JE! NA SISI NI SHABA ILIAYO NA UPATU UVUMAO?

JE! NA SISI NI SHABA ILIAYO NA UPATU UVUMAO?

Jina la Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe daima.. Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Mtume Paulo aliandika hivi;

1 Wakorintho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, KAMA SINA UPENDO, NIMEKUWA SHABA ILIAYO NA UPATU UVUMAO.

2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.

3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu”.

Kifaa chochote cha shaba kikigongwa, au kupulizwa, huwa kinataoa sauti Fulani, kwamfano zile kengele kubwa za kanisani, huwa zinapogongwa basi sauti yake inaweza kusikika mbali kidogo, lakini hasara yake ni kuwa, sauti zile huwezi kuzisikia kwa muda mrefu, zitaenda kwa muda tu na baada ya sikunde tatu au nne zitakwisha kabisa nguvu yake, ni baada ya hapo utaona ukimya mkubwa, hadi zitakapogongwa tena.

Vivyo hivyo na upatu. Upatu ni chombo ambacho kinamuundo wa sahani pana, ambazo kimsingi zinakuwa mbili, sasa hizo sahani zikishagonganishwa pamoja nazo huwa zinatoa sauti Fulani.. Na zenyewe vivyo hivyo, , unaweza kudhani sauti zao zitadumu kwa muda mrefu, lakini baada ya sekunde kadhaa zitaendelea kama mwangwi tu, na mwisho wa siku  zitafifia na baadaye kurudia ukimya wake tena kama mwanzo.

Ndivyo Mtume Paulo alivyoliona kanisa la Korintho na kuwaongezea habari hiyo, aliliona ni kanisa lililokuwa na bidii kubwa sana katika vipawa na karama za Rohoni, Mtume Paulo akilizungumzia hilo katika sura iliyotangulia ya 12. Linanena kwa lugha sana, lina karama zote za Roho, lakini limesahau UPENDO ambao ndio kiini cha Ukristo.

Akawaambia, mtu unaweza ukawa na vyote hivyo, unaweza hata ukautoa mwili wako kuungua moto, lakini kama huna Upendo wa kweli wa Ki-Mungu ndani yako wewe ni sawa na shaba iliayo na upatu uvumao, yaani hayo matendo yako yote hayatakufikisha mbali.. Kama utaotoa mwili wako uungue moto kwa nia ya kujionyesha wewe ni shujaa, au upate sifa, lakini huna Upendo wa kweli na Yule mtu kama jirani yako, wewe sio kitu, akiwa na maana, vitendo vyako vyote hivyo havitakufikisha mbali, mambo hayo yatabatilika tu baada ya muda Fulani kupita.

Na ndo maaana leo hii unaweza kuona kuna watu wakishafanyiwa jambo Fulani na Mungu, basi siku za kwanza kwanza wanajitoa kweli kweli kwake, lakini ukishapita muda fulani utaona wanapoa au wanauacha wokovu kabisa..Sasa hao ndipo ile Shaba iliayo na upatu uvumao, kwasababu kilichowafanya wamfuate Mungu haukuwa UPENDO wao kwake, bali kwasababu walifanyiwa/ watafanyiwa jambo Fulani na Mungu..Hawajui kuwa tabia moja ya  upendo  ni uvumilivu,

Paulo aliendelea kusema..

1Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.

Kumbuka Mungu alitupenda BILA SABABU YOYOTE. Sio kwamba tulikuwa wema, au tulistahili, au tulimpa fedha, au chochote, hapana Yeye alitupenda tu, na sisi anataka tuwe na Upendo kama huo kwake, na kwa wanadamu wenzetu. Huo ndio unaoitwa UPENDO wa AGAPE (Upendo wa Ki-Mungu). Tunakuwa tayari kuwasaidia wengine kiroho, hata kama wanatupenda au hawatupendi, wanatusaidia au hawatusaidii. Ndivyo Mungu anavyotaka. Yeye anawanyeshea mvua yake waovu na wema.

Lakini tukikosa hayo yote, na huku tunataka kujaribu kumtumikia Mungu, na huku hatutaki kuwa kuvumilia, hatutaki kumwamini, hatutaki kuacha husuda, na majivuna  hatutaki kufadhili, tujue tu hizo ni mbio za sakafuni, hazitusaidii chochote.

Hata kama tutakuwa tunaona maono mengi makubwa kiasi gani, , bado mbele za Mungu sisi sio kitu.

Kuna mchungaji mmoja huko Jamaika, alikuwa sio tu ni mchungaji mwenye kanisa kubwa, lakini pia alikuwa ni mtu mwenye Karama kali sana ya kinabii, kiasi kwamba, aliposimama madhabahuni, kabla mtu hajaingia kanisani akiwa pale mlangoni tu, aliweza kumtambua na kumwambia, Fulani kwanini jana ulimdanganya mke wako na kuwambia hiki na hiki.. Na saa hiyo hiyo Yule mtu alidondoka kwa machozi mengi akilia na kuomboleza amemkosea Mungu. Mchungaji huyu aliogopeka na kuonekana ni mtakatifu sana.

Lakini siku moja, wakiwa katika ibada ya nguvu sana, na Roho Mtakatifu alishuka katikati yao, alisikia kuhukumiwa moyoni, ndipo akasimama huku akilia na kuliambia kanisa, leo ninatubu dhambi zangu, kwasababu nimekuwa nikilificha kanisa na Roho Mtakatifu, kwa tabia yangu ya Ushoga, ambayo nimekuwa nayo kwa muda mrefu, na nimeshazini na wanaume wengi sana.

Kanisa liliposikia vile liliishiwa nguvu, mpaka wakataka kusitisha karama zote za kinabii katika kanisa, kanisa liwe linaendelea tu hivyo hivyo bila karama yoyote ya Roho.

Unaona! Tatizo sio karama, tatizo ni upendo (Hofu )  wa mtu aliokuwa nao kwa Mungu. Huyu nabii alikuwa ni Upatu uvumao. Hata sasa tunapaswa tujihakiki sana, sisi kama wachungaji, manabii, wainjilisti, na vilevile washirika. Je! Utumishi wetu unaendana na Upendo halisi wa Mungu?. Tusije tukawa ni watu wa kutaabika usiku na mchana, tunatumika kwa nguvu nyingi, tunaona Mungu akiwafungua na kuwaponya wengi, kumbe nyuma ya pazia Mungu anatuona tunafanya kazi bure.

Bwana atusaidie tuupe Upendo kipaumbele cha kwanza. Kwasababu tukimpenda Mungu, hatutaona sababu ya kumvunja moyo kwa matendo yasiyompendeza.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

NGAZI 7 AMBAZO MKRISTO NI LAZIMA AZIPANDE KUUFIKIA UKAMILIFU.

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

JE UPENDO WAKO UMEPOA?

UFUNUO: Mlango wa 3 part 3

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments