NGAZI 7 AMBAZO MKRISTO NI LAZIMA AZIPANDE KUUFIKIA UKAMILIFU.

NGAZI 7 AMBAZO MKRISTO NI LAZIMA AZIPANDE KUUFIKIA UKAMILIFU.

Kuokoka tu peke yake hakutoshi, zipo ngazi saba, za kupanda ili kuufikilia ukamilifu Mungu anaotaka kuuona kwako kabla hujaondoka hapa duniani. Tunapomwamini Bwana Yesu, kwa kumkiri na kubatizwa, hatupaswi kuishia hapo hapo tu, kwani biblia inatuonyesha tutakuwa watu wasiokuwa na ushuhuda wowote, kama sio kufa kabisa kiroho.

Sasa kulingana na ufunuo Mtume Petro aliopewa na Roho mtakatifu aliandika mambo saba, ambayo mara baada ya mtu kuwa mkristo anapaswa atie bidii yeye mwenyewe kufanya bila kukawia kawia

Na mambo hayo tunayasoma katika kitabu cha 2Petro 1-12. Tukianzana na jambo la kwanza;

  1. WEMA

2Petro 1:5 “Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, …..,

Tukishaamini, ni wajibu wetu kuonyesha Imani yetu kwa matendo yetu mema katika jamii inayotuzunguka,  na kwa watu wote. Wema ni kitendo cha kuonyesha kujali, kuthamini, nidhamu na uaminifu.

Sio kwasababu watu wa kidunia, hawasalimii wengine, na sisi tusiwasalimie watu, au hawawasaidii watu na sisi tusiwasaidie, hawawaelekezi watu na sisi tuwe hivyo hivyo,  huo sio wema, Halikadhalika wewe kama boss kazini kwako, kwasababu umeona, watu wengine wote wanawalipa wafanyakazi wao mshahara fulani kidogo na wewe unawaiga, huwapandishii  mishahara wa kwako au huwapi bonus kwa kazi wanazokufanyia labda kwasababu hazina elimu kubwa au vinginevyo, huo sio wema, wape tu.. Kumbuka ule mfano Bwana Yesu alioutoa, juu ya  wale watu aliowapeleka shambani mwake saa 11 jioni wamfanyie kazi, lakini kulikuwa na wale wengine waliokuwepo tangu asubuhi, na ulipofika wakati wa malipo walitaka wale waliochelewa walipwe kidogo kuliko wao. Lakini Yesu akawaambia..

Mathayo 20:14 “Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15 Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa MWEMA”?

Unaona? Wema wema kama huu pia ni wa kuigwa, housegirl wako au mlinzi wako nyumbani.

 Barnaba naye alitajwa kama mtu mwema aliyeshuhudiwa na watu wote, kwa vile alivyokuwa anawajali sana ndugu, (Matendo 11:-25), hususani wale waliokataliwa, mpaka akaitwa mwana wa faraja.

Na sisi tunapaswa pindi tunapookoka, tupige hatua moja zaidi, tuonyeshe wema wetu kwa watu, tulionyeshee bidii, Kumbuka hilo ni moja ya matunda 9 ya Roho Mtakatifu yanayozungumziwa  katika Wagalatia 5:22. (Utu wema)

Warumi 12:21 “Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema”.

  1. MAARIFA

Petro anaendelea kusema..

“ 1:5..na katika wema wenu maarifa,”

Tukishakuwa na uhakika sasa wema upo ndani yetu, tupige hatua nyingine mbele ya kuongeza maarifa juu yake. Maarifa yanayozungumziwa hapa ni maarifa ya kumjua Mungu, sio ya kibinadamu.

Wakristo wengi sana tunakosa maarifa haya, na hivyo tunaangamia, hatujui utendaji kazi wa Mungu kulingana na wakati na majira tuliyopo ni upi, na ni nini tunapaswa tufanye. Kwamfano, kutokujua kuwa ipo nguvu ya upotevu iliyoachiwa na Mungu mwenyewe, leo hii duniani ili iwadanganye watu wasiotaka kuitafuta kweli, na kwamba nguvu hiyo inafanyakazi katikati ya manabii wa uongo, kwa kupitia miujiza ya kweli ya Mungu. Sasa kwa kukosa kujua maarifa hayo Kunatufanya tuangamie,.

Vilevile kuhusiana na neema ya wokovu, kwamba haitadumu milele kwetu sisi watu wa mataifa, upo wakati itaondolewa na kurejeshwa kule Israeli, na huku kwetu tutabakia kuwa kama mafarisayo na masadukayo. Hilo nalo halijulikani na wakristo wengi, na ndio maana ukristo unachukuliwa juu juu tu, na watu wengi, kwasababu wanadhani muda utaendelea kuwepo wakati wote.

Na mambo mengine mengi kama hayo, yaliyo katika maandiko. Hivyo Mungu anatutaka tuwe watu wa kujifunza Neno lake kila siku, na kuyachunguza maandiko na kwa kuwa tunaye Roho wake mtakatifu ndani yetu atatusaidia kuyaelewa yote, na siri zote na mpango wote wa Mungu unaoendelea nao katika wakati wetu huu tunaoishi.

Hivyo hiyo ni hatua ya pili ya ukomavu, kuhakikisha maarifa ya ki-Mungu yanajaa ndani yetu.

  1. KIASI

“1:6 na katika maarifa yenu kiasi”,

Sasa tukishakuwa na maarifa, tunapaswa tuongezee juu yake kitu kingine kinachoitwa kiasi. Wapo wakristo ambao wamekamilika katika maarifa na utu wema, lakini kiasi hawana, hawawezi kujizuia kwenye baadhi ya mambo, mpaka mwisho wa siku mambo hayo yanageuka kuwa kama dhambi kwao. Utakuta mtakatifu anawaza muda wote kazi za mikono yake, mpaka anakosa muda wa kuwa faragha na Mungu, Na wakati anapopaswa afanya hivyo anasema amechoka, atasali siku nyingine, ataendea ibadani wiki nyingine?

Au mwingine, anashikilia sana kufanya mambo yasiyomjenga, kama vile kutazama Tv, Au kuchati, au kuperuzi internet kuangalia vya kidunia tu..na atatumia muda wake mwingi huko, kufanya hayo mambo, lakini kwenye kusali atatumia muda mchache.

Biblia inatuambia sisi tulio wa mchana tuwe na kiasi (1Wathesalonike 5:8). Ili tupate muda wa kuwa karibu na Mungu wetu.

  1. SABURI

“1:6…Na katika kiasi chenu saburi”,

Anasema, tukishajifunza kuwa na kiasi, basi tuongezee na saburi pia. Saburi, ni uvumilivu/ustahimilivu katika Imani. Tukikosa  utahimilivu hususani pale tunapopishana na majaribu, ni ngumu sana kusonga mbele. Ni rahisi mtu kuacha Imani kwasababu anapitia njaa, au kwasasa hana kazi, au  yupo katika mazingira  yasiyofaa ya kubanwa, au ananyanyaswa na watu.

Mtume walikuwa wanafungwa na kupigwa, lakini bado walikuwa wanaendelea kuhubiri injili, kule kule walipofukuzwa.

Kukosa saburi, kwa ajili ya shida za kiulimwengu ambazo huwa hazidumu, ni ngumu sana kufikia kiwango ambacho Mungu alikitarajia kwetu, Vilevile kutokuwa wavumilivu katika huduma, au Imani, ni jambo ambalo linawakwamisha wakristo wengi sana, pale wanapoona matarajio yao hayajatokea kwa wakati walioupanga basi wanakata tamaa. Tumeaswa tusifike huko, tujifunze kuwa na saburi, kwasababu saburi ni mpango wa Mungu kwetu.

Warumi 5:3 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;

4 na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;

Hivyo hili jambo pia tulihifadhi ndani ya mioyo yetu. Tuliruhusu liwe na nafasi yake. Kwasababu hizo ndio ngazi za kufikia ukamilifu wa Kristo.

  1. UTAUWA

“1:6…na katika saburi yenu utauwa”.

Utauwa ni tabia ya uungu. Mungu ni Mtakatifu, hivyo ili na sisi tuwe na uungu ndani yetu tunapaswa tuwe watakatifu, Lazima tujizoeshe kuishi maisha ya utakatifu ya kuikataa dhambi, na mambo yasiyofaa.

1Petro 1:16 “kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu”

Ili tuweze kuishi maisha hayo tunapaswa tuwe watu wa maombi, watu wa kufunga, watu wa kuwatangazia wengine habari njema. Huo ndio utauwa ambao hata Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa nao. Lakini kama hatutakuwa waombaji, bado hatukifikia kiwango hichi cha utauwa Bwana anachokizungumzia hapa.

  1. UPENDANO WA NDUGU

“1:7 na katika utauwa wenu upendano wa ndugu,”

Sasa ikiwa utauwa umeshakamilika ndani yetu, jambo lingine ambalo tunapaswa kulionyeshea bidii ni upendano wa ndugu. Kumbuka hatua hizi huwezi kuzifikia kama yale ya chini hayajakamilika kwanza.

Upendano wa ndugu unaozungumziwa hapa sio ule wa ndugu wa kimwilini, hapana, bali ndugu katika Kristo. Tunapaswa tufikie hatua hii ya kupendana sisi kwa sisi kama wakristo. Jambo ambalo limekuwa gumu sana kufikiwa na wengi wetu wa leo, kusengenyana, kurushiana maneno, kuumizana, kana kwamba hatujaokolewa na Bwana mmoja.

Hivyo tujitathimini sana, tugeuke, kwasababu mambo haya hayahitaji maombi bali bidii.

1Petro 1:22 “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo”.

Unaona, unahitaji bidii ili kuupata.

7)  UPENDO

“1:7…na katika upendano wa ndugu, upendo”.

Upendano wa ndugu ni tofauti na huu upendo unaozungumziwa hapa. Upendo huu ni upendo wa Ki-Mungu, ambapo mtu akiufikia huo basi mtu anakuwa karibu sana na Mungu, au kwa namna nyingine anakuwa anamjua sana Mungu.

Upendo huu ni upendo usio na masharti, kwamba kisa fulani kanifanyia hivi ndio nimtendee hivi hapana. Mungu aliupenda ulimwengu kisha akamtoa mwanawe wa pekee, sio kwamba tulimfanyia jambo jema kwanza, ndio maana akamtoa hapana, bali alimtoa kwa Pendo lake tu kwetu.

Huu ni upendo usio wa asili ya kibidamu au wanyama, bali asili yake ni mbinguni..Ndio ule unaozungumziwa katika 1Wakorintho 13 unasema..

4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.

Hapa ndipo kilele cha kila kitu.

Sasa tukishaweza kuyafikia hayo yote.. basi Mtume Petro anasema  kwanza tutakuwa si watu wavivu wasio na matunda, pili hatutakuwa watu wa kujikwaa kwaa ovyo katika imani na zaidi ya yote tutakuwa na uwezo wa kuyaona mambo ya mambo yanayokuja.

2Petro 1:8 “Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.

10 Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.

11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo”

Sasa tukishayajua hayo ni wakati wetu sisi sote tujitathimini tupo, katika hatua ipi na kisha, pale tulipozembea au tulipokwama tuanze kupatendea kazi kwa bidii. Tusiwe tu wasomaji wa makala,.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

LIFAHAMU SANA JAMBO HILI, ILI MUNGU AKUTUMIE.

Kitabu kifupi katika biblia ni kipi, na ujumbe wake ni upi?

Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

NA BAADA YA LILE TONGE, SHETANI AKAMWINGIA.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Amina, nime barikiwa jamani 🥹🙏

M
M
2 years ago

Amina ubarikiwe

Lucas mhula
Lucas mhula
2 years ago

Naomba kutumiwa hili somo kwenye WhatsApp yangu🙏🙏

Lucas mhula
Lucas mhula
2 years ago

Amen 🙏🙏🙌