MAFUNDISHO YA NDOA.

MAFUNDISHO YA NDOA.

Mafundisho ya ndoa, na mahusiano.


Ikiwa wewe ndio kwanza unataka kuingia katika mahusiano Yapo mambo kadha wa kadha unahitaji kufahamu.

Jambo la kwanza:

ni lazima ujue njia sahihi ya kumpata mwenza wako, vilevile ujue wakati sahihi wa kumchagua huyo mwenza unayemtaka..

Hapa ndipo watu wengi wanapokosea, wakidhani ni yule tu anayevutia machoni huyo ndiye anayefaa, au ni ule wakati tu wanapojisikia kuoa au kuolewa ndio wanapopaswa waingie katika mahusiano. Ukitumia kanuni hiyo upo hatarini sana  kujutia huko mbeleni..Ni sharti kwanza utulize akili yako bila kuruhusu hisia zako kukuongoza..

Ili kufahamu kwa urefu njia sahihi ya kumpata Mwenza wa Maisha Bofya hapa >>NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

Jambo la Pili:

Unahitaji kufahamu Mambo ya kuepukana nayo wakati mpo katika mahusiano ya uchumba. Watu wengi wanadhani ukishamchumbia binti, basi tayari mpo huru kufanya naye tendo la ndoa wakati wowote..Usijaribu kufanya hivyo kwasababu yapo madhara mengi na makubwa ya ndani na ya nje,.Kwanza Licha ya kuwa unafanya uasherati, ambao hata ukifa utakwenda jehanum, Lakini pia unapoteza baraka zote ambazo Mungu alikuwa ameshakuandalia kwa ajili ya ndoa yako inayokuja.. yapo madhara mengine pia,

Ili kufahamu zaidi madhara hayo na jinsi ya kujiepusha nayo bofya hapa >>JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Jambo la Tatu:

Ili ndoa yako iwe ni ya heri na mafanikio, na yenye kupokea baraka kamili kutoka kwa Mungu, Ni lazima ndoa hiyo  iwe imefungishwa na Mungu mwenyewe..Nikisema Mungu namaanisha KANISANI.

Wapo watu wanaosema, mimi nimefunga ndoa yangu kimila, wengine wanasema tumefunga kiserikalini, N.k., Haijalishi hizo zote utaziita ni ndoa, Lakini hizo sio ndoa za kikristo zinazostahili baraka zote za Kristo.

Ili kufahamu faida na madhara ya kutokufungika ndoa kanisani bofya hapa >> NDOA NA HARUSI TAKATIFU.


Sasa ikiwa wewe tayari umeshaingia kwenye ndoa, na umekidhi hivyo vigezo vyote hapo juu.

Basi yapo pia mambo kadhaa unahitaji kujua. Nimekutana na watu wengi wenye matatizo katika ndoa zao. Husasani wanawake, wengine wameachwa na waume zao, wengine wametelekezwa, wengine wao ndio wanamatatizo n.k.k

lakini zipo siri ambazo bado hawajazijua za mafaniko ya ndoa zao ambazo biblia imeziweka wazi..

Kwamfano Ukimtazama Ruthu, yule hakuwa mwanamke wa Kiyahudi kama wengine tuonaowasoma kwenye biblia, lakini jiulize ni kwanini hadi leo hii unamsoma katika maandiko matakatifu,vilevile ni kwanini uzao wake ulibarikiwa kuliko hata uzao wa wanawake wengine waliokuwa wazao wa kiyahudi,? kiasi kwamba mpaka mfalme Daudi, alipitishwa  katika uzao wake,na sio tu wa Daudi bali pia wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa kupitia Yusufu?..

Kama hujafahamu bado siri ni nini , leo nataka nikupe, siri ipo kwa MKWEWE, NAOMI..Hivyo Ili na wewe mwanamke ubarikiwe uzao wako, na uwe na jina kubwa basi siri yako ipo kwa wakwe zako, hilo haliepukiki..

Ili kufahamu Zaidi habari hizo bofya hapa..>>EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.

Vilevile unahitaji kumfahamu mwanamke mwengine anayejulikana  kama ESTA.. Cha ajabu Esta na Ruthu ni wanawake wawili pekee ambao wanavitabu vyao maalumu vinavyojitegemea katika biblia nzima..Lakini cha kushangaza Zaidi ni kuwa wanawake wengi hawajua siri zilizo ndani ya wanawake hawa. Wanakimbilia kusoma habari za  wanaume, kama wakina Daudi, na Eliya, na Samweli, lakini wanaacha mafundisho ya msingi yanayowahusu kutoka habari za wanawake wenzao kama hawa..

Kama ulikuwa hujui Esta, mpaka amekuwa malkia ni kwasababu kulikuwa na mwanamke mwingine ambaye alikosa heshima kwa mume wake ambaye ni Mfalme, na hiyo yote ni kutokana na uzuri aliokuwa nao,..

Hivyo Baada ya mfalme kukiona kiburi chake ndipo akamtoa katika nafasi ya umalkia, na baadaye Esta akapata kibali cha kuchukua nafasi yake, ukisoma pale utaona Esta naye kilichomfanya awe malkia hakikuwa kigezo cha uzuri wake kama wengi wanavyodhani, au elimu yake, au umaarufu wake, hapana, bali kutoka kwa Hegai msimamizi wa mfalme…ambapo kuna  siri kubwa sana hapo unapaswa uifahamu pia wewe kama mwanamke..

kwa maelezo marefu bofya hapa>> ESTA: Mlango wa 1 & 2

Vivyo hivyo na wewe mwanamke, kudhani kuwa uzuri wako, au elimu yako, au fedha zako, ndio zinaweza kukufanya usimuheshimu mume wako, ukweli ni kwamba ndoa yako haitadumu, na atakayeilaani sio mume wako. Bali ni Mungu mwenyewe kwasababu umekosa kufuata kanuni za kimaandiko Mungu alizoziweka juu ya ndoa ya kikristo.

Waefeso 5:24  “Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo”

Vilevile, kama mwanamke unapaswa ujue nafasi yako katika familia, na katika kanisa la Kristo ni ipi…

Tumezoea kuona nyaraka nyingi zilizoandikwa na mitume zikielekezwa kwa makanisa au wanaume kama vile Timotheo, au Tito, au Filemoni, lakini Upo waraka mmoja mtume Yohana aliuandika kwa mama mmoja mteule..Ambao hata wewe mwanamke ukiujua ufunuo wake  utajifunza nafasi yako katika kanisa la Mungu na  uleaji wako wa Watoto.

Bofya hapa ili kufahamu zaidi >> MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

Vilevile na wewe  kama MWANAUME (Baba), ni lazima ufahamu nafasi yako pia katika Familia..

Jambo moja kwako ni hili  Bwana Yesu alisema..

Waefeso 5:25  “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

26  ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;

27  apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.

28  Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

29  Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.

30  Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.

31  Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.

32  Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.

33  Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe”

Ukimpenda mke wako, utamuhudumia, kwa chakula, kwa malazi, na makazi, ukimpenda mke wako utamtunza kwa mavazi, ukimpenda mke wako utawapenda na ndugu zake..Ukimpenda mke wako, utawapenda na Watoto wake, na hivyo utawatimizia majukumu yote ya nyumbani..

Lakini ukikosa akili kama Nabali alivyokuwa, Unakuwa mlevi, hujali wageni, huwi mkarimu, humchi Mungu, wala hutimizii familia yako mahitaji yake, wewe ni pombe tu, Ujue kuwa Mungu atakuuwa mwenyewe kabla ya wakati wako kama alivyomuua Nabali, na Mke wako mwenye akili ataenda kuolewa na mtu mwingine mwenye akili zaidi yako wee na atakayemjali kuliko wewe..kama ilivyokuwa kwa Abigaili mke wa Nabali.. (Soma 1Samweli 25 )

Sasa kwanini hayo yote yakukute?

Hivyo wote wawili mkizingatia kanuni hizo kila mmoja katika nafasi yake, basi muwe na uhakika kuwa Bwana ataifanya ndoa yenu kuwa ya amani siku zote, yenye mafanikio, na yenye matunda kwa Mungu.

Lakini Mwisho kabisa..

Kila mmoja analojukumu lake binafsi la kumtafuta Bwana, na kumpenda Bwana kuliko kitu kingine chochote. Kwasababu Biblia inasema, wakati tuliobakiwa nao ni mfupi..

1Wakorintho 7:29  “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana”

Hizi ni nyakati za mwisho ambazo, biblia inatushauri tujikite Zaidi katika kuutafuta ufalme wa Mbinguni, kwasababu unyakuo upo karibu. Hivyo japokuwa utakuwa katika ndoa lakini usijiingize sana, au kwa namna nyingine usizamishwe sana katika mambo ya kifamilia mpaka ukasahau kuwa kuna wokovu na Unyakuo..Kwasababu hata huyo uliye naye, Akifa leo anaweza kuwa wa mwingine..Na Zaidi ya yote kule juu mbinguni tuendapo hakutakuwa na kuoa au kuolewa, Hivyo masuala ya ndoa si masuala ya kuyapa kipaumbele sana ziadi ya yale ya ufalme wa mbinguni..Lakini yape kipaumbele Zaidi ya mambo mengine ya kidunia.

Bwana akubariki sana.


Mada Nyinginezo:

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

KWANINI WENGINE WANYAKULIWE,NA WENGINE WAACHWE?

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments