Utaachaje kula kucha?..dawa ya kuacha kula kucha ni ipi?..Je ni kweli tatizo la kula kucha haisababishwi na mapepo?..Je mtu atahukumiwa kwa kosa la kula kucha?..Karibu tujifunze pamoja kwa kuongeza maarifa juu ya mambo haya ili yaweze kutusaidia kuishi kwa amani na furaha..
Tatizo la kula kucha limekuwa limewakabili watu wengi..Na endapo ikitokea mtu anakula kucha mpaka ukubwani na anapojaribu kuacha inashindikana..basi ni rahisi kujihisi kuwa na kasoro fulani,.. Na wakati mwingine kujihisi kwamba kuna roho fulani inayomsukuma kufanya hivyo..na hivyo kumpotezea ujasiri.
Kula kucha ni kitendo ambacho mtu anakuwa katika hali fulani ya kiakili labda mawazo, au katika hali ya kutafakari kwa kina, au katika hali ya kuona aibu, au katika hali ya upweke sana, au furaha sana, au huzuni sana n.k inatofautiana kati ya mtu na mtu….ambapo mtu akiwa katika hali hiyo anajikuta vidole vimefika mdomoni pasipo hata kujijua..Na ufahamu unaporudi anajikuta tayari kashapunguza kiwango fulani cha kucha au nyama pembezoni mwa kucha. Atajaribu kuacha lakini kesho itajirudia hiyo hali…
Kwanza ni muhimu kufahamu utendaji kazi wa roho za mapepo…ndipo turudi kuamua kama ulaji kucha ni mapepo ndani ya mtu au la!..
Mapepo yanapomwingia mtu kazi ya kwanza yanayofanya ni kumfanya yule mtu awe mwovu…Mapepo yakiwa ndani ya mtu yanamfanya asipende kusoma Neno,..yanamfanya atamani kutenda dhambi, yanafanya kuwa mwasherati,..mtazamaji pornography, mtukanaji, mlawiti..yanamfanya avae vibaya (Nusu uchi)..Yanamfanya mtu anaposikia habari za injili anachukia..
Na mapepo yanampeleka mtu siku zote mbali na kweli ya Biblia…yanampeleka mtu mahali pasipo kuwa na MAJI YA UZIMA (Jangwani) Soma Luka 11:24..Na mahali ambapo watu wamekufa kiroho kama disko, bar, kwenye kamari, kwenye vikao vya usengenyaji, penye mikusanyiko ya watu wenye mizaa n.k sehemu hizo katika roho ni makaburini…Bar ni makaburi ya kiroho, disko ni makaburini, kadhalika na madanguro na sehemu nyingine zote za kiulimwengu..
Marko 5:1 “Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. 2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;”
Marko 5:1 “Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.
2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;”
Kadhalika mapepo yakiwa ndani ya mtu yanaweza kumsababishia ugonjwa fulani au udhaifu fulani,..Udhaifu huo unaweza ukawa ulemavu wa viungo au ulemavu wa kiakili, au kiufahamu… kama wa kushindwa kujizuia kufanya kitu fulani.
Ulemavu wa kiufahamu inahusisha mtu kula vitu visivyoliwa, ufahamu wa huyo mtu unampeleka kula vitu ambavyo sio kawaida mwanadamu kuvila…kwamfano mtu utakuta anatamani kula chuma, mwingine anakula sindano, mwingine anakula glasi, mwingine makaratasi, mwingine nyama mbichi unakuta hajisikii kabisa hamu ya kula nyama iliyoiva…mwingine mchanga, n.k mara nyingi watu wa namna hii wanakuwa na roho fulani inayowasukuma wao kufanya hivyo hata kama hawajijui..na ndio roho hizo hizo zinazowasukuma watu kupata hamu ya kuvuta sigara, bangi na hata kunywa pombe…Hivyo suluhisho ni kufunguliwa…ambapo tutaona namna ya kufunguliwa na hizo roho mwishoni mwa somo hili..
Kwamfano wanawake wajawazito kutamani kula udongo (ingawa sio wote) lakini wengi wao,..sisemi udongo gunia zima..hapana bali ile hamu ya kula kiwango kidogo cha udongo..hiyo haisababishwi na mapepo bali maumbile..Mwanamke akishajifungua hiyo hali inakwisha…
Kadhalika hali ya kuvutiwa kula udongo wakati mvua kunyesha…Harufu ile ya udongo inawavutia maelfu ya watu na hata wakati mwingine watu wanafikia hatua ya kulamba kidogo udongo..Hiyo pia haisababishwi na mapepo bali maumbile ya miili yetu jinsi yalivyoumbwa.
Pia hali ya kupenda harufu ya petrol au mafuta ya taa na kutamani kuyala..Hiyo pia haisababishwi na mapepo bali maumbile..
Lakini mambo yote haya..ni kwa kiasi, yakizidi sana kufikia kumfanya mtu anywe lita za petroli au kula magunia kadhaa ya udongo hilo ni tatizo lingine ambalo linaweza kusababishwa na roho za mapepo..hivyo tendo la kiroho linahitajika haraka kuliondoa tatizo hilo.
Sasa tukirudi katika suala la kula kucha..
Asilimia kubwa ya watu wanaokula kucha ni tatizo la kiufahamu, ambalo chanzo chake sio mapepo…Wengi wanachukua tabia hiyo kutoka aidha kwa wazazi au ndugu zao au marafiki pindi wanapokuwa wadogo na kuendelea nayo hivyo hivyo mpaka kufikia hatua ya kuwa sehemu ya maisha yao.
Tabia ya kula kucha haina tofauti sana na tabia ya kula kifuniko cha kalamu au kulamba lamba lips, au kung’ata ng’ata meno…Ni tabia ambazo mtu alipokuwa aidha mtoto au mtu mzima, alimwona mtu fulani akifanya na hivyo yeye naye akajikuta anaiga pasipo kujitambua na hivyo kuwa ni tabia yake..
Hivyo tatizo la kula kucha sio mapepo..Hautasimamishwa kwenye kiti cha hukumu kwa kosa la kula kucha…
Kumbuka; Tunapozungumzia kula kucha hatumaanishi kula vidole mpaka vitoke damu zitoke kama bomba, au kula nyama ya vidole mpaka vidole vichuruzike damu kabisa..hapana. Hali kama hiyo ikitokea basi kuna roho nyingine ya adui inahusika hapo…Lakini kama ni kwa kiwango cha kawaida kama cha watu wengine unaowafahamu hilo halisababishwi na mapepo..
Utaachaje kula kucha? (Zingatia mambo makuu mawili yafuatayo).
KWANZA: Ni kumkabidhi Yesu maisha. Ukitaka kuondoa tabia yoyote katika maisha yako…Kwa nguvu zako huwezi, ni lazima uhitaji nguvu za ziada…Wewe mwenyewe umeona!..Umepambana sana lakini bado…Hiyo ni kuonesha kwamba sisi wanadamu kwa nguvu zetu hatuwezi kufanya lolote…Hivyo mkabidhi Yesu Kristo maisha yako ili kwamba akusafishe na kukufanya mtu kamili…Tubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, tubia uasherati kama ulikuwa mwasherati, rushwa, wizi, ulevi, uvutaji sigara, rushwa, ukahaba, anasa n.k..Na ukishaacha..Hakikisha unakwenda kutafuta ubatizo sahihi kama hujabatizwa..Ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote kwenye maji mengi (Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu Kristo (kulingana na Matendo 2:38)…Na baada ya hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukusaidia kufanya yale ambayo ulikuwa huwezi kufanya.
Usiokoke tu kwasababu unataka kuacha kula kucha..Hapana bali okoka kwasababu unahitaji kubadilishwa maisha yako na Bwana Yesu na unataka kuwa mkamilifu kama Mungu.
Mwambie Bwana Yesu katika sala..wala usifunge wala usiingie kwenye maombi ya mkesha…Mwambie tu..“Bwana kuanzia leo sitaki kula kucha nisaidie”..Basi hivyo tu!..Ukishafanya hivyo..Hatua inayofuata ni ya muhimu sana….NENDA KANUNUE NAIL-cutter au Nail-clipper..kama hufahamu nail cutter ni nini Tazama picha chini..
Unapoacha kula kucha, kucha zako zitaanza kukua na hivyo usipozipunguza kwa kifaa maalumu ni rahisi kushawishika kurudia kuzipugnuza kwa meno..Hivyo ili kuonyesha imani yako ipo katika matendo kanunue kifaa hicho, au kingine chochote kile kitakachotumika kupunguza kucha zako zinapokua..Usiwe na hofu wakati mwingine unaweza ukajisahau na kufikisha vidole mdomoni…Lakini kabla hujaanza kuzitafuna Roho atakusaidia kukukumbusha..hivyo unapokumbushwa kubali kutii… na hiyo hali hatimaye itaisha kabisa…haijalishi umekaa nayo kwa miaka mingapi…Itaisha!..Zipo shuhuda za waliomaliza tatizo kwa msaada wa Mungu, na kwako pia litaisha kama utapenda liishe…Na hata kama tatizo lako linasababishwa na roho za fulani za mapepo basi hatua hizi mbili ni dawa tosha ya kuziondoa hizo roho ndani yako..Hauhitaji kuombewa..Wewe fuata hizo hatua hapo juu na tatizo lako litaisha.
Bwana akuabariki.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali share na wengine nao wanufaike.
Mada Nyinginezo:
Ubatizo wa moto ni upi?
JE! MTUMISHI KUTOKUWA NA FEDHA NI ISHARA KUWA KUNA TATIZO KATIKA IMANI YAKE?
LITANIA YA BIKIRA MARIA JE! NI SALA YA KIMAANDIKO?
NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?
Rudi Nyumbani:
Print this post