Biblia inatufananisha sisi na kama miti izaayo matunda, hivyo kila mmoja wetu anapaswa azae matunda kwa Mungu, kadhalika biblia imetuonya pia mti usiozaa matunda utakatwa, kama tunavyosoma mfano Bwana wetu alioutoa katika
Luka 13:6
“Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.
7 Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, MIAKA MITATU HII naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?
8 Akajibu akamwambia, Bwana, uuache MWAKA HUU NAO, hata niupalilie, niutilie samadi;
9 nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.”
Mtini huo ulipewa muda wa miaka 3, ili uzae matunda, lakini haukuzaa, hivyo mwenye shamba alitaka kuukata lakini akauongezea neema ya mwaka mmoja zaidi iwe 4 ili kwamba ukizaa katika huo muda itakuwa ni vema lakini usipozaa ndipo ukatwe. Mfano huu ukitufundisha kwamba kila mmoja wetu amepewa muda wa kumzalia Mungu matunda, hichi ni kipindi kilichoanza tangu wakati ule uliposikia kwa mara ya kwanza NENO LA KRISTO katika masikio yako mpaka wakati huu uliopo sasa..Ni dhahiri kuwa pengine imeshapita miaka zaidi ya mitatu, lakini je! Tangu huo wakati uliosikia ulilikubali kwa kulizalia matunda? Au ulilipuuzia na kusema bado bado kidogo?.
Na kama kilishapita kipindi kirefu namna hiyo na bado hujabadilika basi ujue upo katika muda wa nyongeza, na wakati wowote unaweza UKAKATWA. Leo hii umeongezewa neema fupi, Mungu analia kwa nguvu ndani ya moyo wako, uache dhambi, umgeukie yeye, na dhamiri yako inakushuhudia kabisa kuwa unamuhitaji Mungu katika maisha yako, unaona kabisa upo katika vifungo vya uovu na dhambi na bado umesikia injili mara nyingi lakini hutaki kugeuka unaufanya moyo mwako kuwa mgumu, upo katika hatari ya kukatwa.
Kumbuka ni neema za Mungu tu unaishi katika muda huu wa nyongeza, hiyo sauti ya Mungu inayolia ndani yako inayokushuhudia hiyo njia yako sio sawa, haitadumu milele ipo siku itanyamaza,. Usitamani ufikie hiyo hatua kwa maana utakuwa ni wakati mgumu sana ambao hata uhubiriweje Injili hautashawishika tena kugeuka kwasababu umeshakatwa. Hali itakuwa mbaya hicho kipindi kiasi ambacho hata ukifanya uzinzi hautasikia kushitakiwa ndani yako, hata ukiwa mlevi utaona ni sawa tu, ukielezwa mambo yahusuyo wokovu utaona ni hadithi za kutunga, Utaishia kukosoa biblia na watakatifu kila siku kwasababu kifo cha kiroho kimeshakuvaa, mwisho wa siku utakufa na utaenda kuzimu kwenye majuto ya milele.
Utafananishwa na mti uliokatwa na kuangukia shimoni..
Muhubiri 11: 3 “……Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.”
> Ukishakatwa kama umeangukia kwenye ulevi utaishi huko huko mpaka kuzimu.
> Ukikatwa kama umeangukia kwenye uasherati utalala huko huko mpaka ile siku ya hukumu.
> Ukikatwa na kama umeangukia kwenye anasa utalala huko huko mpaka kuzimu.
Hivyo ni vema ukaitendea kazi neema ya Mungu, kwa kuizalia matunda unaposikia NENO lake kwa kumruhusu ayabadili maisha yako mapema angali wakati bado upo.
Mithali 28:13 inasema..” Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”
Tubu mgeukie Mungu,
Neema ya Bwana wetu YESU iwe pamoja nawe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
USIMFANYIE JEURI ROHO WA NEEMA.
WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU
NI HALALI KUBATIZA WATOTO WADOGO?
About the author