SWALI: Kwanini kila mahali Mungu anasema, “mahali Fulani nitaliweka jina langu au nimeliweka jina langu”, Je ana maana gani kusema hivyo, ni kwamba lile jina lake la YEHOVA, anakuwa analiweka ndani ya sehemu hizo au?
JIBU: Mahali popote Mungu anaposema nitaliweka jina langu, anamaanisha kuwa sehemu hiyo, au kitu hicho amekichagua, au amekiweka wakfu kitumiwe kwa ajili ya aidha kumtangaza yeye , au kuwambudu, au kumfanyia ibada, n.k. hakuna cha zaida.
Hivyo sehemu yoyote au kitu chochote, au mtu yoyote aliyewekwa wakfu na Mungu (au ametiwa mafuta ya utumishi), basi ujue kuwa tayari mtu huyo au kitu hicho Mungu kashakiwekea jina lake ndani yake. Na mtu huyo, au kitu hicho kinapaswa kichukuliwe kwa umakini sana, kwasababu kikighafilikishwa, aidha na mtu mwenyewe, au mtu mwingine ni rahisi kupata adhabu kali sana kutoka kwa Mungu.
* Kwa mfano katika biblia utaona Mungu aliweka jina lake ndani ya malaika wake kwa kusudi la kuwahudumia wana wa Israeli, na hichi ndicho alichowaambia wakiwa kule jangwani;
Kutoka 23:20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.
21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; KWA KUWA JINA LANGU LIMO NDANI YAKE”.
* Utaona tena Mungu aliliweka jina lake pia juu ya wana wote wa Israeli,. Yaani waisraeli wote walikuwa ni wakfu kwa Mungu kati ya mataifa yote ulimwenguni. Hivyo mtu yeyote au taifa lolote ambalo liliwakosesha, au kuwafadhaisha, lilishiriki adhabu kali kutoka kwa Mungu.
Hesabu 6:27 “Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia”.
Mtu yeyote aliyeilaani Israeli, Mungu alimlaani, na yeyote aliyeibariki Mungu alimbariki, kwasababu Mungu aliliweka jina lake juu yao. Hata sasa Baraka hizi na laana zinaendelea kwa yeyote atakayeitakia heri au shari Israeli.
* Utaona tena Mungu aliliweka jina lake, katika lile Hekalu lililojengwa na Mfalme Sulemani pale Yerusalemu.
2Wafalme 21:4 “Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu”.
Hivyo, wote ambao walikuwa wanalinajisi hekalu la Mungu, mauti au adhabu kali walikumbana navyo.
Lakini wakati mwingine Mungu aliahirisha hasira yake juu ya wana wa Israeli, sio kwasababu walimpendeza sana, hapana lakini ni kwasababu tu alishaliweka jina lake ndani yao. Soma vifungu hivi, utaliona hilo, Ezekieli 36:21, Isaya 48:9-12, Ezekieli 20:9-10,
Vivyo hivyo na katika agano jipya, Mungu ameweka jina lake katika vitu kikuu viwili.
Cha kwanza ni Kanisa lake; Palipo na Kanisa hai la Kristo ujue jina la Mungu lipo mahali hapo. Lile ni hekalu la Mungu. Ambapo Mungu amepaweka pawe wafku kwa ajili ya ibada, sala na dua, na shukrani, sasa ikitokea mtu analinajisi kanisa la Kristo, kwa namna yoyote ile, ajue kuwa anashindana na mkono wa Mungu wenyewe, na bila shaka yoyote, atakuwa matatizoni.
Pili, ni Mungu analiweka jina lake ndani ya mwaminio. Yaani ndani mtu aliyeokoka. Mtu aliyeokoka, moja kwa moja anapokea kibali cha Mungu kuja ndani yake, kwa yule Roho Mtakatifu anayeachiliwa juu yake. Hivyo mtu wa namna hiyo anakuwa ni wakfu kwa Mungu, chombo kiteule cha Mungu. Na mtu yeyote akitajiribu kumfadhaisha, atakuwa anajitafutia madhara mwenyewe kutoka kwa Mungu. Kwasababu tayari Mungu alishaliweka jina lake ndani yake.
Na mtu anaokoka, kwanza kwa kutubu, kwa kumaanisha kabisa kuziacha dhambi zake, na pili, kwa kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na Matendo 2:38
Akishakamilisha hayo, Roho Mtakatifu atakuja juu yake, na kuanzia huo wakati, jina la Mungu litakuwa limeshawekwa ndani yake. Na yeye atakuwa mtiwa mafuta wa Bwana.
Je, na wewe upo tayari leo kuokoka? Kama jibu ni ndio basi fungua hapa, kwa ajili ya kupata maelekezo ya namna ya kutubu. >>>> SALA YA TOBA
Bwana akakubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author