MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?: Bwana Yesu alipofufuka, alifufuka na mwili wa Asili..Na kisha baada ya kufufuka tu, mwili wake ule ukabadilishwa na kuwa wa utukufu. Sasa fahari ya miili ya utukufu ni mbali na miili ya asili, kama biblia inavyosema katika…

1Wakorintho 15:40  “Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.

41  Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.

42  Kadhalika na kiyama ya watu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika;

43  hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu;

44  hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.

45  Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.

46  Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho”

Jambo moja lisilofahamika na wengi ni kwamba “hakuna mwili wa utukufu pasipo ufufuo”..Ufufuo unatangulia kwanza ndipo miili ya utukufu inafuata. Watakatifu waliokufa sasa hawana miili ya utukufu huko walipo.

Kwahiyo Hata sisi siku ya unyakuo ikifika kama tutakuwa tumekufa…Siku hiyo roho zetu zitatolewa paradiso kwanza mahali ambapo zilikuwa zimehifadhiwa(yaani Paradiso), tutarudishwa duniani kuvaa miili yetu ya asili ambayo ilikuwa imeoza kwenye udongo..siku hiyo Bwana atairudisha tena (ili litimie lile neno linalosema hautapotea  unywele wenu hata mmoja). Kama mtu alikufa na kansa na nywele zake zote zilinyonyoka siku hiyo atarudishwa na kuwa mzima bila kansa na akiwa na nywele zake zote. Hiyo yote ni Mungu kuonyesha kwamba Mauti haina nguvu juu ya watakatifu..funza hawana nguvu juu ya watakatifu, magonjwa hayana nguvu juu ya watakatifu, ulipoteza mkono na jicho kabla ya kufa, siku hiyo utafufuka ukiwa na mkono wako na macho yako mawili, ulemavu utashindwa n.k

 Tukiisha fufuka na kuwa na miili yetu ya asili isiyo na kasoro hata moja…kufumba na kufumbua tutabadilishwa miili yetu hii na kuwa miili ya utukufu..pamoja na wale watakatifu ambao watakuwa hai watabadilishwa pia. Kumbuka hatutavuliwa hii ya asili ambayo imeshafufuliwa…hapana…bali ni hii hii itabadilishwa na kuwa ya kimbinguni (kwa lugha ya kigeni tungeweza kusema inakuwa upgraded, inavikwa uwezo wa ajabu kutoka mbinguni)..

Au vinginevyo ufufuo utakuwa hauna maana…Kwasababu huko huko tulipokuwepo tungepewa hilo miili ya utukufu…lakini unaona lazima tufufuke kwanza kama Bwana Yesu alivyofufuka..turudi kwenye miili yetu ya asili kisha miili hiyo ibadilishwe..

1Wakorintho 15.51  “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

52  kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

53  Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

54  Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda”

Unaona?..Hii inayokufa itavaa kutokufa..sio kwamba itatoweshwa na kuletwa mingine..hapana ni hii hii..

Sasa miili hiyo itakuwa imevikwa uwezo wa ajabu wa kimbinguni… …Uwezo huo ndio kama ule wa Bwana Yesu aliokuwa nao baada ya kufufuka na ule malaika watakatifu walionao sasa.

Unakuwa unauwezo wa kula na kunywa lakini hauishi kwa kula wala kunywa, Bwana Yesu alipofufuka alikula samaki na wanafunzi wake akatoweka  na chakula kile tumboni mwake lakini hakuishi kwa hivyo na hata sasa haishi kwa hivyo…Na pia mwili huo unakuwa na uwezo wa kubadilika badilika kama Malaika. Bwana Yesu baada ya kufufuka sehemu nyingine alionekana na sura nyingine(Marko 16:12)..sehemu nyingine alionekana kama malaika..(Yohana alimwona kwenye maono akiwa na macho kama miale ya moto), mwenye mavazi yanayong’aa sana.. Hata leo hii Bwana anaweza kumtokea mtu kwa umbo la mwanadamu wa kawaida kabisa akakaa naye na kula naye..na anaweza pia kumtokea mtu kwa umbo kama la malaika mwenye utukufu mwingi na mwanga mkali hata mtu asiweze kumtokea..kama alivyomtokea Mtume Paulo. Hizo zote ni tabia za huo mwili mpya wa utukufu. Na sisi tutakapofufuliwa tutafanana na Bwana Yesu katika kila engo..miili yetu itakuwa na tabia hizo hizo.

Mwili huo pia una uwezo wa kupotea na kutokea  mahali pengine kama Bwana Yesu, na pia una uwezo wa kupaa bila mbawa kama Bwana Yesu alivyopaa mbinguni ndio maana siku ile ya unyakuo tutapaa mbinguni na wengine hawataweza, na una upeo mkubwa wa kujua mambo yote. Na tabia nyingine nyingi, za kimbinguni mwili huo unao…ambazo hatuwezi kuzijua zote mpaka tutakapovikwa miili hiyo.

Hivyo itakuwa na uchungu sana kukosa kuvikwa mwili huo..Itakuwa ni uchungu sana wakati wa unyakuo wakati watakatifu wengine wanafufuliwa sisi tuwe tumebaki mautini. Ni heri tuteseke sasa lakini siku ile hatutateseka…ni heri tuonekane tumepoteza kila kitu hapa lakini mbele za Mungu tuonekane hatujapoteza kitu.

2Wakorintho 5:1  “Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.

2  Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni;

3  ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tu uchi.

4  Kwa sababu sisi tulio katika maskani hii twaugua, tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa, ili kitu kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima”.

 Ni heri uonekane mjinga na mshamba leo kwa kutokuvaa vimini, na masuruali, na kutokuweka makeup, ni heri ukafukuzwa kazi leo kwa kukataa kufanya uasherati, ni heri ukapitia kila aina ya dhiki leo kwa ajili ya Kristo hata ikiwezekana kufa…Lakini Bwana wetu Yesu alisema maneno haya..

Luka 21:17  “Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu.

18  Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu.

19  Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu”.

Bwana akubariki. Kama hujaokoka..Ni vizuri ukafanya hivyo leo, usingoje Kesho kwasababu biblia inasema “hujui yatakayozaliwa ndani ya siku moja”..Kifo ni kama usingizi..hujui saa utakayopotelea usingizini. Hivyo tubu sasahivi hapo ulipo…Jitenge dakika chache jitenge peke yako.Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia.. ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

“Ee mungu baba, naja mbele zako, nikiwa ninajitambua kuwa mimi ni mkosaji na nimekutenda dhambi nyingi, na kwamba nimestahili hukumu. lakini wewe mungu wangu ulisema katika neno lako kuwa wewe ni mungu wa rehema unayewarehemu  maelfu elfu ya watu wanaokupenda wewe. na leo hii ninakuja mbele zako nahitaji msamaha wako na msaada wako mungu wangu, ninatubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha na kwa moyo wangu wote, .

Ninakiri kuwa yesu kristo ni bwana, na yeye ndiye mwokozi wa huu ulimwenguni. hivyo naomba damu ya mwanao takatifu inisafishe uovu wangu wote sasa nifanyike kuwa kiumbe kipya kuanzia leo na hata milele.

asante bwana yesu kwa kunipokea na kunisamehe.

Amen”.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Ulikuwa na miziki ya kidunia kwenye simu yako ifute yote sasahivi usiache hata mmoja, kulikuwa na watu unamahusiano nao ya kiasherati, futa namba zao sasahivi.

Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo namna hiyo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Na kuna Amani fulani itaingia ndani yako ambayo hiyo ndio itakuwa uthibitisho wa wawe kufanyika kiumbe kipya. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali share na wengine.


Mada Nyinginezo:

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

JE NI KWELI MTU ANAWEZA KUTOKA NJE YA MWILI WAKE?.

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

Je! kuna ubaya wowote kuwaombea ndugu zetu waliokufa katika dhambi, Mungu awakumbuke katika ufalme wa mbinguni?.

Kuna Mbingu ngapi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments