Hekalu la kwanza kama tunavyofahamu lilitengenezwa na Mfalme Sulemani, Ni hekalu lililochukua kipindi cha miaka 7 mpaka kukamilika, na kitu cha kipekee tunachoweza kujifunza katika ujenzi wa lile hekalu ni jinsi uundwaji wake ulivyokuwa. Maandiko yanatuambia katika kipindi chote cha ujenzi, hakukusikika mlio wa nyundo, wala shoka au mlio wa nyenzo yoyote ya ujenzi. Tunasoma;
1Wafalme 6: 7 “Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, IKAJENGWA KWA MAWE YALIOKWISHA KUCHONGWA CHIMBONI; WALA NYUNDO, WALA SHOKA, WALA CHOMBO CHA CHUMA CHOCHOTE, SAUTI YAKE HAIKUSIKIWA ILIPOKUWA IKIJENGWA NYUMBA”.
Unaweza ukajenga picha ni JENGO la aina gani hilo linajengwa pasipo kusikika kelele ya aina yoyote ile?, ni wazi kuwa litakuwa limejengwa kwa utashi wa hali ya juu sana ambao kwa namna ya kawaida haujazoleka katika ujenzi tulionao..
Ghafla tu wananchi waliokuwa wanakaa Yerusalemu wakati ule walishangaa JENGO hili hapa limeshakamilika, wakati wanadhani kwamba jengo ndio linaanza kujengwa, kumbe hawajui kuwa ndio linakaribia kumalizika..kwasababu wakati wa ujenzi wake wenyewe walitegemea wasikie milio ya nyundo, na mashine, na mashoka, na misumeno, na sauti za kelele nyingi za wafanyakazi, ili wajue kuwa ujenzi ndio unaanza lakini mambo hayakuwa hivyo. Kwa nje! Ilionekana kama ni kazi iliyolala tu,
Lakini biblia imetupa siri ni kwanini haikusikika kelele wakati wa ujenzi wake, tunasoma hapo juu ni kwasababu “mawe ya ujenzi yalikuwa yanachongewa mbali sana huko machimboni na kukamilika huko huko kisha kuletwa eneo la ujenzi, tayari kwa kuchomekwa tu! kimya kimya.”..Muda wa mamiezi mengi ulipotea huko machimboni kuchonga miamba, lakini baada ya kukamilika kipindi cha ujenzi kilichukua muda mfupi sana.
JAMBO HILO LINAFUNUA NINI KWA WAKATI WA SASA?.
Kama biblia inavyosema Kanisa la Kristo ni Hekalu la Mungu,(1Wakorintho 3:16). Na kama vile Sulemani alivyokuwa analijenga Hekalu lile, vivyo vivyo YESU KRISTO naye analijenga HEKALU lake, ambalo ndilo kanisa takatifu (bibi-arusi safi).
Na kama vile lile la Sulemani lilikamilika ndani ya miaka 7, kadhalika na hili la Kristo nalo linakamilika katika nyakati 7 za kanisa (Ufunuo 2&3). Na kama vile watumishi wa Sulemani walivyokuwa machimboni duniani kote kutafuta na kushughulika na uchongaji wa yale mawe vivyo hivyo na Bwana Yesu Kristo leo amewatuma watumishi wake waaminifu duniani kote kuwatengeneza watu wake wateule kwa ujenzi wa mwisho kanisa lake tukufu litakalokwenda kukamilika hivi kwaribuni kwa tukio la unyakuo…[hao ndio yale mawe yachongwayo machimboni]
Na kama vile mwishoni mwa mwaka wa 7 jengo la Sulemani lilikamilika na utukufu wa Mungu kushuka mwingi juu yake siku ile. kadhalika na hili kanisa la mwisho la 7 la Laodikia tunaloishi mimi na wewe, ndio tutakalolikamilisha HEKALU la Mungu kisha kumalizia na unyakuo siku ile, jiwe la mwisho litakapoletwa eneo la ujenzi (yaani kondoo wa mwisho atakapoingia katika neema ya msalaba).
Hii inatuonyesha wazi kuwa hatua za UNYAKUO hazitajulikana na watu wengi [yatakuwa ni mambo ya siri]…Wakati watu wanadhani kwamba kanisa la Mungu bado sana linyakuliwe, hawajui kuwa ndio lipo katika hatua za mwisho mwisho, wakati wanasubiri waone na wasikie milio ya matarumbeta na maonyesho, na kushuka moto, hawahafamu kuwa mawe yalishakamilika kuchongwa tangu mwambani.
Ndugu Leo hii Mungu anawaanda watu wake Ki-binafsi, (yaani mmoja mmoja)..na sio kimkusanyiko au kidhehebu, Mungu hawaandai watu kama shirika au jumuiya au kusanyiko hapana, Mungu anamwandaa mtu wake ki-binafsi.
Unaweza ukadhani sasa hakuna watu wa Mungu duniani, kwasababu haulioni kanisa lililosimama lenyewe kikamilifu mbele za Mungu, lakini jua tu kanisa halisi la rohoni la Kristo linazidi kuimarika siku baada ya siku. Na moja ya hizi siku litakamilika, hapo ndipo watapokusanywa wote kwa pamoja kama mtu mmoja na kukutanika mawinguni kwenda mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo.
Mambo ya ulimwengu huu yanatufundisha, kwenye dunia tunayoishi sasahivi ya teknolojia na utandawazi, watu mfano wakitaka kukutanika kufanya vikao, wengi wao hawatumii zile njia za kale tena. Yaani zile njia za kuitana kwa matangazo na kutangaza kila mahali, na kwenda kukodi makumbi ya mikutano, na vipaza sauti n.k. kiasi kwamba hata wale ambao kikao hicho hakiwahusu wanapata taarifa, siku hizi sio hivyo tena majira yamebadilika, watu wanatumia mitandao kufanya vikao vyao.
Mtu mmoja anaweza akawa yupo nyumbani kwake, mwengine yupo nchi nyingine, mwingine yupo ofisini, mwingine yupo chuoni n.k. lakini wote wakitaka kukutanika kufanya kikao wanakutanika mitandaoni na kumaliza mambo yote, na kutimiza malengo yale yale kama tu vile wangekutanika kimwili. Cha msingi tu kila mmoja awe na kifaa husika kitakachoweza kuwakutanisha wote pamoja, na kifaa hicho kinaweza kikawa ni simu, au kompyuta. N.k.
Vivyo hivyo na katika ukristo sasahivi, Ufalme wa mbinguni unayo hekima kuliko ufalme wa duniani. Kristo naye anakusanya wateule wake duniani kote, kwa njia ya utulivu na hekima nyingi, isiyojulikana na wengi..Ni wale tu watakaokuwa na chombo maalumu kitakachoweza kuwaunganisha wote pamoja na Mungu wao kama vile simu ndio watakaoelewa kinachoendelea katika ratiba ya ukombozi ya Mungu.
Na chombo hicho si kingine Zaidi ya BIBLIA (NENO LA MUNGU), na kama vile simu isiyokuwa na network au chaji inakuwa ni sawa na kazi bure, kadhalika Neno la Mungu lisilovuviwa na ROHO MTAKATIFU ndani ya mtu linakuwa ni kazi bure. Ndivyo maandiko yanavyosema.
2Wakoritho 3:6 “….. kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.”
Na ndio maana ni muhimu kuwa na ROHO MTAKATIFU katika kizazi hichi tunachoishi, hiyo ndiyo tiketi pekee ya kuunganishwa katika mtandao wa watakatifu..Hata siku ile watakapoitwa juu mbinguni uwe pia ni mmojawapo wa watakaoisikia sauti ya Mwana wa Adamu. Vinginevyo, unyakuo utakuwa kwako kama ni kitu cha kushtukiza tu.
1Wathesalonike 5: 1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.
5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.
6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.
8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.
9 Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; “
Na JE! NA WEWE NI JIWE LINALOCHONGWA CHIMBONI SASA??…Au unasubiria wakati Fulani ufike ukagongelewe kwenye jengo?…Jenga maisha yako kwa Kristo sasa, utubu dhambi zako, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na uwe ni kwa jina la YESU KRISTO ndipo upokee kipawa cha ROHO MTAKATIFU. Ambaye yeye atakuwa kama network na chaji ya simu zetu..
MAANA SIKU ILE KANISA LITAKAPONYANYULIWA JUU, HAKUTASIKIKA KELELE WALA TAHARUKI YOYOTE DUNIANI..ITAKUWA NI TENDO LA GHAFLA TU!..ee!! fulani hayupo!!, mbona sikuwahi kumwona kama alikuwa ni mtu wa dini sana? Ee!! Mbona tulitazamia tuone kwanza jambo fulani likitokea duniani? Hawajui kuwa mawe yalikuwa yanachongewa machimboni.
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
About the author