DANIELI: Mlango wa 11

DANIELI: Mlango wa 11

Mungu wetu MKUU YESU KRISTO, asifiwe.

Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Danieli, kama tulivyoona katika mlango uliopita, Danieli akionyeshwa maono yale na Gabrieli, akiwa kando ya ule mto Hidekeli jambo hili tunalisoma katika ile sura ya 10, Lakini kwenye hii sura ya 11 na 12 tunaona ni mwendelezo ule ule wa mazungumzo kati ya Gabrieli na Danieli, Kumbuka baada ya Danieli kujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kufunga na kuomba alionyeshwa mambo yatakayokuja kutokea katika kipindi chake na katika nyakati za mwisho, kwa undani zaidi.

Tukisoma…

Mlango 11:1 Tena mimi, katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi, mimi nalisimama nimthibitishe na kumtia nguvu.2 Nami sasa nitakuonyesha yaliyo kweli. Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani. 

Kumbuka sasa hapa ni Gabrieli anazungumza mazungumzo yaliyoanzia tokea sura ya 10, anamwambia Danieli, watasimama wafalme watatu katika ufalme wa Uajemi ambao aliyeko yeye, na watakapoondoka hao atakuja mfalme wa nne, ambaye atakuwa na nguvu kuliko hao wa kwanza. Historia inaonyesha walipita wafalme wanne katika utawala wa Uajemi baada ya Mfalme Koreshi, na inaonyesha huyo mfalme wa nne, alikuwa ni AHASUERO, yule wa malkia Esta, ambaye alikuwa na utajiri mwingi, ndio maana ukisoma kitabu cha Esta utaona aliweza kutawala kutoka bara Hindi mpaka Kushi majimbo 127, hivyo alikuwa ni mtawala mkuu sana, lakini mwisho wa utawala wake, alikuja kushindana na wafalme wa uyunani, lakini hakufanikiwa bali aliangamizwa na ufalme wake ukaanguka katika mikono ya wayunani.

Tukiendelea mstari wa 3-4..

“3 Na mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa mamlaka kubwa, na kutenda apendavyo.

4 Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang’olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao. “

Huyu Mfalme Hodari ni “Alexanda mkuu” ndiye aliyesimama na kuiangusha Uajemi, Na historia inaonyesha alikuwa na nguvu nyingi kila mahali alipokwenda kupigana alifanikiwa,hii ndio ile pembe moja mashuhuri ya yule beberu kama tulivyoiona katika ile sura ya 8, lakini kama hapo inavyosema ufalme wake utavunjika, ni kweli maana alikufa katika umri mdogo miaka 32, na uzao wake haukusimama na kuurithi ufalme wake, kinyume chake ufalme wake uligawanyika katika pande nne, zilizomilikiwa na majenerali waliokuwa chini yake ndio zile pepo nne za mbinguni. 

 Mstari wa 5.

” Na mfalme wa kusini atakuwa hodari; na mmoja wa wakuu wake atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa. “

Historia pia inaeleza baada ya huu Ufalme kugawanyika katika pande nne; kaskazini ilikuwa chini ya Lisimakusi, magharibi chini ya Kasanda, Mashariki chini ya Selekusi na kusini chini ya Ptolemi. Hivyo mmoja kati ya hawa majemedari wake (Alexanda) atakuwa hodari kuliko Ptolemi mfalme wa kusini na huyo sio mwingine zaidi ya SELEKUSI aliyekuwa mfalme wa Mashariki, ambaye historia inasema alifanikiwa kuwaangusha wafalme wale wawili yaani wa kaskazini na wa Magharibi na kumiliki mbili ya tatu ya ufalme wa Alexanda yaani mashariki, magharibi na Kaskazini, wakati Ptolemi alibakiwa na kusini tu.. Hivyo ufalme ukabakia katika pande mbili tu, kaskazini na Kusini.

Tukiendelea mstari wa 6.

“Na baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile. “

Baada ya kipindi fulani kupita historia inarekodi Mfalme wa Pili wa Kaskazini (Antiokia Theo) na Mfalme wa tatu wa kusini (Ptolemi Filadelfia) walikuja kufanya mapatano, Mfalme wa kusini alimtoa Binti yake anayeitwa Berenisi, aolewe na mfalme wa kaskazini kwa mapatano kuwa mtoto atakayezaliwa amiliki falme zote mbili yaani ufalme wa Kaskazini na Ufalme wa kusini, Hivyo mfalme wa Kaskazini alimwacha mke wake wa kwanza(aitwaye Laodika) na kumuoa Berenisi na kuzaa naye mtoto.

Lakini biblia inasema hayo hayatawezekana, kwasababu baada ya baba yake Berenisi kufa, Mfalme wa kaskazini alimtalakia Berenisi na kurudiana na mke wake wa zamani Laodika, aliyeachiwa watoto wawili, Hivyo Laodika alipoona amerudishwa katika nafasi yake ya umalkia alimfanyia hila mfalme na kumpa sumu, Hivyo akafungua wigo wa watoto wake kuurithi ufalme, zaidi ya yote alikuja kumuua Berenisi pamoja na mtoto wake ili asipatikane wa kuchukua nafasi ya watoto wake, Hivyo mtoto wa Laodika aliyeitwa SELEKUSI KALINIKUSI akatangazwa kuwa mfalme mahali pa baba yake, ili kutimiza maono Danieli alioonyeshwa kwamba mfalme, wala yule binti wala mkono wake wala aliyemzaa hawatasimama.

 Tukiendelea…

“7 Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda;

8 na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini. “

Hili chipukizi la mizizi yake (yaani Berenisi) ambaye atasimama mahali pake, alikuwa ni Kaka yake Berenisi aliyeitwa PTOLEMI UGRETESI aliyerithi ufalme wa kusini baada ya Baba yake na dada yake kufa. Hivyo kwa hasira na ghadhabu ya kuuliwa kwa dada yake alipanga jeshi kubwa na kwenda kupambana na mfalme wa kaskazini, alifanikiwa kuingia kwenye ngome ya kaskazini akisaidiwa na mataifa ya kando kando yaliyokuwa yanamchukia mfalme wa kaskazini, hivyo aliweza kuteka nyara nyingi na kurudi nazo Misri, aliweza pia kuteka majimbo baadhi ya Asia ndogo na Siria yaliyokuwa yanamilikiwa na mfalme wa kaskazini na kuyafanya kuwa yake.

Mstari wa tisa unasema..

“9 Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe.

10 Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake.”

Mistari hii inaonyesha jinsi mfalme wa Kaskazini atakavyokwenda katika ufalme wa Kusini lakini alikuja kurudi katika nchi yake, lakini watoto wake wawili ambaye mmoja wao alikuja kufa baadaye walipanga majeshi kwenda kupigana na mfalme wa kusini ili kulipiza kisasi na kufanikiwa kurudisha majimbo yaliyochukuliwa na mfalme wa Kusini (Ptolemi ugretesi), Hivyo mmoja wa wale watoto aliyeitwa “ANTIOKIA MAGNUSI” alimpiga Ptolemi ugretesi na kufanikiwa kurejesha baadhi ya majimbo yaliyochukuliwa nayo ni Siria na Seleukia.

Tukiendelea..

“11 Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake. “

Baada ya Ptolemi ugretesi kufa, “PTOLEMI FILOPATA” akamiliki badala yake, huyu ndiye aliyeingiliwa na ghadhabu kubwa kuona kwamba mfalme wa Kaskazini anamjia na jeshi kubwa, lakini kama biblia inavyotabiri jeshi hilo litawekwa mikononi mwake na ndivyo ilivyokuwa, Mfalme wa Kaskazini alikuja kupigwa na Mfalme wa Kusini katika vita vya Rafia pembezoni mwa Gaza mwaka 217 KK.

 Tukiendelea..

“12 Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi elfu; lakini hataongezewa nguvu. “

Baada ya kushinda vita dhidi ya ufalme wa Kaskazini moyo wake ulijitukuza..

Tukiendelea..

“13 Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadha wa kadha, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi.

14 Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka.

15 Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga.

16 Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake. “

Hili lilikuja kutimia pale Mfalme wa Kaskazini (Antiokia III Magnus) alipopanga majeshi makubwa, na kwenda kupambana na mfalme wa Kusini, na kumshinda, na baadhi ya wayahudi wenye kiburi walimuunga mkono Antiokia kumpinga mfalme wa Kusini,ili kuyathibitisha maono, hivyo ilimsaidia Antiokia kupata nguvu, lakini hawakujua kama hayo yatawageukia kuwa mwiba kwao, kwasababu baada ya huyo atanyanyuka mfalme atakayewatesa na kuwaua. Hivyo aliposhinda akawa na nguvu juu ya NCHI YA UZURI (yaani Israeli) na hakuna taifa lililoweza kusimama dhidi yake.

“17 Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa. “

Zaidi ya yote Antiokia III, alitaka kumiliki mpaka ufalme wa kusini yaani Misri, hivyo alitumia hila kwa kumpa Binti yake (aitwaye Kleopatra) mfalme wa Kusini (Ptolemi) ili kwamba amsaliti na kisha baadaye auchukue ufalme wote lakini hilo halikufanikiwa kwasababu Kleopatra badala ya kumsaliti Ptolemi moyo wake uliambatana naye.

“18 Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe.

19 Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena”. 

Historia inaonyesha baada ya Antiokia III, kuona amelaghahiwa na binti yake, alimua kuhamishia jitihada zake katika nchi za visiwa vya mbali ambavyo ni Asia ndogo na Ugiriki ili kutanua milki yake, lakini Jenerali mmoja wa Kirumi aliyeitwa “LUKAS KORNELIO SKOPIO” alimpiga na kumshinda kabisa na kumnyang’anya alivyokuwa navyo alipojaribu kuivamia Ugiriki, Hivyo aibu yake ikamrudia mwenyewe kama biblia ilivyosema badala ya kushinda, alishindwa.

Na hata aliporudi kwake hakuwa salama baada ya muda mfupi aliuawa.

 Tukiendelea..

“20 Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita. “

Baada ya Antiokia III mfalme wa kaskazini kufa mtoto wake aliyeitwa SELEUKIA FILOPATAalitawala mahali pake, huyu alikuja na sera ya kuongeza kodi katika ufalme wake ili kuzidisha mapato. Alijaribu kufanya hivyo hata katika Israeli na kufikia hatua ya kutaka kujaribu kuteka Hekalu la Mungu lililopo Yerusalemu kwa nguvu lakini hilo halikuwezekana, alikuja kufa baada ya muda mfupi hakufanikiwa kutawala kwa muda mrefu kama Baba zake. Kama ilivyotabiriwa.

 “21 Kisha badala yake atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza. “

Huyu alikuwa ni “ANTIOKIA IV EPIFANE”, ndugu yake Seleukia, alinyanyuka japo alishutumiwa kwa kumuua kaka yake hakupata ufalme kwa njia ya halali, bali alitumia njia za kujipendekeza za kutoa ahadi za kulaghai,kujinyanyua, na rushwa, ili kupata ufalme na jambo hilo lilifanikiwa mikononi mwake. Mfano dhahiri wa mpinga-kristo atakayekuja atatafuta ufalme kwa kujipendekeza.

Mstari wa..

“22 Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika, naam, mkuu wa maagano pia.

23 Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo.

24 Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa wilaya hiyo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa.

25 Naye atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini hatasimama; maana watatunga hila juu yake.

26 Naam, walao sehemu ya chakula chake watamwangamiza, na jeshi lake litagharikishwa; na wengi wataanguka wameuawa. “

Tunasoma katika historia, Antiokia IV Epifane alishuka kupigana na Misri lakini hakushinda kwasababu Misri ilisaidiwa na Rumi, na zaidi ya yote washauri wake walimfanyia hila hivyo akapigwa katika vita.

 “27 Na katika habari za wafalme hao wawili, mioyo yao watanuia kutenda madhara, nao watasema uongo walipo pamoja mezani; lakini hilo halitafanikiwa; maana mwisho utatokea wakati ulioamriwa.

28 Ndipo atakaporudi mpaka nchi yake mwenye utajiri mwingi; na moyo wake utakuwa kinyume cha hilo agano takatifu; naye atafanya kama apendavyo, na kurudi mpaka nchi yake. “

Antiokia alipotoka Misri kwa hasira ya kushindwa vita, alifika Yerusalemu na kuwakasirikia wayahudi pamoja na Hekalu la Mungu, ndipo dhiki ya wayahudi ilipoanzia.

 Mstari wa..

“29 Kwa wakati ulioamriwa atarudi, na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.

30 Maana merikebu za Kitimu zitakuja kupigana naye; basi atavunjika moyo, naye atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.”

Merikebu za Kitimu ni Warumi waliowasaidia wamisri kupigana naye..lakini aligeuza moyo wake ni kurudi Yerusalemu kupambana na hao walioonekana kwenda kinyume na yeye (wayahudi).

“31 Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, nao watalisimamisha chukizo la uharibifu. “

Historia inasema Antiokia IV, aliingia kwenye hekalu la Mungu huko Yerusalemu na kuweka sanamu ya Mungu wake ZEU, na kuwazuia wayahudi wasitoe sadaka za kuteketezwa za daima katika hekalu la Mungu.

Tukiendelea..

“32 Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.

33 Na hao walio wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi.

34 Basi watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo; lakini wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza.

35 Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja.

36 Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika.”

Antiokia ni mfano dhahiri wa mpinga-kristo atakayekuja, kama tunavyosoma kwenye 2Wathesalonike 2:3-4, inasema…3 Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.

Hivyo unaona hapo Antiokia ni kivuli halisi cha mpinga-kristo (PAPA) atakayekuja.

 “37 Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote.

38 Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo.

39 Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa,

40 na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati.

41 Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni.”

Hizi nchi za Edomu, na Moabu pamoja na Edomu hakuzigusa kwasababu zilimsaidia kwenda kinyume na Israeli (Nchi ya Uzuri).

“42 Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka.

43 Lakini atakauwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake.

Historia inaonyesha alifanikiwa kuwa na hazina nyingi za fedha na dhahabu mfano dhahiri wa mpinga-Kristo atakayekuja..(PAPA), Ukitazama utaona hazina kubwa ya dunia sasa ipo Roma.

 Mstari wa 44..

“44 Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi.

45 Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia. “

Antiokia IV Epifane alikuja kufa, Kifo chake kilikuja ghafla na hakuna aliyemsaidia pamoja na kujiiunua kwake kama mungu na kujitukuza vile alianguka ghafla,. Kuonyesha kuwa hakuna tumaini lolote kwa mpinga-kristo atakayekuja na kwa watu wake, Biblia inasema.Ufunuo 18:8″ Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika SIKU MOJA, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu. “

Kumbuka Dhumuni kubwa la Gabrieli kumuonyesha Danieli mambo haya yote moja baada ya lingine yatakayotokea katika utawala aliokuwa anaishi na kwa sehemu utawala utakaokuja, ni kumfanya Danieli aelewe mpango wa Mungu kwa kina. Kama tunavyosoma katika sura zilizopita Danieli hakuonyeshwa mambo haya kwa undani juu ya hizi falme kama alivyoonyeshwa katika Sura hii..

Vivyo hivyo na kipindi tunachoishi sasa, Bwana anayo AGENDA, kwa Kanisa lake, lilipotoka,lililopo na linapokwenda! swali ni je! Unafahamu AGENDA ya Mungu kwa wakati unaoishi??..je unajua kuwa kanisa unaloishi ni la mwisho kati ya yale saba ambayo Kristo aliyataja katika Ufunuo 2 na 3

Je! Unafahamu kuwa mihuri saba ilishafunuliwa?, Je unafahamu kuwa ile chapa ya mnyama imeshaanza kutenda kazi,? tena kibaya zaidi inatenda kazi ndani ya makanisa?..Kama huyafahamu hayo, ni vizuri ukatenga muda umuombe Mungu akufunulie kama Danieli alivyoomba ili siku ile isije ikakujia kama mwivi kwa kukosa kuwa na maarifa..Kumbuka tunaishi katika kizazi ambacho kitaweza kushuhudia kuja kwa pili kwa Kristo, je! umeokolewa?

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; “

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Katika sura ya 12 tutaona jinsi yule malaika(Gabrieli) akimfunulia Danieli mambo ambayo yatakuja kutokea katika ule ufalme wa mwisho wa RUMI.

Kwa mwendelezo >>> Mlango wa 12


Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: MLANGO WA 17

UFUNUO: MLANGO WA 18

CHUKIZO LA UHARIBIFU.

ESTA: MLANGO WA 1 & 2

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.

JE! MBINGUNI KUTAKUWA NA KULA NA KUNYWA?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments