SWALI: Je Mungu aliumba watu wengine kabla ya Adamu?, maana tunasoma katika Mwanzo 1:27, alimwumba mwanamke na mwanamke, na tena tunaona anaumba tena mtu mwingine (Adamu) katika Mwanzo 2:7.
Jibu: Kitabu cha Mwanzo Mlango wa Kwanza kimezungumzia uumbaji wa Mungu kwa muhtasari (yaani kwa ufupi), lakini tunapokwenda katika Mlango wa pili, ndio tunaona uumbaji ukielezewa kwa urefu zaidi. Kwahiyo mlango wa kwanza ni muhtasari wa uumbaji, ndio maana utaona vitu vinaelezewa kwa ufupi tu…Kwamfano utaona Mungu anasema..
Mwanzo 1:11 “Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo
12 Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema,
13 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.”
Hapo, uumbaji wa miti na mimea umeelezewa kwa kifupi sana, haijaelezwa ilitokeaje tokeaje… sasa ili tujue kwa undani zaidi, hiyo miti ilitokeaje tokeaje, ndipo tunakwenda katika mlango wa 2 wa kitabu hicho hicho cha mwanzo, tunaona ikielezewa vizuri zaidi..
Mwanzo 2:4 “Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi
5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;
6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi”
Unaona?..Kumbe Mungu aliposema nchi itoe majani na mche utoao mbegu, siku ile ile aliinyeshea nchi mvua na ndipo nchi ikazaa miti na mimea kadha wa kadha… Maana yake hakusema tu itokee halafu ikatokea kama tulivyosoma hapo katika hiyo Mwanzo 1:11, bali kulikuwa na hatua (process). Ambazo ndizo tulizokuja kuzisoma katika hiyo Mwanzo mlango wa pili.
Kadhalika Mungu aliposema katika Mwanzo 1:27 kwamba… “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”.
Tunaona hapo uumbaji wa mtu umeelezwa kwa ufupi tu, haijaeleza ni jinsi gani huyo mtu alivyoumbwa, mwanaume na mwanamke walitokeaje tokeaji …je! Wote waliumbwa pamoja?..na je waliumbwa kwa malighafi gani?. Sasa majibu ya maswali hayo ndio tunayapata katika Mlango wa pili wa kitabu hicho hicho.. tusome,
Mwanzo 2:4 “Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi
5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;
6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi.
7 BWANA MUNGU AKAMFANYA MTU KWA MAVUMBI YA ARDHI, AKAMPULIZIA PUANI PUMZI YA UHAI; MTU AKAWA NAFSI HAI.
8 Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya”.
Umeona hapo, biblia inasema Bwana Mungu akamfanya mtu kutoka kwenye mavumbi ya ardhi, jambo ambalo halikutajwa katika ile Mwanzo 1:27, na ukiendelea kusoma katika Mwanzo 2:18-24, utaona jinsi uumbaji wa mwanamke ulivyokuwa, kwamba alitwaliwa kutoka kwa mwanaume (ubavuni mwa mwanaume), jambo ambalo halikuelezwa katika ile Mwanzo 1:27.
Kwahiyo kitabu cha Mwanzo mlango wa kwanza ni muhtasari tu wa uumbaji, umeelezea kwa ufupi sana, na mlango wa pili ndio umeelezea kwa undani kidogo. Ni sawa na unaposoma kitabu Fulani labda cha jeografia, unapokifungua mwanzo kabisa utakutana na “yaliyomo”/“table of content”. Lengo la lile ni kukupa muhtasari na kukuongoza utakachokwenda kukisoma.. Na utaona kila kichwa kimeelezea kwa ufupi sana, lakini utakapokwenda katika kurasa zenyewe utaona mada zimeelezewa kwa urefu sana. Ndicho kilichopo katika kitabu cha Mwanzo mlango wa Kwanza..na wa pili..
Hivyo si kweli kwamba kuna watu wengine waliumbwa kabla ya Adamu. Adamu na Hawa ndio wanadamu wa kwanza kuumbwa.. Na walipoasi waliondolewa katika ile bustani ya Mungu Edeni, na kuanzia huo wakati, wote tunaozaliwa tunakuwa tunalibeba anguko lake. Mpaka tutakapozaliwa mara ya pili katika uzao wa Adamu wa pili Yesu Kristo, ambaye yeye hakutenda dhambi hata mara moja, ambaye alijaribiwa kama Adamu lakini hakutenda dhambi, huyo pekee ndiye amewekwa kuwa ukombozi kwetu.
Kila amwaminiye maandiko yanasema atapata ondoleo la dhambi zake, naye atakuwa haishi chini ya laana bali chini ya Baraka, lakini wote wasiomwamini hawatapata ondoleo la dhambi zao, na siku ya mwisho watatupwa katika ziwa lile la moto, aliloandaliwa shetani na malaika zake.
Je wewe ni mmoja wa waliomwamini au ambao hawajamwamini?.. Kama bado tambua kuwa upo chini ya laana ya anguko la Adamu, na hakuna namna yoyote unaweza kuhesabiwa haki bila kumpokea Yesu maishani mwako, haijalishi utafanya mangapi mazuri, kama humtaki Yesu hutamwona Mungu, kwasababu yeye ndiye Njia ya kufika mbinguni, wala hakuna mwingine.
Hivyo mpokee leo kwa kutubu dhambi zako zote, na kwa kudhamiria kuziacha kabisa na baada ya toba yako hiyo, nenda katafute ubatizo sahihi, kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kwa kukamilisha hatua hizo tatu, yaani Imani, ubatizo na kupokea Ujazo wa Roho Mtakatifu, utakuwa umeukamilisha wokovu wako na Roho Mtakatifu atakuongoza katika kuijua kweli yote na kukupa nguvu za kuishinda dhambi.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Rudi nyumbani
About the author