DANIELI: Mlango wa 12.

DANIELI: Mlango wa 12.

Jina la mwokozi wetu YESU KRISTO lihimidiwe milele na milele.

Huu ni mwendelezo wa kitabu cha Danieli leo tukiwa katika ile sura ya mwisho ya maono Danieli aliyoonyeshwa yahusuyo siku za mwisho. Katika sura hii tunaona Gabrieli akiendelea kumfunulia Danieli mfululizo wa mambo yaliyoanzia sura ile ya 10 na 11 ambapo tuliona jinsi Danieli akiambiwa kwa undani mambo yaliyojiri katika utawala wa Uajemi na Uyunani ambao uliishia na mtawala mkatili wa kiyunani aliyeitwa Antiokia IV Epifane aliyewatesa wayahudi. Lakini tukitazama katika sura hii ya mwisho ya 12 tunaona Danieli akionyeshwa picha (japo kwa sehemu) ya matukio yatakayokuja kutokea katika utawala wa mwisho (yaani RUMI).

Tukisoma ule mstari wa kwanza,..unasema

“Danieli 12:1 Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.”

Kumbuka Mikaeli ni malaika anayesimama kwa ajili ya kulipigania taifa la Israeli (Ni malaika wa vita), hata ukitazama katika sura ya 10, utaona Mikaeli alikuja kumsaidia Gabrieli katika vile vita ili kuufikisha ujumbe wa Mungu, Na amekuwa akiwapigania Israeli dhidi ya wale wakuu (au mapepo) ya Falme zile zote zilizotangulia kuwapo. Hivyo ili Mikaeli na jeshi lake waipiganie Israeli vizuri na kushinda inategemea kiwango cha kumcha Mungu cha wayahudi, kikiwa chini inamaana wale wakuu wa giza wanapata wigo mkubwa zaidi ya kuwatesa watu wa Mungu(Wayahudi), vivyo hivyo kiwango cha kumcha Mungu kikiwa juu, ndivyo Mikaeli na jeshi lake linavyoweza kupata nguvu ya kuipigania Israeli na kushinda dhidi ya wale wafalme wa giza. Kwahiyo vita vya malaika vinatemea hali za kiroho za watu wa Mungu.

Na ndio maana utaona wakati wowote waisraeli wakimuacha Mungu maadui zao wanakuja kuwashambulia, lakini wanapomrudia Mungu na kuzishika sheria zake, Mungu anawaokoa na maadui zao kwa kuwapigania. Na ndivyo ilivyo hata kwa wakristo, Kuna malaika amesimama kwa ajili yetu, hakuna malango yoyote ya kuzimu yatakayosimama mbele ya kanisa la Kristo kama likienda katika hali ya utakatifu.

Tukiendelea katika mstari huu tunaona biblia inasema Mikaeli atasimama, na kutakuwa na wakati wa taabu ambayo haijawahi kutokea tangu Israeli iwe taifa, hii inafunua kuwa mambo hayo yatatokea katika siku za mwisho kwenye ule utawala wa RUMI, wakati wa dhiki kuu pale mpinga-kristo atakaponyanyuka na kuwaua wayahudi wengi, biblia imekiita hicho kipindi kama “wakati wa taabu ya Yakobo (Yeremia 30:7)”

Na ndio kipindi alichotabiri Bwana Yesu katika Mathayo 24: 21 “Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.”.

Na pia pale anasema.”wakati huo watu wako wataokolewa”. hii ikiwa na maana kuwa wayahudi wengi watapewa neema ya kumwamini Yesu Kristo kama ndiye Masihi wao aliyetabiriwa kumbuka kwasasa wayahudi wamefumbwa macho hawamwamini Yesu Kristo lakini watakuja kupewa neema hiyo baadaye.

(Ukisoma Warumi 11: 25 inasema..“Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu UGUMU umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.

26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.

27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.).

Jambo hili litatimia pale juma la 70 la Danieli litakapoanza ambapo wale wayahudi 144000 watatiwa muhuri kama tunavyosoma katika ufunuo 7.

Tukiendelea mistari inayofuata…

“Danieli 12:2 Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.

3 Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.”

Hapa tunaweza kuona Danieli akifunuliwa siri zihusuzo ufufuo wa wafu, kwamba wakati utakuja ambapo wafu wote watafufuliwa. jambo ambalo Bwana Yesu alishalizungumzia katika Yohana 5:25” 

28 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.

29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.”

Kadhalika alionyeshwa pia wenye hekima watang’aa kama mwangaza wa jua, pamoja na hao waongozao wengine kutenda haki. Kila mtu anayawafundisha watu katika njia za haki na utakatifu na kuwafanya watazame mambo ya mbinguni, biblia inasema siku ile atang’aa kama nyota za mbinguni.

Mstari wa 4 unasema..

“4 Lakini wewe, Ee Danielii, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.”

Danieli anaambiwa aufunge unabii huo mpaka wakati wa mwisho ulioamriwa ikiwa ikiashiria kuwa wakati wa mwisho(ambao ndio tuliopo sisi) mambo hayo yatafunuliwa, na watu wataelewa yaliyoandikwa humo ndani, na ndio maana ukienda mbele kidogo anasema MAARIFA yataongezeka.

(Maarifa yataongezeka):Kumbuka maarifa haya, ni maarifa ya kumjua Mungu, siku hizi za mwisho maarifa yameongezeka juu ya masuala ya kimungu, japo sio kwa watu wote bali kwa watu wachache wenye hekima, ilikuwa ni ngumu kwa wakati ule wa Danieli, kumuelewa mpinga-kristo atakuja kwa namna gani, au shetani anafanyaje kazi, lakini kwa wakati wetu kwa kupitia Bwana YESU, mambo hayo yapo wazi, na historia ikithibitisha hayo yote kuwa mpinga-kristo atatokea si pengine zaidi ya kanisa Katoliki la RUMI,.

Vivyo hivyo maarifa juu ya utawala wa amani wa YESU KRISTO wa miaka 1000 hayakujulikana kwa wakati ule, lakini sasahivi tunafahamu, n.k.; Na maarifa haya yanaendelea kuongezeka siku baada ya siku kwa msaada wa Roho wa Mungu mpaka tutakapofikia kilele cha utimilifu.

Kadhalika na maarifa katika mambo ya ulimwengu, yameongezeka, kama tunavyoona Jinsi Teknolojia inavyozidi kuongezeka, usafiri umekuwa wa haraka sana, watu wanaenda huku na huko dunia imekuwa kama kijiji. Na maarifa yataongezeka katika kila eneo.

Tukiendelea…

“Danieli 12:5 Ndipo mimi, Danielii, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili.

6 Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?

7 Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, hapo alipoinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa”. 

Tunaona baada ya Danieli kuelezwa juu ya dhiki kubwa itakayokuja huko mbeleni, Hapa tunaona malaika mmoja akimuuliza yule mtu aliyekuwa juu ya mto, kwamba hayo mambo yatadumu kwa miaka mingapi hadi yaishe, ndipo yule mtu akawaambia itakuwa ni kwa wakati na nyakati mbili na nusu wakati (ikiwa na maana ni MIAKA MITATU NA NUSU). Hii inaonyesha kuwa kipindi cha dhiki kuu kitadumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu.

Danieli 12:8 Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?

9 Akasema, Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.”

Tunaona tena hapa Danieli kwa jinsi alivyokuwa “mtafutaji na mchunguzaji” alitaka kujua kwa undani tena juu ya matukio yatakayotokea katika utawala wa mwisho wa Rumi, kama alivyoelezewa na Gabrieli juu ya utawala wa Uajemi na Uyunani katika sura ya 11. Lakini aliambiwa Enenda zako Danieli, maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri mpaka wakati wa mwisho ikiwa na maana kuwa asitafute kujua zaidi ya hapo, kwani yaliyosalia yamewekwa kwa ajili ya watu wa siku za mwisho yaani mimi na wewe.

Swali ni je! Na sisi tunatafuta kufahamu mambo hayo kama Danieli alivyotafuta kujua ya kwake?.

Danieli anaendelewa kuambiwa..

“Danieli 12:10 Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.”

Umeona hapo wakati wa mwisho dunia ikiwa katika kilele cha maovu, watu wamemsahau Mungu kwa mambo maovu kama anasa, ulevi, uasherati, matendo ya kikatili, fashion, udanganyifu wa mali n.k. wapo ambao watajitakasa na kujifanya kuwa watakatifu zaidi. Mfano dhahiri tunauona kwa Nabii Eliya wakati Israeli yote imegeukia kuabudu mabaali, na maovu yamezidi kila mahali, na pale Eliya alipojaribu kuwashitaki Israeli wote mbele za Mungu akidhani ya kuwa amebakia peke yake anayemcha Mungu. Lakini Mungu alimwambia kuwa amejisazia watu ELFU SABA wasiopigia goti baali.

Na vivyo hivyo kwa kizazi hichi kilichopotoka pale unapodhani hakuna tena watu wanaompendeza Mungu, hakuna tena wanawake wanaovaa vizuri, hakuna watu wanaomwabudu Mungu katika Roho na kweli , hakuna watakatifu n.k. fahamu kuwa Mungu amejisazia watu wake wachache kila mahali wanaoupendeza moyo wake na hao ndio watakaokuwa na hekima na kuzidi kujisafisha na kuelewa mambo hayo. Lakini kwa wale waovu biblia inasema wataendelea kuwa wabaya na hawatajua chochote na siku ile itawajilia kama mwivi, hivyo jiangalie na wewe upo kundi gani?. Usidanganyike na upepo wa huu ulimwengu kwamba wengi wanafanya hivi na mimi ngoja nifanye..Utaangamia.

Mwisho kabisa Danieli anaambiwa..

“Danieli 12:11 Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.

12 Heri angojaye, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.

13 Lakini enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama katika kura yako mwisho wa siku hizo.”

Kuanzia kipindi kile mpinga-kristo atakapoingia katika HEKALU na kuwazuia wayahudi wasiendelee kutoa sadaka ya daima katika nyumba ya Mungu, ambayo itakuja kutengenezwa tena huko Yerusalemu (kumbuka maandalizi yote ya kujengwa sasa hivi yapo tayari), kwahiyo kuanzia hicho kipindi mpaka mwisho wa dhiki kutakuwa na siku 1290.

Sasa kumbuka biblia inasema kipindi cha dhiki kuu kitadumu kwa siku 1260 Yaani miaka mitatu na nusu ambapo mpinga-kristo atakuwa anafanya mauaji duniani kote, lakini hapa utaona zimeongezeka siku nyingine 30 za ziada yaani (1290-1260=30). Hizi siku 30 zilizoongezeka, ni kipindi kinachojulikana kama SIKU YA KUOGOFYA YA BWANA kwa kuajili ya kujilipizia kisasi kwa waovu wote wakaao juu ya nchi. Ni kipindi kitakachodumu katika hizi siku 30 ambacho kitahusisha mapigo ya vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu. (Ufunuo 16).

Ukiendelea mstari wa 13…utaona kuna siku nyingine tena 45 zimeongezea juu ya zile 1290 na kuwa siku 1335. Hichi kitakuwa ni kipindi cha matengenezo pamoja na hukumu ya mataifa,ambapo Bwana atakuja na mawingu na wafu watafufuliwa wahukumiwe (Ufunuo 20:14).

Hivyo kulingana na ukali wa hiyo dhiki yaani (dhiki ya mpinga-kristo pamoja na mateso ya SIKU YA BWANA) ni watu wachache sana watakaopona (wateule-wayahudi), Biblia inasema katika siku hiyo watu wataadimika kuliko DHAHABU (soma Isaya 13:9-13)

Na kama Bwana Yesu alivyosema katika Mathayo24:

22 “…..kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.”..Na ndio maana utaona ni siku 1335 ambazo ni chache sana ukilinganisha na kama ingekuwa ni miaka 10 hakika asingepona mtu yeyote.

Mwisho wa yote Danieli anaambiwa “12 HERI ANGOJAYE, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.”

Kumbuka ni wayahudi ndio wanaoambiwa HERI wakizifikia hizo siku, hivyo ni uvumilivu na kujificha, na saburi nyingi zinahitajika kwao, pamoja na hekima ya kuzihesabu hizo siku mpaka huo wakati utakapotimia wa Mungu kulipiza kisasi kwa mataifa yote yaliyoshirikiana na yule mnyama ambapo wakati huo Bwana atakapokuja hatarudi peke yake bali atarudi na Bibi-arusi wake(Kanisa) waliokwisha kunyakuliwa kabla ya dhiki kuanza..

Ndipo baada ya hayo utawala wa miaka 1000 utaanza ambapo BWANA atatawala kama MFALME WA WAFALME na BWANA WA MABWANA, na watakatifu wake watakuwa makuhani na wafalme milele na milele. Haleluya.

Je! Ndugu utakuwepo kwenye huo utawala? Je! umeokolewa?, angalia hatari iliyopo mbeleni, shetani anataka ubaki katika hali hiyo hiyo ili siku ile uijutee milele, anataka uzidi kupuuzia ivyo hivyo kila siku, usione kuwa Bwana anakaribia kuja, usipotaka kuacha ulevi,ushirikina, usengenyaji, uzinzi, vimini, suruali, fashion,pornography, kilichosalia mbele yako ni Hukumu tu.

Kumbuka Mungu hapendezwi na kufa kwake mwenye dhambi ..na ndio maana alisema.

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Mpe Bwana maisha yako leo upate uzima wa milele…usiidharau damu ya thamani iliyomwagika kwa ajili yako pale Kalvari.

Na yeye alisema pale msalabani kwa wale waliompokea.. “IMEKWISHA!!”

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Nyinginezo:

SEHEMU YA MAANDIKO ILIYOFICHWA.

UNYAKUO.

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA.

BEI YA UFALME WA MBINGUNI.

MCHE MWORORO.

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Yohana Majinge
Yohana Majinge
2 years ago

Barikiwa sana nimejifunza kitu