Shalom karibu tuyatafakari maandiko, leo tutaangazia kile kisa cha Yesu na yule mtu aliyekuwa na mapepo kule makaburini. Pengine ulishawahi kuisoma hii habari mara nyingi, lakini naomba tuisome tena kwa mara nyingine, kwasababu Neno la Mungu halina mwisho wa kujifunza (Zab 12:6). Hivyo usomapo zingatia hususani hivyo vipengele vilivyowekwa katika herufi kubwa.
Marko 5 : 1-19
“ 1 Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.
2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;
3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;
4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.
5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.
6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;
7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.
8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.
9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.
10 AKAMSIHI SANA ASIWAPELEKE NJE YA NCHI ILE.
11 Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha.
12 Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.
13 Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini.
14 Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea.
15 Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa.
16 Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe.
17 WAKAANZA KUMSIHI AONDOKE MIPAKANI MWAO.
18 Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye;
19 lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu”.
Utaona katika habari hiyo, mapepo hayo yalipokutana tu na Yesu, na kuambiwa wamtoke yule mtu, biblia inatuambia yalianza “kumsihi sana Yesu” Yalianza kumlilia na kumwomba kwa nguvu sana na kwa bidii, kwamba Bwana asiyafukuze nje ya nchi ile?.
Ulishawahi kujiuliza ni kwanini hayakutaka kupelekwa nje ya nchi ile?. Sio kwasababu yangeshindwa kuishi, hapana lakini ni kwasababu tayari yalikuwa yameshawezeka mambo yao mengi ya uharibifu katika mji ule, hivyo kuondolewa pale na kwenda kuanzisha uharibifu mwingine ugenini, si jambo dogo itakuwa ni hasara kubwa kwao.
Hiyo inatupa picha kuwa mapepo yamejigawanya kulingana na maeneo ya kijeografia, hivyo yale mapepo yaliyokuwa ndani ya yule mtu, yalijua mchoro mzima wa mji ule, yalijua takribani watu wote waliokuwa katika ule mji, na mipango ya kuwaangamiza.
Sasa tukirudi kwenye habari tunaona, kulikuwa na wale watu wanaochunga nguruwe pembezoni wakitazama kila kitu kinachoendelea, wakayasikia kabisa yale mapepo yakimsihi sana Bwana pale, pengine kwa nusu saa, au lisaa hatujui lakini yalikuwa yanamlilia Bwana kweli kweli, Na mwisho wa siku Bwana hakuyaondoa, aliyaacha yaendelee kubaki tu katika ule mji isipokuwa tu yamtoke yule kichaa.
Hivyo wale watu walipoona vile, wakaenda kuitana kule mijini na vijijini, sasa badala wamsihi Yesu aendelee kubaki katika ule mji ili awasaidie kwasababu maadui zao bado wapo mjini, kinyume chake wao ndio wakaanza kumsihi Yesu aondoke mipakani mwao.?
Unaona hilo? Ni sawa na kusema Ondoka Yesu, tuachie mapepo. Cha ajabu nao pia wakaiga mbinu ya mapepo, ya kusihi, wakamsihi Bwana pale pengine kwa dakika kadhaa..Na mwisho wa siku Yesu akawasikia nao pia, akapanda zake chomboni mwake akaondoka, hawakumpa hata nafasi ya kulala siku moja wala kuingia mjini maili moja, alifika pale ufukweni na kugeuza siku hiyo hiyo.
Tunajifunza nini?
Mashetani nayo yanamwomba Mungu, na Mungu anayasikia. Ukitaka kuthibitisha hilo kasome (1Wafalme 22:20-23, na Ayubu 1:9).
Hivyo yanakuwa na kibali maalumu cha kuendelea kubaki mahali fulani, au ndani ya mtu fulani. Sasa kama sisi tutakuwa ni watu wa kuukataa wokovu, ni watu wa kupinga njia za Mungu pale anapotujia kwa lengo la kutuponya roho zetu..Kamwe usitazamie kama utaweza kushindana na majeshi ya mapepo wabaya.
Wale watu waliona jinsi mapepo yale yalivyokuwa mabaya, kwanza yanawafanya watu kuwa vichaa, pili yanafanya kazi ya kuua, ndio maana utaona yalienda kuwauwa wale nguruwe ziwani, kuonyesha kuwa kazi yao kubwa ni uuaji, lakini walimkataa, Sasa kwa kuwa walimkataa Yesu wakamfukuza, yale mapepo pengine yalirudi kazini yakaenda kuwafanya vichaa wengine hata elfu kumi kwa namna ile, na kusababisha vifo vingi.
Hivyo nasi tujue kuwa tusipomsihi Yesu, mapepo yatamsihi kwa niaba yetu, na yatakuwa na haki kabisa ya kukaa ndani yetu, au katika jamii yetu, au koo zetu, kwasababu Yesu hayupo katikati yetu. Tumemfukuza atoke mjini kwetu.
Mpokee Bwana, hii dunia pasipo yeye hakuna ushindi. Shetani kazi yake ni kuharibu (1Petro 5:8-9).
Kama upo bado nje ya Kristo ni vema ukatubu dhambi zako, umrudie yeye leo, Na kama hujabatizwa basi tafuta pia kufanya hivyo mapema sana.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author