Category Archive Mafundisho

KUONGOZA WATU WENYE SHINGO NGUMU.

Haya ni mafundisho maalumu kwa viongozi aidha wachungaji, au wasimamizi ndani ya kanisa..Maadamu una kundi la watu aidha 2-3 au zaidi la kuwasimamia, basi mafunzo haya yatakusaidia sana.

Kutoka 32:9-10

[9]Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu 

[10]basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. 

Mungu alipomuita Musa kwenda kuwaokoa watu wake, alijua asili Ya hao watu watakuwa ni wa namna gani. Pengine Musa alidhani anawaokoa watu ambao ni wema sana, watulivu, na wapole.

Lakini mambo hayakuwa kama hivyo, licha ya kuona miujiza mikubwa namna ile, bahari kupasuka, mana kushuka Mbinguni, miamba kutoa maji, nguzo ya moto kuwaongoza usiku kila siku…

Bado walitengeneza sanamu za ndama na kusema hii ndio miungu yetu iliyotutoa Misri tuiabudu..walinung’unika, walimsengenya kiongozi wao, waliasi na kujiundia Makundi..Ni watu ambao walikuwa ni wagumu kuongoza, wazito kutii na wapesi kulalamika.

Ni vema kujua kuwa kila kiongozi wa kweli kuna siku atapitia kama Musa alivyopitia.. 

Ikifikia hatua hii wengi wanasema kama utumishi ndio huu ni heri niache, kama naonyesha fadhila zote hizi kinyume chake narudishiwa masengenyo na uasi, ni heri niache…

Ukifikiri hivyo bado hujawa kiongozi, Mungu alijua asili yao kwamba ni watu wenye shingo ngumu..alijua Yuda ni msaliti lakini bado alimpatia mwanae, amchunge.

Kutoka 32:9-10

[9]Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu 

Hao hao bado aliwaokoa na akataka wachungwe..

Shingo ngumu ni mtu wa namna gani?. Ni mtu anayefananishwa na ng’ombe ambaye hataki kufungwa Nira na Bwana wake…shingo inakuwa ngumu kuvishwa nira..

Hii ni aina ya watu ambao Hawana utii, hawachungiki, hata waone miujiza mikubwa namna Gani, hata wasaidiweje, si rahisi kuacha tabia zao za usengenyaji, wizi, uasi. Kiburi N.k.

Lakini bado Mungu anawaacha chini ya mchungaji waangaliwe..

Musa alikutana na waabudu sanamu, wanung’unikaji, Na wasahaulifu wa fadhili za Mungu…

Lakini alifanyaje?

Hata pale ambapo Mungu alitaka kuwaangamiza Musa aliwaombea. Alisimama kufanya upatanisho kwa ajili yao.

Ni ujumbe gani tunapewa?

Kiongozi wa kweli badala ya kughahiri kumchunga kondoo wake humwombea kwa bidii ili Bwana amponye asipotee kabisa kwenye dhambi.

Kiongozi wa kweli, huwa tayari hata kupoteza maisha yake kwa kondoo wake.. Musa alisema..

Kutoka 32: 32 Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. 

Uongozi sahihi sio Kuongoza Watu wakamilifu, lakini kuongozo Watu dhaifu Kwa Mungu mkamilifu.

Uongozi Sahihi huweka katika uwiano sahihi “neema na kweli”

Ni vema kufahamu pia si kila wakati Musa alikuwa anasimama kuwatetea Waovu, hapana wakati mwingine aliruhusu upanga wa Mungu upite, Ili dhambi iogopwe…utakumbuka wakati ule walipotengeneza Sanamu ya ndama, na hasira Ya ki-Mungu ilimvaa Musa, ndipo Akazivunja zile mbao mbili, kisha awaita watu walio upande wa Bwana wamfuate, Na wale waliosalia waliadhibiwa vikali kwa mauti.

Dhambi iwapo kanisani, haipaswi kuvumiliwa..Kutoa adhabu na wakati mwingine kuwaondoa wale wabaya ndani ya kundi ili lisiendelee kuharibiwa..

Lakini katika yote wewe kama kiongozi, huna budi kujifunza Uvumilivu, kuwaombea kondoo wako, na kuwa mpole, lakini pia kushughulika na dhambi Vikali katika nyumba ya Bwana. 

Lakini kumbuka ijapokuwa Ni kazi, yenye mapito mengi ya masumbufu na maumivu Lakini thawabu yake na faida yake haifananishwi na gharama ulizoingia.. Hivyo penda kuchunga watu wa Mungu…Ndio heshima ya juu ya upendo kwa Mungu wako.

Mithali 14:4

[4]Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe; Bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi. 

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

TOFAUTISHA KATI YA MAFUNDISHO YA YESU, NA YA WAANDISHI.

MHESHIMU MCHUNGAJI WAKO.

Print this post

UVUKISHE MIPAKA UPENDO WAKO.

Jina la Mwokozi YESU, Ngome Imara libarikiwe (Mithali 18:10).

Hatujaitwa kujipenda tu wenyewe, au kuwapenda wale wenye imani moja na sisi au watu wa familia zetu tu!, bali tumeitwa kuwapenda hata watu walio mbali na imani zetu, tamaduni zetu, na hata itikadi zetu (hao ndio Biblia imewatafsiri kama majirani zetu).

Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Katika Agano la kale ilizoeleka kufahamika kuwa Jirani wa mtu ni Yule wa jamii moja naye, itikadi moja naye, na hata Taifa moja naye, jambo lililowafanya wana wa Israeli wasiwe na ushirika na mtu mwingine yoyote kutoka katika Taifa lingine, na wala wasiwe na upendo na mtu wa Taifa lingine lolote na kuwaona wote maadui (Na kwa wakati huo hawakufanya kosa kwasababu hawakuujua ukweli wote wa Upendo wa Mungu).

Lakini alipokuja Bwana YESU, (mjumbe wa Agano jipya sawasawa na Waebrania 12:24) yeye alitukamilishia kweli yote..na kuwafundisha kuwa majirani zao si tu watu wa Taifa lao, au wanaowajua…

Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Jambo hili Bwana Yesu aliliweka vizuri tena, wakati alipojiwa na yule mwanasheria ambaye alitaka kujionyesha yeye ni mwenye haki (kwamba anawapenda majirani zake) pasipo kujua jirani yake ni nani,

Huyu alipokuja alimwuliza Bwana je! Jirani yangu ni nani?.. kuna jibu Bwana alilompa, tusome..

Luka 10:25 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

26 Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?

27 Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.

28 Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.

29 Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani?

30 Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.

31 Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.

32 Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.

33 Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,

34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.

35 Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.

36 Waonaje wewe, katika hao watatu, ni YUPI ALIYEKUWA JIRANI YAKE yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?

37 Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”.

Kufuatana na mfano huu.. ni wazi kuwa huyu Mwanasheria alijiona kuwa yeye hana upendo kabisa!… Kwasababu hapo Bwana alikuwa anaonyesha kuwa Kuhani na Mlawi ambao walikuwa ni wayahudi, walishindwa kumsaidia myahudi mwenzao, aliyeangukia katika mikono ya wanyang’anyi, na badala yake anakuja kusaidiwa na Msamaria (mtu asiye wa imani yao wala Taifa lao).

Maana yake Yule Msamaria kafanya Ujirani mwema kwa myahudi aliyeangukia kwenye mikono ya wanyang’anyi zaidi hata ya wayahudi wenyewe… Hiyo Ikifunua kuwa ujirani sio tu kwa mtu wa imani moja na wewe, au wa Taifa moja na wewe, au rangi moja na wewe.. hata mtu mwenye itikadi tofauti kabisa na zetu, huyo tumeamriwa tumpende na hata kumfadhili pale inapobidi.

Na ndicho Bwana YESU alichokuwa anajaribu kukipanda kwa wayahudi kwamba kama vile Mungu aliyemtakatifu anavyowanyeshea mvua yake wenye haki na wasio haki, na sisi pia hatuna budi kunyesha mvua zetu za upendo na Baraka kwa wanaofanana nasi na wasiofanana nasi, kama vile Mungu anavyowaangazia Jua lake waovu na wema, na sisi hatuna budi kuangaza fadhili zetu kwa watu wote (wenye haki na wasio haki), huo ndio ujirani mwema.

Lakini tukijifunga kwa imani zetu, jamii zetu, itikadi zetu na kuwadharau wengine wote na hata kutoonyesha upendo, basi tufahamu kuwa tumejifungia wenyewe fadhili za MUNGU.

Bwana Yesu atasaidie sana, kwasababu kwa nguvu zetu hatutaweza.. pale tunapoambiwa “tumpende adui”.. ni jambo zito sana… Lakini kwasababu yupo Roho Mtakatifu aliyewekwa kutusaidia udhaifu wetu, basi tutaweza na kushinda na zaidi ya kushinda..

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.

Maran atha!a

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

IMEANDIKWA NINI KATIKA TORATI? WASOMAJE?

Jina la Bwana YESU KRISTO libarikiwe.

Jenga utamaduni wa kusoma Biblia, siku za mwisho ibilisi anazidi kuwekeza nguvu nyingi kwa watu wasisome wala kulielewa Neno, badala yake wapende tu kusikiliza mahubiri au kufanyiwa maombezi, lakini si Kusoma.

Lakini ukweli ni kwamba tukitaka kuisikia sauti ya Mungu ya wazi kabisa, njia ni kusoma Neno, tukitaka kumwona Mungu suluhisho ni kusoma Neno, tukitaka kumwelewa Mungu katika viwango vingine jawabu ni kusoma Biblia, tukitaka kuishi maisha ya kumpendaza Mungu,ni kusoma tu maandiko. Usipuuzie kamwe kusoma maandiko.

Hebu tujifunze kwa Bwana YESU wakati ule alipokutana na Yule mwanasheria ni maneno gani alimwambia…

Luka 10:25 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

26 Akamwambia, IMEANDIKWA NINI KATIKA TORATI? WASOMAJE?

27 Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.

28 Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi”.

Zingatia hayo maneno  katika mstari wa 26, ….IMEANDIKWA NINI KATIKA TORATI?…. WASOMAJE?

Najiuliza kwanini Bwana Yesu hakumpa jibu la moja kwa moja, lakini badala yake anamrudishia swali.. “IMEANDIKWA NINI KATIKA TORATI?…. WASOMAJE?”  maana yake kama angesema siju, ni  wazi kabisa Bwana YESU asingempa jibu lolote, badala yake angemwambia akasome maandiko (akatafute katika maandiko)..Na leo hii wengi tunamwuliza sana Bwana maswali ambayo majibu yake yapo kwenye maandiko…..

Tukimwuliza Bwana swali ambalo jibu lake lipo katika biblia, anaweza kujujibu kama tu alivyomjibu huyu mwana sheria…. IMEANDIKWA NINI KATIKA BIBLIA?…. WASOMAJE?

Hatuwezi kumlazimisha MUNGU azungumze kitu ambacho tayari alishakizungumza katika maandiko…tukimwuliza kitu ambacho tayari kipo ndani ya Biblia tunaweza tukapokea jibu kama hilo hilo tu… IMEANDIKWA NINI KATIKA BIBLIA?…. TWASOMAJE?

Na kitu pekee anachohakikisha shetani tusikijue ni  UWEZA WA MUNGU pamoja na UWEZA WA MUNGU katika hayo maandiko.. kwa namna gani?

Marko 12:24 “Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?”

Weka ratiba ya kujifunza Biblia mtu wa Mungu, usiishie tu kusikiliza mahubiri, usiishie tu kusikiliza maombi.. bali soma soma soma.. Wakati mwingine unaweza ukawa unapitia vipindi ambavyo hujui nini cha kufanya, huo ni wakati wa kusoma Biblia utapokea ni nini cha kufanya huo wakati..

Unaweza kupitia wakati ambapo hujui uombe nini, soma Biblia utapata nini cha kuombea n.k

Nabii Danieli alikuwa sana kimaarifa na hata kujua nini cha kuoma kwa kusoma maandiko na si tu kutegemea maono yake na njozi zake.

Danieli 9:2 “katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.

3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.

4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake”

Na zingatia: Kusoma Biblia si tu kutafuta neno moja la siku na kutembea nalo hilo, acha hiyo desturi!. Neno la Siku liwe ni ufupisho wa kingi ulichokisoma.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kwanini biblia ni neno la Mungu?

Kitabu kifupi katika biblia ni kipi, na ujumbe wake ni upi?

Je biblia inatufundisha tuwe wapole kiasi? (Wagalatia 5:22-23)

Je kuna haja gani ya kuamini biblia iliyoandikwa na watu?

Mistari ya biblia kuhusu sadaka

Print this post

USIMPE MWANAO VITU SASA.

Huu ni mfufulizo wa mafunzo maalumu ya wazazi kwa watoto..

Ukiwa kama  mzazi, Njia bora ya malezi, sio kumjali mtoto wako, kwa kila kitu sasa.. Hata kama ni haki yake kukipata, Usiwe mwepesi kumfanyia kila jambo leo hata kama una uwezo wa kumfanyia, Usimjali sasa, mjali kwa baadaye. Tumia nguvu hizo kumwekezea kwa baadaye lakini sasa shughulika naye kitabia, kinidhani, ki-utu..Acha hiyo tabia ya kujali-jali  utamuharibu mtoto.

Wengi wetu tunashindwa kujua, kuwa ni kanuni ya ki- Mungu mtoto aishi kama mtumwa, hata kama yeye ndio mrithi wa yote.

Wagalatia 4:1 Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;
bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba

Mzazi mwenye Akili na maono bora kwa wanawe, haangalii mali zake anazitumiaje kwa mwanawe sasa, bali huangalia tabia gani anamjengea leo, ili kesho aweze simama vema maisha yake, au mali zake.

Embu fikiria vema, yule Baba Tajiri aliyekuwa na wana  wawili, ambao kwa siku nyingi waliishi na baba yao bila kuona faida ya utajiri wa baba yao. Mpaka siku moja mmojawao (yule mdogo) uzalendo ukamshinda, akamwambia baba yake nipe sehemu ya mali yangu inayoniangukia, hatimaye akapewa akaondoka, lakini maisha yaliyopo-mgeukia hali ikawa mbaya, mwishowe akazingatia kurudi kwa baba yake. Na baba yake akampokea akamfanyia karamu kubwa. Lakini yule mwana mwingine aliporudi mashambani, na kuona sherehe kubwa kwa ndugu yake, akachukizwa, ndipo akamwambia baba yake “Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, Lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;”

Tusome;

Luka 15:11-31

11 Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;
12 yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.
13 Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
14 Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.
15 Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
16 Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
17 Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
19 sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.
21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.
22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;
23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;
24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.
25 Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.
26 Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?
27 Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.
28 Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.
29 AKAMJIBU BABA YAKE, AKASEMA, TAZAMA, MIMI NIMEKUTUMIKIA MIAKA MINGAPI HII, WALA SIJAKOSA AMRI YAKO WAKATI WO WOTE, LAKINI HUJANIPA MIMI MWANA-MBUZI, NIFANYE FURAHA NA RAFIKI ZANGU;
30 lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.
31 Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.

Nataka uone sifa ya huyo baba, kwa wanawe, ijapokuwa alikuwa na mali, lakini hakutaka Watoto wake, waishi kwa mali zake, bali waishi kama watumwa wengine. Sio kwamba alikuwa anawatesa, Hapana, alikuwa anawatengeneza ili baadaye wakishajua maisha hasaa ni nini kivitendo, ndipo awaache huru, wapewe vyote na baba yao, wafurahie maisha wayapendayo.

Leo hii imekuwa kinyume chake, utaona mtu ndiye anayetumia nguvu zake, na mali zake, kumdekeza mtoto, kama yai, kumletea wafanyakazi ndani, wawapikie, wawafulie, wawapigie deki, na pasi, wenyewe wakae wakitazama muvi Netflix, na kucheza magemu, kwenye Ipad, na computa,

Akidhani anamlea mtoto, kumbe anamlea mwana-mpotevu. Mtoto akikosea tu, hawezi kuadhibiwa, mzazi anasema sitaki mtoto wangu ateseke kama mimi nilivyoteseka, kwani ni nani kakwambia mtoto akiadhibiwa ni lengo la kuteswa? Watoto hawafundishwi kufunga, hata kwa sehemu (nusu siku), au kupelekwa mikesha mara moja moja wajifunze kanuni za kiroho, wazazi wanasema  hawa bado wadogo. Hivi ni kazazi gani tunakilea??

Si lazima kila siku ale mboga saba, si lazima umpe chakula anachokitaka yeye, siku nyingine fululiza ugali maharage, wiki mbili nyumbani, mwache alie, mpaka azoee..Mambo kama hayo  unaweza kuona unamtesa mtoto, lakini ndio njia sahihi ya maleza..unamtengeneza mtu imara sio lege-lege.

Likizo inapofika, kuliko kumpeleka beach kwenye mapembea, na masherehe, mpeleke kijijini kwenu, aone mazingira ya asili, ale vyakula vya kule, atumie vyoo vya kule ambavyo sio vya kuflash, aende akakatie ng’ombe majani, aende na wafungaji machungaji akae huko mpaka likizo iishe, ndipo arudi..

Lakini wewe mwenyewe huku nyuma unajua ni nini unafanya, ukimwandalia akiba, nzuri, ili baadaye atakapoelimika kiroho na kimwili, ukimpa vya kwako, au ukimdekeza atakavyo, ataweza kujisimamia mwenyewe, na kuwa mtu mkakamavu thabiti, na Jasiri, mwenye utu na kiongozi awezaye kuishi katika jamii, na kuwajali na walio wanyonge na wenye shida.

Hayo ndio malezi bora ya mtoto. Mfanye leo mtumwa ili kesho awe mfalme, lakini ukichagua kumfanya leo mfalme, jiandae kesho kuwa mtumwa mfano wa mwana- mpotevu.

Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NI NINI KINATOKA KINYWANI MWA MTOTO WAKO?

MRUDI MWANAO NAYE ATAKUSTAREHESHA

NAFASI YAKO WEWE MAMA KWA MTOTO NA WAJUKUU WAKO NI IPI?.

Print this post

Biblia inaposema watu wakali hushika mali sikuzote, ina maana gani? (Mithali 11:16)

JIBU: Tukiangalia mwanzo wa mstari huo, unasema..

Mithali 11:16 Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.

Ukitazama tafsiri nyingine maana iliyonyooka zaidi ya mstari huo, unasema “mwanamke wa adabu huheshimwa daima, lakini watu wakali hushika tu mali”.

Yaani unalinganisha, sifa njema, na vitu vingi, akilinganisha mwanamke anayewekeza maisha yake katika tabia nzuri, matokeo yake heshima itakuwa kwake ambayo itadumu daima, lakini mtu mkali anayewekeza katika kujilimbikizia mali isivyo halali, akiwakandamiza wengine, akitumia ukali, akiwanyima mshahara wengine, ni kweli na yeye atapata matokeo yake ambayo ni mali nyingi tu. Lakini hana heshima yoyote nyuma yake. Haachi kitu chenye thamani kitakachoweza kuwa faida kwa wengine, hana la kuigwa, hana la kusifiwa isipokuwa, malalamiko, uchungu na machozi kwa wengine.

Hivyo andiko hilo linalinganisha sifa njema na mali. Ni heri  ujijengee sifa njema ambayo hiyo itafuatwa na vizazi hata vya mbeleni, kama vile tuwaonavyo wanawake wacha Mungu kwenye maandiko, mfano wa Ana binti Fanueli, Mariamu, Sara, watu kama  akina Ayubu, Danieli, Yusufu, ambao njia zao huigwa hata sasa, kuliko kuwa kama Nabali aliyetajirika lakini mpumbavu, hana chochote cha kuigwa na watu.

Ni heri maskini ahubiriye watu, na kuwaleta kwa Kristo, wanaacha dhambi, na kupokea Roho Mtakatifu, kuliko mtu yule ambaye kutwa nzima anachowaza ni kujiwekezea nafsi yake, kuiba, na kudhulumu, kutumia ukali kupata mali mambo ambayo yataishia hapa hapa tu duniani.

Mithali 22:1 Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Tafsiri ya Mithali 3:27 inayosema ‘Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao’

Maana ya Mithali 29:9 Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha. 

Maana ya Mithali 26:2 Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake,

Print this post

KUSHAWISHWA HAKUTOSHI, AMINI KIKAMILIFU!

Mtume Paulo, alipokamatwa kule Yerusalemu na kupelekwa mbele ya wafalme kuhukumiwa, tunaona ujasiri wake ulikuwa wa ajabu, badala atumie nafasi ile kujitetea, kimahakama, kinyume chake alitumia nafasi ile kuhubiri injili, kiasi cha kumfanya mfalme Agripa kushawishwa kwa muda mfupi kuiamini injili.. Ujasiri wa namna hiyo hakika, ni wa kuigwa sana.

Matendo 26:28

25 Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.
26 Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.
27 Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.
28 AGRIPA AKAMWAMBIA PAULO, KWA MANENO MACHACHE WADHANI KUNIFANYA MIMI KUWA MKRISTO.
29 Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.

Lakini Tunaona jambo moja, huyu mfalme Agripa alichomwa sana na maneno ya mtume Paulo, alishawishwa ipasavyo na injili ile, lakini hakuwa tayari kugueka moja kwa moja kwa Kristo, aliishia tu kushawishwa.. Ukweli ni kwamba mtu katika hatua hiyo bado hujaokolewa..

Ni sawa na leo hii, watu wengi wanapoisikia injili, ni kweli wanashawishwa, wanaiheshimu, wanaifurahia, wanachomwa mioyo yao, wengine wanaomboleza na kuhuzunika juu ya dhambi zao, lakini je! Wameikubali na kutii?

Utaona wataishia tu kusema, nimebarikiwa!, wataishia kusema Neno zuri linaonya!, wataishia kusema, Mungu nisaidie, nimeguswa leo, ndugu hiyo haimaanishi kuwa umeokoka, huna tofauti na Agripa.

Watu walioshawishwa kwelikweli, waliochomwa mioyo, ni lazima utaona kuna kitu cha ziada watafanya watauliza “Tufanyeje ndugu zetu?”

Matendo 2:  37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, TUTENDEJE, NDUGU ZETU?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.
41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.

Umeona?, hawakuishia tu kusema “asante Petro kwa Neno” hawakuishia kusema “ubarikiwe mtumishi” ..“Umetujenga mchungaji”. Walisema, tutendeje ndugu zetu?..Tuchukue hatua gani?

Utaona Wakabatizwa, wote siku ileile, wajazwa Roho, Wakadumu katika fundisho la mitume, kila siku. Ndio hao walioisambaza injili ulimwenguni kote.

Leo ndio tunahitaji kuona Kundi la watu wa namna hii, ambao wanachukua hatua ya kumpokea Yesu kikamilifu na kumfuata kwa mioyo yao yote, kimatendo. Na sio kama akina Agripa, ambaye hakuwa na matunda ya kuitii injili.

Saa ya wokovu ni sasa, usiseme kesho nitaokoka, hakuna wokovu wa kesho, acha kujidanganya, bali ni leo. Aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi usifurahie mafundisho, usifurahie miguso ya ki-mahubiri swali ni je umeokoka? Kristo leo akirudi utaenda naye?

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.

WOKOVU NI SASA

Na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. 

Print this post

KATIKA NJIA IITWAYO NYOFU.

Sauli (Mtume Paulo) alipokuwa anaelekea Dameski kwa lengo la kuwafunga na kuwatesa watakatifu, kama tunavyoifahamu habari alitokewa na Yesu njiani, mwanga Mkali ulimpiga machoni, akashindwa kuona, Wakamchukua mpaka ndani ya mji akiwa kipofu.

Lakini tunaona alipokuwa kule, hakuwa katika hali ya kawaida, bali katika maombolezo makubwa rohoni, hakula chakula chochote, wala maji..(maana Yake alikuwa katika mfungo), lakini si hilo tu zaidi sana alikuwa akiomba dua.

Baada ya hapo tunaona jambo lingine likitokea mtu mmoja aliyeitwa Anania anatokewa na Yesu, kisha anaagizwa amfuate Paulo. Lakini eneo analoagizwa ni katika njia iliyoitwa NYOFU… 

Maana Yake “njia iliyonyoka”.

Matendo 9:8-12

[8]Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. 

[9]Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. 

[10]Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. 

[11]Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; 

[12]naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. 

Unaweza kujiuliza kwanini apelekwe njia ile ..tena iitwe kwa jina la NYOFU na si lingine labda “njia kuu”, au “nzuri” au “panda” bali nyofu?

Ni kwasababu rohoni, Kristo huwaweka watu wake Katika hiyo njia. Njia iliyonyoka.

Hapo mwanzo Paulo alikuwa katika njia iliyoharibika, mbovu, ya kuupinga ukristo, ya uuaji, ya utukanaji, ya dhambi, ya mauti.

Lakini alipokutana na YESU, akatolewa huko akawekwa katika njia iliyonyooka ya utumishi wake.

Ni ajabu kuona watu wengi leo wanampinga Kristo, hawataki kuokoka, wakidhani udini ndio utawanyooshea mapito yao, fedha ndio zitawasawazishia mabonde Yao, elimu ndio zitaangusha milima yao.

Kumbe hawajui kuwa njia iliyonyooka ni maisha ndani ya Kristo tu!. Kwingine kote ni mabonde, milima Na mwishowe shimoni na mauti. Hakuna pumziko Nje ya Kristo.

Yohana mbatizaji aliliona hilo akapaza sauti yake kwa nguvu Akisema..

Yohana 1:23

[23]Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. 

Kumwamini Yesu ndio kuinyoshe njia ya Bwana..

Je upo katika njia ya nyofu.

Okoka leo, uponywe kila kitu ndugu, kumbuka Umepotea nje ya Kristo,hakuna mjadala na huo ndio ukweli, hakuna tegemeo kama Yesu hajakuokoa. Fanya haraka utubu, leo uiamini kazi ya Kristo ya ukombozi iliyokamilishwa kwa ajili yako pale msalabani. Muda ni mchache mlango wa neema hautadumu Milele.

Ikiwa upo tayari leo kumkabidhi Yesu maisha yako. Basi bofya bofya hapa kwa mwongozo wa sala ya toba. >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Jehanamu ni nini?

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Print this post

HIVI UNAMTESA MWOKOZI WAKO?

Sauli, Sauli, mbona waniudhi? 

Kuna mambo unaweza ukayafanya ukadhani ni sawa machoni pako. Lakini kumbe hujui kama unaleta huzuni kubwa kwa Kristo.

Mtume Paulo ambaye hapo mwanzo aliitwa Sauli, alikuwa akishindana na mawazo,  na jamii ya watu waliomwabudu Mungu akidhani anashindana na ubaya kumbe anashindana na Kristo mwenyewe.

 mpaka alipokutana  na Kristo mwenyewe njiani alipokuwa anakwenda Dameski..akaambiwa maneno haya..Sauli, Sauli, mbona waniudhi? 

Matendo 9:4-5

[4]Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? 

[5]Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. 

Hilo Neno waniudhi, kwenye tafsiri ya asili linamaanisha hasaa “wanitesa”?  Biblia ya kiingereza inaeleza vizuri zaidi inatumia neno “persecutest”…yaani kutesa..

Sasa haya ni Makundi mawili yanayomtesa Kristo.

  1. Wasioamini
  2. Waamini wanao-rudi nyuma

Paulo alikuwa mfano wa wapagani  waliomtesa Kristo, pale alipokuwa anawaburuta watakatifu, anawafunga, anawapinga, na kuwatukana…hakujua kuwa anamtesa Kristo mwenyewe..Leo hii makundi ya watu wanaowapinga watakatifu, wanaoyapinga makanisa ya kweli, wanaowatukana watumishi wa Mungu, wanaowapiga na kuwaua wafahamu kuwa wanamtesa Kristo.

Ikiwa wewe ni mmojawapo kuwa makini, uache mara moja, ni heri utubu leo umpe Yesu maisha yako. Akuokoe.

Lakini  kundi la pili ni wale waamini- waliorudi nyuma. Mtu ambaye ameshaokoka, Halafu anaiacha Njia kwa makusudi anayafanya yale machafu aliyoyaacha nyuma huyo anamtesa Kristo, tena yale mateso ya msalabani kabisa.

Waebrania 6:4-8

[4]Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, 

[5]na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, 

[6]wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri. 

[7]Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu; 

[8]bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa. 

Acha tabia ya kuzoelea dhambi, ukishaokoka ukitenda dhambi, haihesabiki kama kosa kama la wapagani bali uasi.  

Kama Ulimpokea Kristo ili umtese, kuokoka kwako kuna maana gani? Ulishawahi ona mtoto anampiga Baba yake?  Hiyo si laana?

Ndivyo ilivyo kwako unapozini na huku umeokoka, unapokunywa pombe na kufanya anasa.. Tubu haraka sana umrudie Kristo

Penda utakatifu, Ishi maisha matakatifu..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Kwanini Yeremia ailaani siku yake ya kuzaliwa? (Yeremia 20:14)

Nini maana ya Mithali 16:30 Afumbaye macho, kusudi lake ni kuwaza yaliyopotoka; 

Print this post

Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana

Mariamu alipotokewa na Malaika na kuelezwa habari ya mambo ambayo hayawezekaniki kibinadamu, alionyesha tabia ya kitofauti sana…hakuanza kubisha, Hakuanza kukinzana na kusudi na mpango wa Mungu juu yake, ulio juu ya upeo wa ufahamu wake, kinyume chake aliukubali, tena si Kwa maneno ya juu juu tu, bali kwa ukiri wa utumwa…akasema

“Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”

Maana yake ni kuwa ikiwa jambo hilo linanilazimu kulitumikia mimi nitafanya hivyo kama Mtumwa..

Luka 1:34-35,38

[34]Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?

[35]Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu…

[38]Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Mariamu ni kielelezo kamili cha mwanamke thabiti wa kikristo, lakini sio tu mwanamke bali bali kwa kanisa la Kristo kwa ujumla.

Utii wa namna hii ndio Bwana anaoutaka kwa watu wote wamchao yeye..

Ijapokuwa kibinadamu haikuwezekana, akijua pia ikishatokea itamletea aibu katika jamii, atakaposadikika amepata ujauzito, kimiujiza hakuna atakaye mwelewa, watasema ni mzinzi, akijua pia kuna majukumu mengine mazito yatafuata..bado alilipokea kusudi la Mungu..lililo juu ya uwezo wake.

Hakukubali kuingia kwenye kosa kama la Musa, kusema mtume mwingine, hakulimbikia kusudi la Mungu kama Yona kukimbilia Tarshishi…bali alilipokea zaidi ya mtumwa.

Si ajabu kwanini Bwana alimpa neema kubwa namna ile…

Ndugu/kaka Bwana anatazama Utayari wako zaidi ya uwezo wako, anatazama utii wako zaidi ya umri wako.

Kila mmoja wetu leo, aliyeamini katika agano jipya ameitwa kufanya MAKUBWA mfano tu wa Mariamu…Hakuna hata mmoja ambaye hajaitwa kwa ajili ya mambo makubwa ya Mungu… kwasababu Mungu ni Mungu wa miujiza na yaliyoshindikana.

Isipokuwa Imani zetu ni haba Kwa Mungu ndio maana hatuoni matokeo makubwa. Kinachohitajika ni kujiachilia tu kwake..kisha kumwacha yeye atende kazi zake ndani yetu.

Haijalishi wewe ni mwanaume au mwanamke, mzee au kijana, una elimu au huna elimu, tajiri au maskini.. kubali kujiachia kama Mariamu katika kusudi lolote la Mungu.. unapoona una nafasi ya kuombea wagonjwa Fanya hivyo, una nafasi ya kuwashuhudia watu mitaani, masokoni, viwanjani fanya hivyo, huko huko Bwana atajifunua kwako kwa namna isiyo ya kawaida. Na Utukufu utamrudia yeye.

Kumbuka tu Mungu amechagua kutumia vyombo Dhaifu kukamilisha kusudi lake timilifu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je Mariamu alikuwa na umri gani alipochukua mimba ya Bwana YESU?

JE BIKIRA MARIAMU ALIKUFA?

USICHELEWE KUMPAKA BWANA MARHAMU!

Print this post

ZINGATIA MOYONI MWAKO.

Jina la Bwana YESU libarikiwe.

Mungu huwa anasema nasi mara nyingi mioyoni mwetu, lakini huwa hatuzingatii na mwisho wake tunaingia katika matatizo.

Matokeo ya kutozingatia sauti ya Mungu ni makubwa, hebu tujifunze kwa mwana mpotevu, aliyeomba urithi kwa Baba yake.

Luka 15:11 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; 

12 yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. 

13 Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati”. 

14 Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. 

15 Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 

16 Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. 

17 ALIPOZINGATIA MOYONI MWAKE, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. 

18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako”

Nataka tuone huo mstari wa 17, unaosema.. “ALIPOZINGATIA MOYONI MWAKE”.

Maana yake tayari sauti ya MUNGU ilikuwa imeshaanza kumsemesha muda mrefu sana moyoni mwake, kwamba njia anayoiendea sio sahihi, mambo anayoyafanya ni mabaya na hivyo ageuke, lakini hakuwa ANAZINGATIA hiyo sauti.

Na kwa kadiri alivyokuwa anaipuuzia ndivyo mambo yalivyozidi kuwa mabaya, mpaka siku alipoamua kuizingatia.

Inawezekana sauti ya MUNGU inasema nawe moyoni mwako muda mrefu (dhamiri inakushuhudia), usiiendee hiyo njia, usiendelee kufanya hayo unayoyafanya, lakini huzingatii, leo anza kuzingatia sauti ya MUNGU, na geuka acha hiyo njia, mrudie Baba yako, mpe Mungu moyo wako…

Mithali 23:26 “Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu”.

Zingatia sauti inayokuambia UOMBE, zingatia sauti inayokuambia ufunge, Zingatia sauti inayokuambia usome Neno, zingatia sauti inayokuambia Usamehe, zingatia sauti inayokuambia mtumikie MUNGU, wakati mwingine zingatia hata sauti unayokuambia uhame hapo ulipo…

Matokeo ya kuikaidi hiyo sauti ni mabaya, ni kama hayo ya Mwana mpotevu na yale ya Yona.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Print this post