KUFAHAMU SIO KUJUA

KUFAHAMU SIO KUJUA

Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze maandiko..

Ipo tofauti kati ya “kufahamu jambo” na “kulijua jambo”.. Unaweza kulifahamu jambo lakini usilijue kwa undani, vivyo hivyo kuna tofauti ya “kuyafahamu maandiko” na “kuyajua maandiko”.  Hivi ni vitu viwili vyenye tofauti kubwa sana, hebu tujifunze kidogo kwa namna gani.

Tusome habari ifuatayo kisha tufafanue..

Mathayo 22:23 “Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza,

24 wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao.

25 Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake.

26 Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba.

27 Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.

28 Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye.

29 Yesu akajibu, akawaambia, MWAPOTEA, KWA KUWA HAMYAJUI MAANDIKO WALA UWEZA WA MUNGU.

30 Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni”.

Nataka tuzingatia hilo neno “MWAPOTEA, KWA KUWA HAMYAJUI MAANDIKO WALA UWEZA WA MUNGU”.

Kumbuka hawa watu waliokuja kumwuliza Bwana hilo swali ni MASADUKAYO, ni watu wa dini, wanayoyafahamu maandiko karibia yote ya kwenye torati, na hapa wanamjia YESU kwa swali linalotoka katika maandiko ya MUSA (torati), wakisema “Mtu akifa basi mke wake anaruhusa ya kuolewa na ndugu wa karibu”.. jambo ambalo ni kweli kabisa lipo kwenye Biblia.

Lakini pamoja na kwamba walikuwa wanayafahamu hayo maandiko, bado Bwana YESU anawaambia “Hawayajui maandiko” na tena wanapotea sana.

“29 Yesu akajibu, akawaambia, MWAPOTEA, KWA KUWA HAMYAJUI MAANDIKO WALA UWEZA WA MUNGU.

30 Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni”.

Tuirudie tena habari hii katika Marko..

Marko 12:24 Yesu akajibu, akawaambia, JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII, KWA KUWA HAMYAJUI MAANDIKO wala uweza wa Mungu?

25 Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni.

26 Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?

27 Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana”.

Kumbe wakati ambao wanajidhania kuwa wanayajua maandiko kwa wingi wa mistari wanayoifahamu vichwani mwao, Kristo alikuwa anawaona hawajui chochote, na hiyo ndio sababu kuu ya kupotea kwao, hawayajui maandiko bali wanayafahamu tu.

Ndugu hatupaswi kuwa kama compyuta au simu ambao inaweza kuwa na vitu vingi pamoja na biblia nzima, lakini haiyajui maandiko, na wala yale maandiko hayaisaidii kwa chochote.

Hatupaswi kuwa na idadi kubwa ya mistari vichani ambayo haina ufunuo wowote. Mistari yenye nguvu na ibilisi anayoigopa ni ile iliyopo moyoni iliyobeba ufunuo, maana yake yenye uhai katika maisha ya mtu, na inayomwongoza, na yenye nguvu, na inayothibitisha imani.

Masadukayo walikuwa wanafahamu tu Musa kasema, na kujitamba katika hayo, pasipo kujua kuwa andiko bila ufunuo ni bure..

Sasa swali ni je!, tutayajuaje maandiko badala ya kuyafahamu tu?

Kinachotangulia ni kuyafahamu, ni lazima tuyafahamu na kufahamu kunakuja kwa kuyasoma au kuyasikia yanaposomwa.. baada ya kuyafahamu hatua inayofuata ni kuyajua. Na njia pekee ya kuyajua maandiko ni kwa kupitia Roho Mtakatifu..

Huyu peke yake ndiye anayeweza kutuhamisha kutoka katika kuyafahamu maandiko mpaka kuyajua, kwani anapoingia ndani ya Mtu, anakuwa ni Mwalimu mwingine wa ziada, kukufundisha maana za ndani ya maandiko uyasomayo, anakuchambulia na kukufundisha mambo ambayo hata ukirudia kusoma tena hilo andiko ulilolisoma utaona kama vile ni jingine kabisa, na huo ndio uhudumu wa agano jipya unaotajwa katika 2Wakorintho 3:6, ambao unatutosheleza.

2Wakorintho 3:6 “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha”.

Je tayari umempokea Roho Mtakatifu?.. kama bado mwamini YESU na tubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha, kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana YESU KRISTO, baada ya hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukaa na wewe siku zote, kwani ahadi ya Roho Mtakatifu ni kwa kila mtu.

Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JE UNAZAA MATUNDA NA KUWAPONYA MATAIFA?

Ipi tofauti ya “Majibu” ya Maombi na “Majaribu”.

Ipi Tofauti ya Agano jipya na Agano la Kale?.

TOFAUTI KATI MAASKOFU, MASHEMASI, WAZEE WA KANISA NI IPI?

Nini tofauti kati ya kileo na divai ?

Print this post

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply