Jibu: Tusome,
Waamuzi 1:19 “Bwana alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; ASIWEZE KUWAFUKUZA HAO WALIOKAA KATIKA HILO BONDE, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma”.
Ni kweli Bwana hakuweza kuwafukuza hao watu waliokaa mabondeni… Lakini si kwamba alikuwa hana uwezo wa kuwafukuza, bali kulikuwa na kusudi kwanini hakuweza kuwafukuza..
Ili tuelewe vizuri tuanzie kuisoma habari hiyo kuanzia mstari wa 17..(zingatia maneno yaliyoanishwa kwa herufu kubwa).
Waamuzi 1:17 “Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na WAKAWAPIGA WAKANAANI waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma.
18 Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake.
19 BWANA ALIKUWA PAMOJA NA YUDA; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma”.
Mstari wa 19, unaanza kwa kusema “Bwana alikuwa pamoja na Yuda” maana yake ni kwamba, katika vita Yuda alivyokwenda kupigana, Bwana alikuwa pamoja naye..(kumbuka Yuda anayezungumziwa hapa sio Yule mwana wa Yakobo, wala sio Yule Yuda aliyemsaliti Bwana Yesu), bali ni kabila la Yuda kwa ujumla, ambalo wakati wa kuingia katika nchi ya Ahadi lilipaswa liupiganie urithi wake kwa kuwatoa wenyeji wa Kanaani ili kusudi wapate ardhi ya kukaa wao, kama urithi wa kabila zima.
Hivyo katika harakati za kupambania urithi wao huo walikutana na makabila mengi mbalimbali, ambayo mengine yalikuwa na nguvu sana na mengine manyonge, yale yaliyokuwa manyonge Yuda walikwenda kwa ujasiri na kuyapiga na kuyapokonya ardhi, kwasababu hayakuwa na silaha zenye nguvu za kuwazidi,
Lakini yale yaliyokuwa na Nguvu nyingi za kivita, Yuda waliyaogopa, hivyo hawakudhubutu kwenda kupigana nayo, na kwasababu hiyo Mungu asingeweza kuyaondoa kwasababu Mungu kamwe hatembei na watu wasio na Imani, hivyo akawaacha,
Lakini kama wangechukua hatua ya kwenda kupambana na hao maadui zao, pasipo kutazama ni silaha za aina gani wanazomiliki, ni wazi kuwa Mungu angewasaidia katika vita hiyo, na hatimaye wangewaondoa hao watu na kuutwaa urithi wao.
Sasa baadhi ya makabila ambayo Yuda waliyaogopa ndio hao waliokuwa wanakaa mabondeni, na sababu ya kuyaogopa biblia imeitaja pale kuwa “makabila hayo yalikuwa na magari ya chuma kwaajili ya vita”..Yuda wakaogopa wasiende kupigana nayo, jambo ambalo Yoshua mtumishi wa Mungu alishawaonya kuwa wasiyaogope makabila hayo..
Yoshua 17:17 “Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu;
18 lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, WAJAPOKUWA WANA MAGARI YA CHUMA, WAJAPOKUWA NI WENYE UWEZO”
Utaona pia hiyo sio mara ya kwanza wana wa Israeli kuyaogopa mataifa yenye nguvu kupita wao, soma pia Hesabu 13:33 na Waamuzi 4:3
Hiyo inatufundisha nini?
Tunachojifunza ni kuwa “Mungu hawezi kufanya jambo lolote kwetu pale tunapomkosea Imani” Hilo ndilo jambo ambalo Mungu hawezi kufanya!!! Na lingine ambalo hawezi kufanya ni DHAMBI!
Yakobo 1:6 “Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote”.
Ukiamini kuwa Mungu hawezi kukuponya, basi fahamu kuwa KWELI HATAWEZA KUKUPONYA!, Ukiamini kuwa Mungu hawezi kukutendea jambo Fulani au kukupigania, basi fahamu kuwa ni KWELI MUNGU HATAWEZA KUKUTENDEA HILO JAMBO, wala KUKUPIGANIA katika hiyo vita iliyo mbele zako.
Siku zote fahamu kuwa PASIPO IMANI HAIWEZEKANI KUMPENDEZA MUNGU (Waebrania 11:6).
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Mtu akija kwangu naye HAMCHUKII baba yake hawezi kuwa mwanafunzi wangu?
About the author