Dalili ya kwanza ya uchanga mkubwa wa kiroho ni hofu ya wachawi…Ukijiona unaogopa wachawi, au “uchawi” huo ni uthibitisho wa kwanza kabisa kwamba wewe ni mchanga kiroho, na Neno la Mungu bado halijakaa ndani yako, haijalishi upo madhabahuni unahubiri kwa miaka mingapi! Bado ni mchanga.. Mtu anayeogopa wachawi au anayewatukuza mno wachawi hana tofauti ni kima anayeogopa kinyago cha mtu shambani, kinachomtishia asile mazao…
Uchawi ni sehemu ndogo sana ya vita vya mkristo!..Idara kubwa ya shetani sio “vitunguli na vibuyu”..Hiyo ni idara ndogo sana ya shetani, ambayo hata pasipo kujijua Mungu tayari anakulinda nayo pasipo hata wewe kujijua. Sasa kama wewe ni msomaji wa biblia hebu nionyeshe mahali popote ambapo Bwana Yesu alizungumzia habari za wachawi/uchawi..au mahali popote alipokuwa anawafundisha wanafunzi wake aliwaonya wajihadhari na wachawi???…
Idara kubwa na kuu ya shetani ni roho ya mpinga-Kristo ambayo hiyo inakwenda kinyume na Kristo…Na hiyo inatenda kazi ndani ya kanisa, na inatumia watumishi wa uongo wanaojigeuza na kuwa kama watumishi wa Mungu! Na inakaribiana sana na roho ya kweli. Ndio hiyo hata Bwana alikuwa anapambana nayo,(ndio ile iliyokuwa inafanya kazi ndani ya mafarisayo na masadukayo) na ndio Bwana aliwaonya sana mitume wajihadhari na hao…
Mathayo 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali”.
Idara hiyo iliwasumbua sana mitume walipokuwa wanahubiri injili, mpaka wengine kuuawa, ilihusika kuwaua wakristo Zaidi ya milioni 80 duniani kote kikatili tangu kipindi cha kanisa la kwanza, inaua rohoni inaua pia mwilini, ndio hiyo hiyo inazungumziwa sehemu kubwa kwenye kitabu cha Ufunuo. Na ndio hiyo itakayokuja kufanya kazi katika kipindi cha dhiki kuu.
Sasa tukirudi kwenye mada..je! Mnyama paka kulia usiku juu ya bati ni uchawi?..
Jibu ni La!..sio uchawi…ukisikia paka analia usiku nje sio uchawi!!!….Paka wanaolia usiku ni kutokana na sababu za mazaliano..(sauti zile wanazitoa ili kuvutia mazaliano)..Paka wa aina yeyote Yule wakati wa mazaliano ni lazima atoe hizo sauti, awe ni paka wa kahaba, awe wa kanisa, au wa mtumishi wa Mungu…ni lazima ikifika kipindi cha mazaliano atoe hizo sauti, na anaweza kutoa wakati wa mchana au wakati wa usiku…na sauti hizo ni lazima zifanane na sauti za watoto wachanga!!…kama hatatoa sauti zinazofanana na za watoto wachanga basi kuna kasoro katika huyo paka!..paka asiye na kasoro yoyote ni lazima atoe hiyo sauti.
Sasa kwanini wanatoa hizo sauti zinazofanana na watoto wachanga???…Ndivyo Mungu alivyowaumba!..kama tu sauti wanazotoa kanga, au mbuzi au kuku wanapofikia wakati wa mazaliano au wakati wa kutaga!!. Na paka macho yake usiku ni lazima yang’ae yanapopigwa na mwanga…Na paka wana tabia zinazofanana na chui..ni wepesi kupenya mahali hata kama ni padogo sana..na wanapotembea si rahisi kusikika, na ni wepesi wa kutoroka mahali kwa haraka, kufumba na kufumbua unaweza usiwaone mahali walipopotelea…ndivyo walivyoumbwa!..(ili sisi tumtukuze Mungu, kwa uumbaji wake), na paka wote tabia zao ni kama za chui kupenda kutembea usiku na sehemu zilizoinuka!..
Kwahiyo ni kawaida kutembea juu ya mabati na ukuta wakati wa usiku, na hata kukimbizana!..na wanatabia pia za kuingia ndani kwa mtu hata kama hawajakaribishwa, hivyo kama hujafunga mlango anaweza kuingia mpaka ndani na hata kuzalia huko…na wanatabia ya kuwa ving’ang’anizi (utamfukuza atarudi tena, na utarudia hivyo mara kwa mara), ndivyo walivyoumbwa!!
Na sio dhambi kufuga paka! wa rangi yeyote Yule (awe mweusi, mweupe, kahawia au yeyote yule), kama ndani una panya wengi!..wanafaa kwa shughuli hizo za kuwadhibiti…au kwa fahari/(kwa kupenda tu) sio dhambi kuwafuga…tena ni vizuri zaidi kama una mapenzi nao!
Na bundi na popo ni hivyo hivyo…wameumbwa kipekee na Mungu (hawatembei mchana bali usiku na vyakula vyao vinapatikana huko huko gizani). Hawa si wanyama wa kufuga ndio maana unawaona wapo kivyao vyao..
Sasa wengi wasiokuwa na maarifa wanakuwa na hofu wanapowaona wanyama hawa wanaonyesha tabia zao hizo za kipekee walizopewa na Mungu, ambazo hazionekani kwa wanyama wengine!…na kuishia kusema ni wachawi wamewatembelea…wanaposikia paka usiku wanalia batini kama watoto wachanga, wanakosa usingizi na kuamini wachawi wamewatembelea!..wanapoona popo wametoka mitini jioni na kutanda angani, wanakosa amani..wanapoona bundi kasimama anamacho kama ya mtu, nguvu zinawaishia kabisa!!…wanajua sasa ni wachawi wanafanya kazi zao!!….kumbe ni kukosa tu maarifa!. Mwisho wa siku wanaishia kuwaua hao viumbe wakidhani ndio wamemshinda shetani!..
Na hiyo inamfanya mkristo kupoteza muda mwingi, hata wiki nzima,au mwezi mzima, au miaka na miaka kupambana katika sala dhidi ya wanyama hao(akiamini kuna uchawi ndani yao)…paka kaonekana kaingia ndani hapo hapo, maombi ya kufunga mwezi mzima yanaanza!..maji ya upako yatakwenda kutafutwa mitaa yote!, kila mtumishi ataitwa!..mwisho wa siku ni hofu hofu kila mahali…kila mtu unayekutana naye unahisi ni mchawi!, nimewahi kusikia watu wanasema na kuamini mende na mijusi, wanatumika kiuchawi!..hivyo ukiona mende ndani kwako ni wachawi kuna nguvu za giza hapo!
Usikose maarifa ndugu, wala usipoteze muda wako kwa vitu visivyokuwa na maana…Ukisikia paka wanalia batini usiku, kama wanakukera toka nje wafukuze! Wataondoka, na muda huo ombea mambo mengine ya muhimu kama, familia yako, kanisa na huduma yako kama unayo, ombea na wengine..usianze kushindana kukemea wanyama hao ambao wapo katika ulimwengu wao..Ukiona kelele za kuku usizozielewa hebu nenda kaulize kwanza uzijue tabia za viumbe hao kabla ya kuchukua maamuzi yasiyokuwa na maarifa!, kama sauti za fisi a zinakukera usiku basi hama nenda maeneo ya mjini hutazisikia kamwe..
Ni hofu tu ambazo shetani anawajengea watu waaamini kwamba yeye ni mkuu kuliko Mungu…ili wamwogope yeye zaidi ya Mungu. Wewe kama ni mkristo, unapaswa uwe na ujasiri na Imani yako useme “wachawi hawana kitu kwangu” Kama vile Bwana alivyosema “shetani hana kitu kwangu”..Kisha endelea kuishi Maisha yako ya kawaida.
Bwana akubariki!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?
ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.
About the author