SWALI: Naomba kuuliza, huu mstari una maana gani? “..VITU VIWILI visivyoweza kubadilika ambavyo kwa hivyo Mungu hawezi kusema uongo”?! (Waebrania 6:18).
JIBU: Shalom..
Tusome…
Waebrania 6:17 “Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati;
18 ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo”
Kama ukianza kusoma kuanzia mstari wa 13 kwa umakini, mpaka mstari wa 18, utajua kuwa Vitu hivyo viwili visivyoweza kubadilika ni AHADI YAKE na KIAPO CHAKE.
Hivyo ndio vitu viwili pekee vya Mungu visivyoweza kubadilisha Neno la Mtu.
Kwa mfano katika Maisha ya kawaida, Mtu akitaka kuthibitisha neno lake Huwa anatoa Ahadi..Kwamfano unaweza kumwambia mtu nitakuja kesho kukutembelea…Na yule mtu ili kupata uhakika zaidi na kwamba hutamdanganya ataweza kukuambia “embu niahidi”..na wewe utamwahidi…Na ili kupata uthitisho ulio mkubwa zaidi anaweza pia kukuambia “hebu Niapie kwamba utakuja”..
Maana yake kwa ahadi uliyomuahidi, na kiapo ulichomwapia…Ni ngumu wewe kuwa umemdanganya! Ni lazima utamtembelea tu kwa vyovyote vile hiyo siku ya kesho, Na hata kama kikitokea kitu ambacho kitazuia safari hiyo, utakapokumbuka kwamba ulishatoa ahadi, na tena ulishaapa, basi unajikuta unatimiza ahadi yako kwa gharama zozote zile.. (Sasa huo ni mfano tu, sisi wakristo haturuhusiwi kuapa).
Vivyo hivyo Mungu, ili kutuhakikishia kuwa Neno lake ni kweli…Neno hilo kaligeuza na kuwa Ahadi, na hajaishia tu kulifanya kuwa ahadi, bali kaenda mbele Zaidi kaliapia…ili kwa vitu hivyo viwili, (Ahadi na kiapo) atuhakikishie sisi Watoto wake kwamba yeye si MWONGO, Maana yake ni lazima atalitimiza tu neno lake alilolitamka kutoka katika kinywa chake.
Ndio maana Mtume Paulo hapo, anachukua mfano wa Ibrahimu, jinsi Mungu alivyolithibitisha Neno lake kwa kumwapia zile ahadi alizompa.
Waebrania 6:13 “Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake,
14 akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza”.
Hivyo Neno la Mungu limehakikiwa kwa “ahadi na kiapo”…kwamfano aliposema kwenye Neno lake
Yohana 16:23b “… Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu”.
Hapo mzizi wa hilo neno ni kwamba “tumwombe Baba” basi, lakini Bwana Yesu akituambia tumwombe tu Baba bila kutupa ahadi yoyote, tusingeamini kwamba tutapata majibu..Hivyo ili kulithibitisha hilo neno, akaongezea mbele yake ya kwamba “tukimwomba atatupa”…hilo neno “atatupa” tayari ni Ahadi…. Lakini hajaishia hapo ili kulithibitisha kuwa hajatudanganya akaongezea na kiapo juu yake na kuanza kwa kusema “Amin…Amin nawaambia”..tukimwomba Baba kwa jina lake atatupatia.
Hivyo tunapomwomba Baba popote pale, tufahamu kuwa ni haki yetu kupokea majibu yetu kama tumeomba sawasawa na mapenzi yake…hajatudanganya!, kwasababu katupa ahadi na kiapo..
Unaweza pia kusoma maneno mengine mfano ya hayo, kwa kuongeza maarifa, kasome Yohana 14:12, Luka 18:29-30.
Zaburi 138:2b “….Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote”
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?
About the author