Swali: Tunasoma unabii wa Bwana YESU kuwa atakula siagi na maziwa, je ni kwa namna gani hilo lilitimia?
Jibu: Turejee..
Isaya 7:14 “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
15 Siagi na ASALI ATAKULA, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema”.
Siagi inayozungumziwa hapo ni ile inayotokana na maziwa..
Mithali 30:33 “Kwa maana kupiga maziwa HULETA SIAGI….”.
Kwahiyo kusema “Siagi na Asali” ni sawa kabisa na kusema “Maziwa na Asali”.. Hivyo unabii unaonyesha kuwa Mtoto YESU atakula Maziwa na Asali sawasawa ahadi Bwana aliowapa wana wa Israeli kipindi anawapandisha kutoka Misri..
Hesabu 14:8 “Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali”.
Lakini kabla ya kuangalia kwa undani ni kwa namna gani Bwana alikula Maziwa/siagi na Asali, tujifunze kwanza hatua wana wa Israeli walizopitia mpaka kuingia nchi imiminikayo maziwa na asali.
1.KUITWA KUTOKA MISRI.
Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”.
Kutoka 3:17 “Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.”
Na tukirudi kwa upande wa mtoto YESU naye pia aliitwa kutoka Misri, na kupandishwa mpaka nchi ya Israeli wakati akiwa mchanga..
Mathayo 2:14 “Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;
15 akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, KUTOKA MISRI NALIMWITA MWANANGU.”
2. KUFANYA MAPENZI YA MUNGU.
Ili ahadi ya kufaidi maziwa na asali katika nchi ya ahadi ni lazima wawe wanamcha MUNGU na kumpendeza, kwa kufanya mema, lakini kama watafanya mabaya basi hiyo nchi itawatapika..
Kumbukumbu 6:18 “Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa Bwana; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri Bwana aliyowaapia baba zako”
Kwa upande wa wana wa Israeli wapo waliofanya mema wakafanikiwa, na wako waliofanya mabaya na wakaikosa ahadi hiyo ya maziwa na asali, Lakini kwa upande wa Bwana YESU baada ya kupanda kutoka Misri maandiko yanasema alichagua MEMA, na kuyakataa MABAYA hivyo basi akashiriki ahadi ya kula Siagi na Maziwa sawasawa na ahadi ya Bwana..
Isaya 7:14 “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
15 SIAGI na ASALI ATAKULA, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema”.
Umeona?.. kumbe Kristo alijifunza kuyakaa mabaya tangu utoto wake na kuchagua mema?..na hiyo ikawa sababu ya kubarikiwa sana katika nchi ile aliyokuwepo, Kristo hakuishi maisha ya tabu, wala hakuwa na haja na kitu, vyote alipewa na Baba na alishabarikiwa tangu utoto, hakutawaliwa na magonjwa ya Misri, wala shida za kiMisri.
Sasa swali lingine ni hili, ni kwanini hatumsomi Bwana akiwa na mali nyingi?.. sababu kuu ni kwamba hakuwa anajilimbukizia, vyote alivyobarikiwa alivitoa kwa watu, na vingine hakutaka kuchukua, lakini haimaanishi kwamba alikosa, laiti angefungua mlango wa kupokea vyote vya mwilini alivyopewa na Baba na kujilimbikizia, huenda ndani ya siku moja angekuwa mtu tajiri Zaidi ya mtu yeyote aliyewahi kutokea.
Lakini alijiweka katika hali hiyo kwasababu alijua upo utajiri mkuu Zaidi ya huu wa duniani, ambao ataupokea hapo baadaye,
Kwahiyo Siagi na Asali inawakilisha Baraka zote za rohoni na mwilini katika nchi mtu aliyepo, ijapokuwa alijiweka katika hali ya umasikini lakini alikuwa ni tajiri sana, na rohoni alibarikiwa sana kwa Roho Mtakatifu zaidi ya mtu mwingine yoyote, miujiza aliyoifanya ni ya kupita kawaida na neema aliyoibeba ni kubwa sana kiasi cha kumtoa mwanadamu katika hukumu ya milele na kumwingiza katika uzima wa milele.
Na tunapomwamini na sisi tunaingia katika mkondo huo wa Baraka zake, kwanza tutapata uzima wa milele na pili tutapata baraka za mwilini.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Maana ya Mithali 30:33 Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi
About the author