Kwanini yesu kristo ni wa muhimu kwetu?
Moja ya majukumu tuliyonayo ni “Kumfahamu sana Yesu Kristo”..Hili ni moja ya jukumu kubwa sana tulilonalo kwasababu ndio msingi wa ukombozi wetu..Tusipomfahamu Yesu kwa mapana na marefu basi ni ngumu kujua nafasi zetu pamoja na Neema tuliyopewa…Na matokeo ya kutomwelewa Yesu ni kuishia kuidharau neema na kupotea.
Sasa jukumu la kumjua Yesu, sio kujua sura yake alikuwa ni mzuri kiasi gani, au alikuwa na rangi gani, au alikuwa na nywele za namna gani, au alikuwa anapenda kula nini?..Hapana hilo sio jukumu tulilopewa la kumfahamu kwa namna hiyo..Jukumu tulilopewa ni KUIFAHAMU VIZURI ILE NAFASI ALIYONAYO. Tukishaifahamu ile nafasi basi tutamjua Mungu sana. Na mpaka sasa hakuna aliyefikia kikomo cha kuijua hiyo nafasi yote..bali kwa siku zinavyozidi kwenda tunazidi kuilewa na ndivyo tunavyozidi kumpenda Mungu na kumheshimu.
Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”
Leo tujikumbushe ni kwa namna gani kifo cha Yesu kilivyokuwa na umuhimu kwetu sisi tuliokuwa tumepotea kwenye dhambi.
Katika Biblia tunasoma muda mfupi kabla ya Bwana Yesu kupandishwa msalabani..Pilato aliwafungulia mfungwa mmoja ambaye alikuwa ni mkatili katika mji ule..Na huyo si mwingine Zaidi ya BARABA.
Huyu Baraba alikuwa na Kesi ya mauaji ya watu kadhaa hapo mjini, na alikuwa ni mkatili..Biblia inamwita “mfungwa mashuhuri” (Mathayo 27:16). Watu wote walimshuhudia kuwa alikuwa ni mkatili, hivyo walikuwa hawamhitaji hata kidogo, hivyo alikamatwa na warumi na kutiwa gerezani akisubiria hukumu yake ipite..Na bila shaka angeuawa kifo cha kikatili kuliko mtu mwingine yoyote yule, kwasababu kila mtu alikuwa amemkinai. Na alivyokuwa kule gerezani kila mtu pamoja na yeye mwenyewe alikuwa anajua ndiye anayestahili adhabu kubwa kuliko wote. Kulikuwa hakuna uwezekano wa kupona hata kidogo…Lakini kama wasemavyo watu “hata mnyororo ulio imara sana, lazima utakuwa na sehemu yake dhaifu”..Hata kama sehemu inaonekana hakuna njia basi Mungu anaweza kufanya njia.
Baraba akiwa mule gerezani labda moyo wake ukaanza kumchoma na kujihisi alifanya makosa, aliua wale watu pasipo hatia, akitazama pembeni anajua kuna mtu aliua tu mtu mmoja na alihukumiwa kukatwa kichwa yeye akijiangalia kashaangusha watu kadhaa huko nyuma hukumu yake itakuwaje?…
Siku moja tu asubuhi alishangaa anaitwa nje, atoke gerezani..na alipotoka akijua anakwenda kuuawa na pengine wafungwa wote wakajua anakwenda kumalizwa kwa hasira nyingi..ghafla anatoka nje anaona watu wengi wanamshangilia nje, wanafurahi kufunguliwa kwake..anaona wanampigia mpaka vigelegele, Baraba afunguliwe! Baraba afunguliwe!… kwa pembeni anamwona Pilato anamwambia kuanzia leo upo huru kama watu wengine, rudi nyumbani kwako kafurahi na mke wako na Watoto wako, upo huru..Wakati anashangaa jambo hilo linawezekanaje labda walikosea wanamaanisha Baraba mwingine…. kwa pembeni kidogo anaona mtu amewekwa taji la miiba kichwani kakaa kimya sana, mpole kama mwanakondoo anayekaribia kuchinjwa….Pilato anamwambia Yule kabeba hukumu yako…Yule atakufa kwa niaba yako…Ni wazi bila shaka alishangaa kidogo..
Naamini Maisha yake yalianza kubadilika kuanzia pale na kuendelea…Kwasababu alijua chanzo cha uzima wake na uhuru wake ni nini?..kwamba kama si Yesu kuwa vile alivyokuwa, kufanyiwa yale aliyofanyiwa, kama sio Yesu kukataliwa yeye angekufa…kwasababu kama Yesu angekubaliwa basi yeye asingepona…Hivyo kwa kupingwa na kupigwa kbbwake Yesu yeye amepona!.
Je mtu wa namna hiyo atarudia tena kuua?, atamkebehi YESU?, Ataudharau msalaba? Atajisifu?…Na je mfano akiudharau msalaba na kutoka pale na kuendelea na mauaji yake unahisi ni nini kitampata mbele za Mungu na watu?
Hiyo ndiyo nafasi ya Yesu kwetu ilivyo… Baraba ni mfano wa mimi na wewe…Sasa ni kwa namna gani Bwana Yesu anachukua dhambi zetu?..Sio kwa kubeba kifurushi na kukiweka mabegani kwake…Hapana ilimgharimu Maisha yake…ilimgharimu kukataliwa, kupingwa, kutemewa mate, kutukanwa, kudhihakiwa..Kwajinsi alivyodhihakiwa sana na kutukanwa sana ndipo thamani ya Baraba kule gerezani ilivyokuwa inazidi kupanda. Hadhi ya Bwana Yesu ilishuka ili yetu ipande.
Wakati Baraba yupo kule gerezani alikuwa hajui kama Kristo anatukanwa huko nje kwaajili yake.
Ndugu yangu…Msalaba sio jambo la kupuuzia au kuchezea hata kidogo…Mambo yote mema unayoyapata leo hii ni kwasababu ya Yesu Kristo, kama sio yeye dunia ingeshaisha siku nyingi…Mungu angeshaimaliza dunia kwa laana kitambo sana…Maisha yangeshaisha miaka mingi sana iliyopita huko nyuma.
Watu wengi hawajui kuwa wanapiganiwa na Mungu pasipo hata wao kumwomba Mungu, wengi hawajui hata katika uasherati wao ni Mungu ndiye anayewapa riziki pasipo hata wao kumwomba, na hawajui ni hiyo neema, ni kwasababu ya YESU KRISTO. Kama sio Yesu kuteseka miaka 2020 iliyopita hakuna mwasherati ambaye mpaka leo angekuwa anaishi..Wote tulistahili kufa.
Lakini Neema hii unaichezea..unadhani ni haki yako kuishi na usherati wako, uwizi wako, ufisadi wako, ulevi wako, uuaji wako, utukanaji wako, usagaji wako, ulawiti wako, uchafu wako n.k Hii Neema ipo siku itaisha na siku hiyo ndipo utakapojua kuwa Hii neema ilikuwa ni ya thamani kiasi gani.
Hii Neema itakapoondolewa, itaondoka na kanisa..watakatifu wataondolewa ulimwenguni, dhiki kuu itaanza, mpingakristo atanyanyuka, ataua wengi na baadaye maji ya bahari na visima na mito yote itageuzwa kuwa damu, utatokea ugonjwa wa majipu ulio hatari kuliko huu uliozuka sasa unaoitwa CORONA. Utasambaa duniani kote hakuna mtu atakayesalimika kwa wale watakaoachwa kwenye unyakuo, wakati huo hakutakuwa na mtu wa kukwambia utubu dhambi zako.
Siku hizo hakutakuwa na masinema tena watu wanayokwenda kuangalia michezo , hakutakuwa na mipira watu wanayokwenda kuangalia, barabara zitakuwa wazi, kila mtu atakuwa peke yake peke yake akiugulia mapigo hayo..Unaona leo ugonjwa huu wa Corona leo ulivyosababisha mabarabara kufungwa, mashule kufungwa, hakuna mtu kwenda kazini kwenye mataifa yaliyoathirika, kila mtu kajifungia ndani..siku hizo itakuwa mara 100 ya hiyo, hata mnyama wako wa kufugwa hutamsogelea, kutakuwa hakuna kutembea mabarabarani..kila mtu anashiriki mapigo hayo kivyakevyake.
Katikati ya gonjwa hilo la ajabu litakalolipuka la majipu…mvua zitaacha kunyesha, jua litashushwa chini, kutakuwa hakuna kitu chochote kilicho kijani kitakachoonekana, mvua ya mawe itashuka, sio ya mawe ya barafu..mawe kama mawe, makubwa kama talanta, kutatokea matetemeko na milipuko ya volcano duniani kote, na baada ya siku za maunguzo ya jua kupita….jua litakuja kuondolewa kutakuwa na giza la ajabu kuliko lile lililotokea kipindi cha Farao, nyota hazitakuwepo, mwezi utaonekana kuwa mwekundu kama damu kwa kipindi kirefu, mambo hayo yote yanakuja ndani ya wakati mmoja..na mambo mengine mengi ya ajabu yatakuwepo, mambo haya sio hadithi za kutunga kasome Ufunuo 16 yote, utaona, na kama unyakuo utakupita basi utayashuhudia hayo yote.
Waebrania 10:25 “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
26 Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;
27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.
28 Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.
29 MWAONAJE? HAIKUMPASA ADHABU ILIYO KUBWA ZAIDI MTU YULE ALIYEMKANYAGA MWANA WA MUNGU, NA KUIHESABU DAMU YA AGANO ALIYOTAKASWA KWAYO KUWA NI KITU OVYO, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?
30 Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.
31 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.”
Kama hujageuka na kutubu mlango wa Neema leo upo wazi…Ni heri usitumie muda ku-comment na ku-like badala yake ukatubu kama hujatubu. Usisome tu kama hadithi ya kukufurahisha, bali ujumbe huu ukawe sababu ya mageuzi kwako..
Na maana ya kutubu ni “kugeuka”..maana yake unadhamiria kuyaacha yale uliyokuwa unayafanya yasiyompendeza Mungu, na unakwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi na kupokea Roho Mtakatifu. Mambo hayo unayafanya kwa moyo wako wote.
Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa > WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
About the author