LIFAHAMU SANA JAMBO HILI, ILI MUNGU AKUTUMIE.

LIFAHAMU SANA JAMBO HILI, ILI MUNGU AKUTUMIE.

Tunapaswa tujue daraja kubwa sana la Mungu kututumia sisi kwa ajili ya kazi zake maalumu, ni kuishi maisha ya uchaji wa Mungu ambao  utashuhudiwa na watu wa nje. Kiasi kwamba hata Mungu akipitisha neno lake kinywani mwako, watu wengi wataamini moja kwa moja kwasababu maisha yako tayari yalishawashuhudia hata hapo kabla.

Tukiweza kufikia hapo, basi tujue Mungu atatufunulia mambo mengi sana, kwa ajili ya ufalme wake. Kwamfano katika biblia tunamsoma mtu mmoja anayeitwa Anania, Mtu huyu alitumwa na Mungu ili amfuate Paulo, amwombee, na ambatize. Unaweza ukajiuliza kwani hapakuwa na wakristo wengine pale karibu na ile nyumba ambayo Paulo alikuwepo, mpaka Mungu amtoe Anania mbali kidogo, aje pale?. Jibu ni kuwa walikuwepo, lakini Mungu alijua ili ushuhuda wa mtume Paulo baadaye uwe na nguvu katikati ya watu atakaowasimulia ilimuhitaji mtu, aliyejulikana kweli na watu wengi ni mcha Mungu na  mwaminifu, na ndio maana akampelekea huyu Anania..

Tusome kidogo..

Matendo 9:10 “Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana.

11 Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba;

12 naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena.

13 Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu;

14 hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako.

15 Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.

16 Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.

17 Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.

Sasa utajiuliza uaminifu wake, umeandikwa wapi kwenye maandiko? Tukisoma matendo sura ile ya 22, utaona mtume Paulo alipowekwa mbele ya baraza la wayahudi ili kutoa ushuhuda wake, utaona akimtaja mtu huyu kama ni mtu  aliyejulikana na wayahudi wote kwa utauwa wake..Sasa pale mbele kidogo utaona alisema..

Matendo 22:12 “BASI MTU MMOJA, ANANIA, MTAUWA KWA KUIFUATA SHERIA, ALIYESHUHUDIWA WEMA NA WAYAHUDI WOTE WALIOKAA HUKO,

13 Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.

14 Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake.

15 Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.

16 Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake”

Unaona? Kumbe Sifa zetu nzuri kwa Mungu miongoni mwa watu wanaotuzunguka, ni daraja zuri la Mungu kututumia kwa shuhuda zake nzito, lakini kama tutaitwa watumishi, halafu mitaani tuna shuhuda za matukio ya kizinzi, au tutajiita wakristo tuliookoka lakini mitaani tunajulikana kama wasengenyaji, au watukanaji, tunategemea vipi Mungu atutumie? Kama tutakuwa wakristo halafu kazini kwetu tunaiba, Mungu atatutumiaje kama alivyomtumia Danieli?

Kumbuka Danieli alikuwa mwaminifu sana katika kazi yake ya uwaziri mkuu kule Babeli, pamoja na kwamba alikuwa katika shughuli za kidunia lakini Mungu alimtumia, kutufikishia sisi maono makubwa ambayo mpaka sasa hivi yanatusaidia. Hiyo yote ni kwasababu alishuhudiwa na watu wote, ni mtu anayemcha Mungu. Nasi pia Kama tutaitwa wakristo halafu mitaani tunaonakena tumevaa nguo zisizo na heshima, watu watatuheshimuje?

Kumbuka sisi ni barua tunayosomwa na watu wote, biblia ndio inatuambia hivyo 2Wakorintho 3:2. Kama watu hawatatuheshimu, basi tujue kuwa Mungu ndio Zaidi.

Hivyo ni wajibu wetu, tubadilike, tuanze kujenga shuhuda zilizo hai, kwa watu wanaotuzunguka, tuweke kando mambo yote yanayotukwamisha. Vikao vya usengenyaji tujiepushe navyo, tabia za kidunia pia tujitenge nazo, Na kwa kufanya hivyo, kidogo kidogo, ndivyo tutakavyomvutia Mungu atutumie kama alivyofanya kwa Anania.

Bwana atusaidie sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

SIRI YA KUFANIKIWA KWA MTUME PAULO.

Tofauti kati ya lijamu na hatamu ni ipi kibiblia?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

YONA: Mlango 1

JE! NI WAPI UTAPOKEA HISIA ZA KWELI ZA KI-MUNGU?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucas mhula
Lucas mhula
2 years ago

Amen ashukuriwe Mungu kwa maarifa haya