Zipo siri nyingi za ufalme wa mbinguni ambazo Mungu amezificha katika agano la kale, na ndio maana biblia inatuambia torati ni kivuli cha mambo yanayoendelea katika agano jipya (Waebrania 10:1)..
Kwa mfano embu tuiangazie ile Habari ya Musa baada ya kutoroka Misri na kukimbilia katika jangwa la Midiani, kwa ufupi biblia inatuambia alipofika kule alikutana na binti mmoja wa kikushi (ki-Afrika) aliyeitwa Sipora, Ambaye alifanikiwa kumwoa na akaishi naye kama mke wake kwa kipindi kirefu sana, pengine Zaidi ya miaka 30 Na…
Lakini siku moja Musa alipokuwa anachunga mifugo ya mkwewe kule jangwani baada ya miaka 40 kupita tangu atoke Misri, ghafla alitokewa na Mungu na kupewa maagizo ya kuwarudia tena ndugu zake kule Misri kwa lengo la kuwaokoa. Ndipo Musa akatii mara moja kushuka Misri, lakini kuna jambo nataka ulione pale, kwamba Musa hakuondoka Midiani na kwenda na Mke wake ili ashuhudie lile kusudi la Mungu la kuwaokoa wana wa Israeli..Bali alimwacha kwao, salama akaondoka yeye peke yake Pamoja na Haruni.
Na baadaye Bwana alipomaliza kuwakomboa wana wa Israeli kule Misri kwa mkono wa Musa, na kuwavukisha bahari ya shamu, shughuli yote ile nzito ilipokwisha ndipo tunamwona sasa, Sipora akiletwa na Yethro baba yake kwa Musa kule jangwani..
Unaweza kujiuliza ni kwanini Sipora hakwenda Misri na Musa..
Musa anamfunua Kristo, na Sipora anamfunua bibi-arusi wake..
Sasa kama vile Musa alipowakimbia ndugu zake kule mwanzoni, walipotaka kumshitaki kwa farao, lakini alitoroka na kukimbilia jangwani na huko akakutana na Sipora ndivyo ilivyo kwa Yesu Bwana wetu, ndugu zake wayahudi (yaani Waisraeli)
walipomkataa, akawaacha ukiwa kama maandiko yanavyosema (katika Mathayo 23:27-39), akaenda zake mbali nao, mahali wasipopajua wao (Yohana 7:33-36), ndipo huko huko akakutana na sisi watu wa mataifa, tukapewa neema tusiyostahili ya kufanyika bibi-arusi wa Kristo..
Sisi(watu wa mataifa) tunafananishwa na Sipora kwa Kristo..
Na kama vile Musa alivyotumia muda mwingi wa kuishi na Sipora kabla ya kuwarudia tena ndugu zake, vivyo hivyo na Kristo naye ameishi na kanisa lake takatifu la mataifa sasa kwa takribani miaka 2000. (Ndio maana neema ipo kwetu sasa, sisi watu wa mataifa ndio tunaomtumainia Yesu kuliko waisraeli,..Wayahudi sasa hawamwamini Kristo hata kidogo.)
Lakini siku moja isiyo na jina, ghafla, Musa aliona kijiti kinateketea moto na muda huo huo Mungu akamwambia aondokea arudi kuwaokoa wana wa Israeli ambao walikuwa wanamlilia tangu zamani awaokoe dhidi ya maadui wao.. Ndivyo itakavyokuwa siku ile ambayo Mungu atapowarudishia tena hii neema ya wokovu wana wa Israeli ili waokolewe na maadui zao..Itakuwa ni ghafla tu ya siku moja..
Ipo siku Wayahudi watarudiwa na Mungu tena, na ufalme utarudishwa kwao Soma..
Matendo 1:6 “Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?
7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe”.
Umeona hapo!..maana yake yapo majira yanayokuja ya Mungu kuwarudishia Israeli ufalme!
Siku hiyo Mungu atamtuma Kristo tena ulimwenguni kuja kuwaokoa, lakini hatakuja mikono mitupu kama ilivyokuwa hapo mwanzo, bali atakuja na fimbo mkononi mwake, kuyaadhibu mataifa, na kipindi hicho kitakuwa ni kipindi cha dhiki kuu ya ajabu ambayo haijawahi kutokea duniani..
Mapigo Kristo atakayoyaleta duniani yale ya Musa ni mfano mdogo sana, soma Ufunuo 8,9,16, utaona pale..
Lakini cha ajabu ni kuwa katikati ya mapigo hayo Mke (Bibi-arusi )wa Yesu Kristo hatakuwepo..(kama vile Sipora jinsi alivyokosekana wakati Musa anashuka Misri)
Sasa atakuwa wapi?
Jibu lipo wazi, atakuwa ameshakwenda kwenye unyakuo siku nyingi!!.. Hivyo dhiki zote na mapigo yote hayatamuhusu hata kidogo kama ilivyokuwa kwa Sipora..
Na jambo lingine ambalo ni vizuri ukajua ni kuwa, Bibi-arusi(mke) huwa anathamani kubwa, kuliko ndugu machoni pa mhusuka..Na ndio maana utaona hata pale Haruni na Miriamu ndugu zake Musa walipojaribu kumzungumzia vibaya tu Sipora, Mungu aliwaadhibu saa hiyo hiyo (Hesabu 12).
Hiyo ni kuonyesha kuwa thamani ya kuwa bibi-arusi wa Kristo ni kubwa kuliko kitu kingine chochote.. Unaona ni jinsi gani mimi na wewe tulivyo na nafasi kubwa machoni pa Kristo Zaidi hata ya wale wayahudi unaowaona kule Israeli wanaoishika torati?, Lakini hiyo ni mpaka tutakapokubali kuutii wokovu.
Na kumbuka sio kila anayesema nimeokoka ni bibi-arusi, hapana, kigezo cha kuwa bibi-arusi wa Kristo ni sharti uwe bikra rohoni, yaani umejitenga na mambo maovu, kwa Maisha matakatifu unayoishi na vilevile unao uhusiano wa karibu na Kristo aliyekuokoa.. Lakini sio kwa kutamka tu..
Hizi ni siku za mwisho, Kama bado hujampa Kristo Maisha yako, au haujaitengeneza taa yako vizuri fahamu kuwa Unyakuo upo mlangoni sana, Siku moja inapopita ujue kuwa ndivyo unavyoikaribie ile siku, pengine ni leo usiku, pengine ni kesho tu, pengine mwezi huu hauishi Kristo atakuwa amesharudi..Jiulize akirudi na kukuta katika hali hiyo uliopo, utajibu nini na injili zote unahubiriwa?
Kumbuka aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi.
Wayahudi macho yao yalifumbwa wasimwamini Kristo, lakini siku za mwisho watakwenda kumwamini Kristo atakaporudi kwao (upatapo muda kapitie vipengele hivi Warumi 11 na Zekaria 12)
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author