Shalom jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.
Kuna wakati Bwana Yesu aliwaambia mitume wake maneno haya..
Yohana 12:24 “ Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi..”
Aliwaambia maneno haya, kwanza kutokana na wanafunzi wake kuona wingi wa watu waliokuwa wanamfuata ili waokolewe hususani wale waliotoka mpaka nchi za mbali kuja kumuona na pia alisema vile ili kuwafundisha wanafunzi wake, akijerea tendo, alilolifanya muda mfupi, au siku chache zilizopita,..
Na tendo lenyewe halikuwa lingine Zaidi ya lile la Lazaro..
Kama wengi wetu tunavyofahamu Lazaro alikuwa ni mtu aliyependwa na Yesu sana, alikuwa ni Rafiki wa Yesu tangu zamani, Lakini siku moja aliumwa sana, na taarifa zikamfikia Yesu, Lakini Yesu hakuchukua hatua yoyote, badala yake aliendelea kubaki kule kule mahali alipokuwepo, akamwacha aendelee kuugua mpaka afe,..
Na alipojua ameshakufa, bado hakufanya haraka kurudi siku hiyo hiyo kumuona, bali alingojea tena siku mbili, ndipo baadaye akashuka kwenda Bethania alipokuwa anaishi yeye na Dada zake..Kama tunavyosoma habari alipofika alimkuta ameshawekwa kaburini, anatoa harufu,.(Yohana 11 )
Unaweza ukajiuliza ni kwanini alimwacha mpaka aoze, ni kwasababu baadaye alikuwa anataka kuwafundisha wanafunzi wake kinadharia juu ya huo mstari tuliouona hapo juu, na madhara yake jinsi yatakavyokuwa..
Sasa Bwana Yesu alipofika na kumfufua Lazaro tena, na kumrudisha katika hali yake ya mwanzo tena katika afya Zaidi ya ile aliyokuwa nayo hapo mwanzo, biblia inatuonyesha tendo lile la kufufuka tu kwa Lazaro, lilikuwa ni tendo lililoutikisa ulimwengu wa giza… Yaani kwa ufupi ushuhuda ule wa Lazaro, uliwavuta watu wengi sana kwa Kristo, mpaka kufikia hatua ya wakuu wa Makuhani kutaka kumuua yeye naye (yaani Lazaro)…
Yohana 12:9 “Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu.
10 Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye;
11 maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu”.
Hiyo ni kuonyesha kuwa jinsi gani Lazaro aliyekufa akazikwa akaoza alivyokuwa na athari kubwa katika ulimwengu wa roho, kuliko yule ambaye hakuwahi kupitia hayo.
Jiulize hapo kwanza kwanini Lazaro, hakuwa vile?..Kwanini hakukuwa na mtu aliyemfuatilia, kwanini hakumvuta mtu yeyote kwa Kristo, japokuwa alikuwa ni Rafiki wa Karibu wa Bwana Yesu, tena aliyependwa.
Hata sasa haijalishi mtu anaweza akawa anasema Kristo ni Rafiki yangu kiasi gani, anaweza akawa anakujua kweli kama Lazaro wa kwanza.. lakini hakujui kama Lazaro ambaye alikufa akaoza akazikwa, kisha akafufua tena..
Na ndio maana sasa Bwana Yesu akawaambia wanafunzi wake baada ya tukio lile kipindi kifupi baadaye..
Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi..”
Ndipo mstari huo ulipokuwa chimbuko lake..Akiurejea mfano wa Lazaro..
Ikiwa wewe ulishaokoka lakini hutaki kuwa tayari kufa, na kuoza kwa habari ya dhambi, hata wakati mwingine kuonekana kuwa ni mjinga, au umerukwa na akili kwasababu tu hutaki kufanya jambo Fulani kwa ajili tu ya Kristo, basi huwezi kuwa Lazaro wa pili.Wala huwezi kudai kuwa umezaliwa mara ya pili.. Ikiwa utakuwa unaogopa kuacha kuvaa vimini kisa tu ndugu zako au marafiki zako watakuonaje, watakuita wewe ni mshamba, basi bado huwezi kumletea Kristo mazao yoyote, haijalishi utasema umedumu katika wokovu muda gani..wapo waliodumu na Kristo Zaidi ya sisi mfano Yuda, lakini hakuwa na mazao yoyote kwa Bwana, na mwingine huyu Lazaro ambaye alipendwa pia lakini hakuwa na matunda yoyote kwa Bwana, kwasababu walikuwa bado hawajafa kwa habari ya dhambi.
Ikiwa utaogopa, kuacha Maisha ya uzinzi kisa unawaonea haya hao waasherati wenzako ulionao, na marafiki zako, unaogopa watakuita mlokole, na wewe hutaki kuitwa hivyo, basi ujue mpaka hapo bado hujafa ukaoza ukafufuliwa na Kristo na hautakuwa na matunda yoyote yakumfaa Kristo. Ndugu habari hizi unazisikia kila kukicha lakini bado unafanya moyo wako kuwa mgumu, unazidi kujitoa katika mstari wa neema kidogo kidogo…
Ikiwa kweli tunatamani tuwe na matunda ya rohoni, basi tuwe radhi pia kuiacha dunia moja kwa moja, hiyo ndio kanuni ya Kristo wala hakuna njia nyingine ya mkato.
Kumbuka tena hili Neno
“Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi..””
Bwana atusaidie sote,
Ubarikiwe sana..
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?
Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza
Mstari huu unamaana gani? ″Walakini hautapotea hata Unywele mmoja wa Vichwa vyenu? (Luka21:18)
Ni kwa namna gani Yesu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka?
MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.
About the author