Ukoma enzi za biblia ni ugonjwa uliojulikana kama pigo kuu kutoka kwa Mungu, kutokana na dhambi ambazo mtu alizozitenda.
Mtu aliyegundulika kuwa ana ukoma ilikuwa anatengwa na jamii nzima ya Israeli. Anapelekwa mahali ambapo wakoma wenzake walipo, mbali kidogo na makazi ya kawaida ya watu na haruhusiwi kuja kujichanganya na watu wengine asije akawaambukiza wale wasio na ugonjwa huo. Hata familia yake mwenyewe hakuruhusiwa kuisogelea, aliendelea kukaa huko huko, mbali kwa kipindi chote ambacho Mungu atamponya, na kama ikitokea hata ponywa basi maisha yake yote atakuwa ametengwa. Walawi 13.
Lakini ukoma haukuwa tu katika mwili bali ulikuwa pia katika nyumba. Utajiuliza nyumba nazo zilipigwa na ukoma na Mungu? Jibu ni ndio biblia inatuambia hivyo;
Wana wa Israeli walipokuwa jangwani Mungu aliwaagiza, akawaambia watakapoifikia hiyo nchi ya ahadi, na kukutana na nyumba ambayo Mungu kaipiga kwa ukoma, wasiikae, wasubiri kwanza kwa muda wa siku saba, kisha kuhani atakwenda kuingalia, na akiona ukoma ule, umeisha ndipo watakaporuhusiwa kukaa, lakini kama bado upo itakarabatiwa pale palipoathirika, na hapo watasubiri tena, kuangalia, ikiwa umeisha basi watu wataruhusiwa kuingia, lakini kama bado, kinyume chake ugonjwa ndio umezidi tu kutapakaa nyumba nzima..Basi nyumba hiyo yote ilikuwa inabomolewa na kila kitu chake kilikwenda kutupwa nje ya mji.
Walawi 14:33 “Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
34 Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu;
35 ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu;
36 ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, mbele ya kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili kwamba vyote vilivyomo nyumbani visiwekwe kuwa unajisi; kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aitazame;
37 naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta;
38 ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba;
39 siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba;
40 ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji;
41 naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu;
42 kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba.
43 Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa,
44 ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, na tazama, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaokula hiyo nyumba; ni katika unajisi.
45 Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hata mahali palipo na uchafu.
Sasa ni kwanini Mungu aitazame mpaka nyumba na kuipiga kwa ukoma? Kwa wakati ule zipo nyumba ambazo zilijengwa katika damu, nyingine katika dhuluma, nyingine rushwa, wizi, nyingine uzinzi n.k. Sasa nyumba kama hizi, Mungu hakuruhusu watoto wake, wazikae na ndio maana akazipiga kwa ukoma.
Hiyo inatufundisha nini sisi wa agano jipya?
Biblia inatuambia miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, ni nyumba za Mungu. Sasa pale anapotaka kushuka halafu anakutana na vimelea vya ukoma wa kiroho, tunachokisubiria ni nini kama sio kuharibiwa? Anakuja na kukutana na ulevi, uzinzi, uvutaji sigara, ni nini mtu huyo anatarajia kama sio kuuliwa na Mungu.
Anapokuja na kukutana na ushirikina, fitina, utazamaji wa picha za ngono, anakutana na uvaaji wa suruali kwa mwanamke, na nguo za kikahaba, na uchubuaji ngozi, ni nini anakingojea hapo kama sio kuharibiwa?
Kuna watu wanasema Mungu haangalii mwili bali roho, nataka nikuambie mwili wako unathamani kubwa kwa kama tu vile roho yako ilivyo, na usipoangalia na kuutunza utapigwa tu na Mungu, Kama aliweza kuzipiga nyumba ambazo hazina uhai wowote zamani, atashindwaje kuupiga mwili wako ulio na uhai ndani yake.
1Wakorintho 3:17 “Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.
Kama vile nyumba inavyopewa siku saba za kuangaliwa maendeleo yake, kama ukoma utaondoka au utaendelea, vivyo hivyo, na wewe ambaye unaliharibu hekalu la Mungu, usipumbazike kuona mbona hakuna hatua yoyote Mungu anayoichukua juu yangu. Upo wakati Mungu atasema sasa inatosha, mtu huyu hana faida yoyote kwangu, nimwondoe, tu… Anaweza asikuue kimwili, lakini rohoni ukawa mfu aliyeoza anayesubiria tu kufa kwenda kuzimu.
Mungu anatazamia tumzalie matunda katika miili yetu, vinginevyo atatung’oa mara moja, kwasababu kukaa bila kumzalia matunda anatuona kama TUNAMHARIBIA TU NCHI YAKE.
Luka 13:7 “Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?”
Hivyo, tubu mrudie Mungu, hizi ni nyakati za kumalizia, Kristo yupo mlangoni kurudi. Ulimwengu haujawahi kukutimizia furaha ya roho yako. Ni Kristo tu peke yake ndiye anayeweza kukupumzisha na kukuponya.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312 Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
About the author