitafanana. Kwamba sote tukitoka hapa tutapita pale, kisha tutamalizia na pale.

Ni Mungu ndiye anayemchagulia kila mtu mapito yake kwa jinsi apendavyo yeye. Mwingine akishaokoka Bwana atampitisha mashariki kwenda Magharibi, mwingine ataanza naye kusini kwenda kaskazini, na ndio hapo utaona, mmoja ataanza kwa kupoteza kila kitu, mwingine Mungu atambariki atamfanikisha katika maisha yake atakuwa bilionea, mwingine atakuwa na maisha ya kawaida, mwingine atakuwa na ya chini. Mwingine atakuwa na afya sikuzote, mwingine atakuwa na magonjwa yasiyotibika na Bwana hamwondolei kwa kipindi fulani kirefu.

Lakini katika mapito hayo yote, Kristo atahakikisha kuwa anampa nguvu ya kuweza kukabiliana au kuchukuliana na hayo mazingira  bila kukengeuka au kuona ni mzigo mkubwa sana kwake.

Tatizo kubwa la  watakatifu ni kuwa tunataka njia zetu ziwe kama za mtu fulani pale tunapodhamiria.

Sote tunataka tuwe mabilionea kama Sulemani. Ndugu mawazo ya kumpangia Mungu ni wapi akupitishe yatakugharimu. Kwasababu njia zake hazikaririki, hazitafutikani, wala hazichunguziki. Atakupitisha ajuapo yeye, sio ujuapo wewe.

Kuna mmoja atakuwa kama Yohana mbatizaji, hali wala hanywi anakaa majangwani, kuna mwingine atakuwa kama Bwana Yesu anakula na kunywa..kikubwa ni matokeo ya wito ndicho kitakachoeleza wito wa mtu huyo ni kweli au la. Wote wawili Yohana na Bwana Yesu walikuwa na mafanikio makubwa katika huduma zao, japo mapito tofauti, hivyo kila mmoja wito wake ulikuwa ni wa kweli.

Njia za Mungu kwetu sisi hazichunguziki, kaa katika nafasi yako na wito wako, mwamini Bwana hapo hapo ulipo ikiwa kweli umeokoka na umemanisha kumfuata Yesu, kamwe usijilinganishe na mkristo mwingine, kisa yeye ni tajiri kuliko wewe, au ana uwezo wa kuhubiri sana kuliko wewe.

Mtazame Yesu tembea katika njia yake aliyokupangia, hata kama ni mlemavu, isiwe sababu ya wewe kupoteza uelekeo wa wokovu katika maisha yako.Kila pito la mtu, lina sehemu kubwa mbeleni kulisaidia kanisa la Kristo. Maisha yako ni ushuhuda wa kuwaponya wengine mbeleni. Hujui kwanini Mungu akupitishe katika mapito hayo. Hivyo acha kuzikariri njia za Bwana…

Sulemani alikuwa ni mtu mwenye akili nyingi, ambazo alipewa na Mungu, akili za kuweza kuchunguza kila kitu kilicho duniani, lakini alipofika katika njia za Mungu alikiri kuwa hakuna anayeweza kuzielewa alisema..

Mhubiri 8:17 “basi, niliiona kazi yote ya Mungu, ya kuwa haitafutikani na mwanadamu kazi inayofanyika chini ya jua; kwa sababu mwanadamu na akijisumbua kadiri awezavyo kuitafuta, hata hivyo hataiona; naam, zaidi ya hayo, mwenye hekima ajapodhania ya kuwa ataijua, lakini yeye hataweza kuiona”.

Sasa ni kwa namna gani hazitafitikani?

Ni kwa sababu nyakati nyingine Mungu anakupitisha mahali usipopatarajia, wana wa Israeli hawakujua kuwa wangeelekezwa baharini walipokuwa wanatoka Misri, lakini ndio ilikuwa njia ya Bwana kwao. Unaweza kuelekezwa na Mungu, mahali ambapo hakuna dalili yoyote ya wewe kutoka kumbe ndio Mungu kakusudia upite hapo, aonyeshe maajabu yake.

Pili wakati mwingine Mungu anatabia ya kuvuruga mipango yetu. Kanisa la kwanza lilkuwa linakwenda vizuri, katika raha yote, lakini Mungu akamnyanyua Paulo alitese kanisani mpaka Kifo cha Stefano. Kanisa likaogopa nikaondoka Yerusalemu. Kumbe nyuma ya kutawanyika kule kulikuwa na kusudi la Mungu injili ihubiriwe dunia nzima. Paulo alipomaliza kusudi hilo akageuzwa na yeye moyo akawa mhubiri. Njia za Mungu hazichunguziki.

Hata wewe mambo yako yanaweza kwenda sawa, halafu ghafla Mungu akayavuruga, lakini mwisho wake ukawa mwema. Kupata na kupoteza, nyakati za raha na shida, milima na mabonde..tarajia katika safari hii ya ukristo..Njia za Mungu hazichunguziki.

Lakini katika yote Bwana anasema.. Sisi tulioamua kumfuata yeye kwa mioyo yetu yote kamwe hatutakaa tupotee katika njia hiyo hata  kama tutakuwa hatueleweki, tutakuwa wajinga kiasi gani, hatutakaa tupotee, lakini tutafikia tu mwisho mwema kwasababu njia hiyo ni salama sana na hakika.

Isaya 35:8

[8]Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.

Anasema pia…

Yeremia 29:11

[11]Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.

Wote waliomfuata Yesu, waliofaida yake, katika kila pito. Jitwike msalaba wako mfuate Yesu. Kwasababu yeye ndio Njia pekee ya kufika mbinguni na kuumaliza mwendo wako salama.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Dia ni nini katika biblia? (Mithali 13:8)

Mofa ni nini? na inafunua nini kiroho?(1Samweli 28:24).

Kujazi ni nini? (Mathayo 6:4)

Zile Rangi saba za Upinde wa Mvua zinawakilisha nini?

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Joshua
Joshua
1 year ago

Mungu na akubariki na mataifa yapate injili ya kweli.