NENO HILI NI GUMU,NI NANI AWEZAYE KULISIKIA?

NENO HILI NI GUMU,NI NANI AWEZAYE KULISIKIA?

NENO HILI NI GUMU, NI NANI AWEZAYE KULISIKIA?


Tuwe tayari pia kuyapokea maneno magumu kutoka kwa Kristo.

Si maneno yote aliyokuwa anayazungumza Bwana yalikuwa ni mepesi kuyapokea kwa namna ya kawaida,..

Kuna wakati aliwaambia wanafunzi wake,

Mathayo 10:37 “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”

Jaribu kufikiria wakati huo, Kristo alikuwa bado hajasulibiwa, na wala hakukuwa na mtu yeyote aliyewahi kudhani kuwa siku moja atakwenda kutundikwa mtini uchi mfano wa wanyanganyi..Lakini tunaona hapa Kristo anawaambia wanafunzi wake juu ya kujitwika misalaba kana kwamba wanaelewa ni nini maana ya kujitwika msalaba na kumfuata yeye, au walishawahi kumwona yeye akijitwika msalaba wake…

Kwa namna ya kawaida, unaweza ukadhani ni rahisi kulipokea hilo neno,.. ni sawa na leo hii, umsikie raisi anasema mtu yeyote anayetaka nimfanye kuwa waziri ahakikishe kwanza anabeba bomu lake mkononi na kutembea nalo kila siku,.. na muda wowote awe tayari kujilipua…Unaweza kusema raisi anazungumza maneno gani haya..

Ndivyo ilivyokuwa kwa Kristo, misalaba ilikuwa ni kwa ajili ya watu waovu tena wale walioshindikana wenye kesi nzito za mauaji..sasa kusikia eti mtu mwema kama yeye anataja mambo ya misalaba ilikuwa ni kauli tata sana.

Kauli nyingine ya Bwana ni hii:

Yohana 6:53 “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake”

Fikiria tena leo hii mtu anakuambia uule mwili wake, na uinywe damu yake, si utamwona kama ni mchawi?.. Vivyo hivyo na maneno mengine mengi, kama lile alilosema yeye ni chakula kitokacho mbinguni, na bomoeni hekalu hili nitalijenga ndani ya siku tatu. N.k.

Maneno kama hayo ndiyo yaliyowafanya wengi wa wanafunzi wake wasifuatane naye tena..

Yohana 6:60 “Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?

61 Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza?

62 Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza?

63 Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima”.

Je! Na leo hii bado anatenda hivyo?

Hata leo hii Kristo anapowaita watu wamfuate sio kila jambo atalitolea sababu zake siku hiyo hiyo,…wewe unachopaswa kufanya ni kumtii tu na kumwamini maadamu ni mwanafunzi wake,… anapokuambia acha hiki, hata kama hukielewi vizuri leo wewe acha na umfuate, anapokuambia badilisha mavazi yako,tupa vimini, na mawigi, na malipstik na mahereni, usiwaze waze mara mbili anamaanisha nini,….wewe ni kipofu hivyo usijifanye unaona!.

Anapokuambia jitenge na marafiki wa aina hii usianze kuwaza dunia itanionaje, akikuambia acha hiyo kazi unayoifanya, usianze kuwaza Kesho nitakula nini,..Sababu zote hizo atakuja kukupa huko baadaye mbeleni kwa jinsi unavyozidi kutii…lakini kwasahivi mtii kwa kile atakachokuambia ufanye..

Mitume 12, walipoitwa waliambiwa neon moja tu! “NIFUATE”..wakaacha kila kitu hapo hapo na kumfuata, hawakupewa maelezo ya kutosha wanakwenda wapi…

walistahimili maneno magumu kama hayo, mpaka ukafikia wakati wa wao kuelewa sababu ya mambo yote, wengine walishindwa kuyapokea na ndio maana hawakufika Pentekoste, lakini mitume wale 11 wa Bwana na mwingine mmoja wa 12 aliyekuja kuongezeka walitii na ndio maana walifika Pentekoste. Na Mungu akawafanya kuwa nguzo za kanisa.

Sikuzote unapaswa ujue maneno ya Kristo Ni Roho tena ni uzima, hata kama huyaelewi kwasasa.. Ibrahimu aliambiwa akamtoe mwanawe kafara, lakini kwasababu alimwamini Mungu anayemtumikia, akahesabu kuwa Mungu anaweza kumfufua tena mwanae huko atakakokuwa hata kama atakuwa ameshaoza na kuwa udongo,..(Waebrania 11:18-19) hakujali kwamba kitendo anachokwenda kufanya ni kitendo cha kigaidi..lakini alitii, leo hii ndio tunaelewa Mungu alikuwa anafunua nini katika kumwambia afanye vile..Lakini badala ya kupoteza ilikuwa kinyume chake kupata..

Kubali kuipoteza nafsi yako leo kwa ajili ya Kristo, Ukifahamu kuwa siku moja utaipata. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

KARAMA YA MUNGU NI UZIMA WA MILELE.

SIKU ILE NA SAA ILE.

 

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments