USIWE MSIKIAJI TU! BALI MTENDAJI.

USIWE MSIKIAJI TU! BALI MTENDAJI.


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia..

Neno la Mungu wetu linafananishwa na vitu vingi katika biblia, kuna mahali linafananishwa na “Taa” (Zab.119:105)”, sehemu nyingine linafananishwa na Upanga wa roho (Waebrania 4:12, Waefeso 6:17)” Na kuna sehemu linafananishwa na “Kioo”. Na leo tutajifunza ni kwa namna gani linafananishwa na kioo, ili tuelewe tabia nyingine ya Neno la Mungu.

Kama tunavyojua kioo kazi yake ni kuakisi taswira ya kitu. Kwa mfano mtu anapotaka kujijua yupoje kimwonekano, hususani uso wake, hakuna namna anaweza kujua uso wake upoje, bila kutumia kioo. Akitaka kujua uso wake upoje na sehemu gani na gani afanye marekebisho ni lazima atatumia kioo kama yupo peke yake.

Kikawaida mtu mwenye busara, anapoamka asubuhi, baada ya kufanya usafi wa mwili wake, kabla hajatoa mguu wake kutoka nje, kwenda kwenye shughuli zake ni lazima ajitazame kwenye kioo.. Ili ajihakiki kama uso wake upo sawa au la!, atajihakiki kama nywele zake zimechanika vizuri, isije kuwa upande mmoja kitana hakijapita vizuri, vile vile atajihakiki hakuna tongotongo lililobaki machoni n.k Hivyo kama kuna kasoro yoyote, atairekebisha pale pale akiwa na kioo chake kabla hajaondoka, kwasababu kioo hakidanganyi!..

Lakini mtu asiyejali, anapoamka asubuhi anaweza kujiangalia mara moja kwenye kioo, akajiona kasoro zake kwamba hajachana nywele, wala hajajipaka mafuta usoni… na kwa kupuuzia atasema nitarekebisha hizo kasoro ndogo muda mfupi  kabla sijaondoka.. watu wa namna hiyo  kama ukichunguza, mara nyingi wanajikuta wanaondoka pasipo kuchana nywele, au kuosha uso vizuri, au kupaka mafuta… Na Utaona baadaye wakishafika mbali  na kupita karibu na kioo chochote huko mjini ndio wanakumbuka aa! kumbe hizi nywele sikuzichana tena!…. Au..aaa nilisahauje tena kupaka mafuta usoni, na tayari nilikuwa nimeshayaandaa pale?.

Sasa hiyo ni kwasababu gani?. Ni kwasababu walijitazama kwenye kioo, na badala ya kurekebisha kasoro zao wakati ule ule walipokuwa wanajitazama kwenye kioo, wakapuuzia wakijitumainisha kuzirekebisha baadaye!. Na mwisho wa siku wanajisahau kuwa bado hawajachana nywele, au kupaka mafuta.na wanajikuta wanaondoka hivyo hivyo.. (majuto ni baadaye wameshafika mbali)

Na ndio Neno la Mungu lipo hivyo hivyo, pindi tunapolisikia Lile ndio KIOO chetu!!.. Linatuonyesha kasoro zetu!… kasoro ambazo hatuwezi kuziona kwa macho! Lenyewe linatuonyesha.. Na lengo la kutufumbulia kasoro zetu, ni ili sisi tuzirekebisha Papo kwa Hapo, na wala si kusubiri kesho au baadaye!.. Hapana bali papo kwa hapo.. Maana yake tunapolisikia Neno la Mungu tunalitendea kazi saa hiyo hiyo, hatuliweki kiporo.. Hiyo ndio tabia ya Neno la Mungu!. Hebu tusome mistari ifuatayo…

Yakobo 1:22  “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.

23  Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.

24  Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

25  Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake”

Umeona hapo?.. “Anajiangalia, kisha anaenda zake na kusahau alivyo”

Neno la Mungu linapokuja mbele yetu, na kuzifunua kasoro zetu, hata kufikia kukubali  kuwa sisi ni wakosaji… hapo ni sawa na kioo kimewekwa mbele yetu kutuonyesha kasoro zetu. Na hivyo Mungu wetu anachokitegemea kwetu ni sisi kujirekebisha wakati ule ule, na si kusubiri baadaye…

kwasababu tukisubiri baadaye, tutajikuta unarudia kujiona tupo sawa! hatuna kasoro yoyote..(Unajikuta unajisahau kuwa wewe ni mtu wa namna gani)..utajiona huna kasoro zozote. Na ndicho kinachowatokea wengi leo. Utaona mtu kasikia injili leo, na kweli imemchoma na kapata kila sababu za kutubu!. Lakini moyoni mwake hayupo tayari kutubu pale pale, anasema atatubu tu!.. pasipo kujua kuwa kioo kipo mbele yake kwa wakati huo, kikishaondoka hapo, kinachofuata ni kujisahau tu yeye ni mtu wa namna gani.

Ndio maana biblia imetuonya hapo juu.. kuwa tusiwe wasikiaji tu!, bali watendaji wa Neno.

Je na wewe ni msikiaji tu? Au ni mtendaji pia!.. Ni maneno mangapi ya Mungu umeyatendea kazi  saa hiyo hiyo baada ya kuyasikia?. Je! Siku ile uliposikia na kushuhudiwa kuwa wazinzi wote watatupwa katika lile ziwa la moto, ulichukua hatua gani?. Je uliacha uzinzi kwa vitendo au kwa mdomo tu!..Je siku ile Neno la Mungu lilipokushuhudia moyoni mwako kuwa fashion, na mavazi yasiyo ya kujisitiri ni dhambi mbele za Mungu, ulichukua hatua gani??. Uliyaacha siku hiyo hiyo au ulisema nitayaacha siku moja!!..

Kumbuka biblia inasema saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubalika ndio huu. Inawezekana na leo tena umepata nafasi ya kusikia maneno yale yale ya Bwana, kuwa wazinzi, waasherati, wezi, wanaovaa mavazi ya nusu tupu na ya kuonyesha maungo, wanaotazama picha za ngono mitandaoni, wanaojichua, wanaoupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu..n.k wote hao hawataurithi uzima wa milele. Hichi ni kioo kimewekwa mbele yako!.. kinakuonyesha kasoro zako, ni heri ukazirekebisha sasa, usingoje kesho wala baadaye.

Kama unataka kuzirekebisha sasa, hapo ulipo anguka piga magoti, na kisha kiri mbele za Baba wa mbinguni kuwa umekosa, na tubu kwa kudhamiria kutozifanya tena, kama ulikuwa unafanya uzinzi na uasherati unaachana na mtandao wote uliokuwa unafanya nao uasherati, kama ulikuwa unavaa nguo za kizinzi, unazichoma sasa hivi baada ya toba yako, wala usimpe mtu mwingine na wala usizingojeshe kesho, vivyo hivyo na mambo mengine yote..unayaacha kwa vitendo, angali bado kioo kipo mbele yako sasa.

Na baada ya kutubu hivyo, hatua inayofuata ni ya muhimu sana, nayo si nyingine zaidi ya ubatizo!. Ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38, Na baada ya kubatizwa Roho Mtakatifu atakusaidia kufanya yaliyosalia, kwasababu tayari wewe utakuwa milki yake halali.

Bwana akubariki na Bwana atusaidie.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:


Mada Nyinginezo:

MAAGIZO AMBAYO HAYAJAAGIZWA!

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

UFUNUO: Mlango wa 1

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

WAKATI WA JIONI KUTAKUWAKO NA NURU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments