Nini maana ya usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka!.(Kumbukumbu 25:4)

Nini maana ya usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka!.(Kumbukumbu 25:4)

Jibu: Neno kupura maana yake ni “kutenganisha mbegu ya nafaka kutoka katika suke lake”. Kwamfano tunapozitoa punje za ngano, au mchele kutoka katika masuke yake, hapo tunakuwa tumezipura hizo nafaka, tunapotoa maharage kutoka katika yale maganda yake, hapo tumepura maharage.

Sasa zipo njia nyingi za namna ya kupura nafaka,  zamani njia maarufu  zilizokuwa  zinatumika ni aidha kutumia watu au wanyama. Lakini katika zama zetu hizi, zipo mashine za kufanya hivyo.

Kwahiyo njia hiyo ya kwanza ya kutumia watu, ni pale watu wanapoyatwaa masuke makavu na kuyatwanga au kuyachapa na kitu mfano wa fimbo nzito, njia hii ilikuwa ni ya kuchosha kidogo kwasababu ilihitaji nguvu na watu, na ilikuwa inachukua muda mrefu. Lakini pia ilikuwepo njia ya wanyama, ambapo mnyama kama ng’ombe analazimishwa kupita juu ya  masuke ya nafaka hizo kavu, na anapozikanyaga, zile mbegu zinatengana na masuke yake. Hivyo njia hii ilikuwa ni rahisi, kwasababu ilikuwa haitumii nguvu, na ilikuwa ni ya muda mfupi!. Ni sawa na kilimo cha mkono na kile cha kutumia ng’ombe. Kile cha ng’ombe ni rahisi Zaidi kuliko cha mkono.

Sasa wakati wa kupura kulikuwa na tabia ya watu kuwafunga ng’ombe midomo wakati wa kuzipura nafaka!, ili wasizile zile nafaka. Kwahiyo mtu yupo tayari kumfanyisha ng’ombe kazi ya kupura tani kadhaa za nafaka, lakini hataki hata aonje katika kile kidogo, wakati anazipura. Sasa kwa tabia hiyo ndipo Mungu akawapa amri wana wa Israeli kwamba wakati wa kupura nafaka wasiwafunge ng’ombe vinywa, maana yake wawaache na wenyewe wale katika hizo nafaka zinazopurwa.

Kumbukumbu 25: 4 “Ng’ombe apurapo nafaka usimfunge kinywa”.

Sasa kwanini Mungu aliitoa hiyo sheria?. Ni kwasababu ng’ombe hata iweje hawezi kumaliza tani nzima ya nafaka, atakula kidogo tu atashiba!, hiyo nyingine ataacha, hivyo haiwezi kuleta athari yoyote wala hasara yoyote kwa mzigo ule wote wa nafaka. Kwasababu mpaka umeamua kutumia ng’ombe kupuria na si mkono wako, maana yake mzigo wa nafaka ulio nao ni mwingi. Kwahiyo kumnyima ng’ombe chakula kidogo tu katika hicho, ambacho ni anakila tu hapo hapo, na wala hakipeleki ghalani, ni kukosa utu na huruma.

Mithali 12:10 “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili”.

Sasa ufunuo wa mstari huo ni nini?..Mtume Paulo kwa uweza wa Roho alitoa ufafanuzi

Tusome, 1Wakorintho 9:9, (zingatia vipengele vilivyoainishwa kwa herufi kubwa)

1Wakorintho 9:9 “Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, USIMFUNGE KINYWA NG’OMBE APURAPO NAFAKA. JE! HAPO MUNGU AANGALIA MAMBO YA NG’OMBE?

10 Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake.

11 IKIWA SISI TULIWAPANDIA NINYI VITU VYA ROHONI, JE! NI NENO KUBWA TUKIVUNA VITU VYENU VYA MWILINI?

12 Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo.

13 HAMJUI YA KUWA WALE WAZIFANYAO KAZI ZA HEKALUNI HULA KATIKA VITU VYA HEKALU, NA WALE WAIHUDUMIAO MADHABAHU HUWA NA FUNGU LAO KATIKA VITU VYA MADHABAHU?

14 NA BWANA VIVYO HIVYO AMEAMURU KWAMBA WALE WAIHUBIRIO INJILI WAPATE RIZIKI KWA HIYO INJILI”.

Katika mfano huo, ng’ombe kafananishwa na Mtumishi yeyote wa kweli wa Mungu, au anaweza kuwakilisha kanisa la Kristo, maana yake ni kwamba kama kuna sehemu unanufaika kiroho aidha kanisani au kupitia mtumishi wa Mungu, kwamba kupitia yeye au hilo kanisa, pamechangia pakubwa sana kupata mafanikio yako ya kiroho na kimwili, hupaswi kuzuia chochote katika vile Mungu alivyokubariki, yaani kumbariki yule mtumishi au lile kanisa, au ile huduma. KWASABABU HATAKULA CHOTE!, ni kidogo tu.. Ng’ombe anapokusaidia kupura tani zako za nafaka, anachotaka kutoka kwako kama ujira wake, ni kile chakula cha siku tu!..wala hahitaji ghala lako zima, utakuwa usiye na utu kama utamnyima hata hicho!!. Kwasababu hicho ndicho kitakachompa nguvu ya yeye kuendelea kukusaidia kuzipura hizo nafaka.

Kadhalika utakuwa ni mtu wa ajabu sana, kama utakuwa unanufaika na Baraka za kimbinguni kupitia watumishi wa Mungu, halafu hujigusi hata kidogo!!!.. Ni biblia ndio inasema hivyo, kwamba  hao wahubirio injili, wapate riziki kupitia hiyo. Lakini kama utaona ni sawa wewe kunufaika kiroho lakini si sawa kuchangia chochote!.. Hapo unajipunguzia thawabu zako tu! Za rohoni na mwilini. Biblia inasema wewe ni mkatili! Na mwovu! (Mithali 12:10).

Ametumia mfano mrahisi tu! Wa ng’ombe apurapo nafaka!… ili tuweze kuelewa ni jinsi gani ilivyo ni jambo la kikatili, kuzuilia fedha yako au chochote Mungu anachokubariki,  katika kuipeleka kazi ya Mungu mbele, na ilihali unanufaika na hicho kitu kwa asilimia kubwa.

Unaweza kusoma tena juu ya jambo hilo hilo katika 1Timotheo 5:18.

Je! Wewe ni miongoni mwa wanaowafumba vinywa ng’ombe zao wapurapo nafaka?..wewe ni mmoja wao wa watu wakatili na waovu??. Kama ni mmoja wao basi tubu!..kwasababu ulikuwa unafanya dhambi, na anza kuwa mwenye huruma, na mtu unayejali. Mtolee Mungu kwa moyo pasipo kulazimishwa, kwasababu pumzi unayovuta hulipii chochote, uzima ulionao anakupa bure!, injili unayoipata kila siku hautozwi chochote, sasa kwanini na wewe usijali pasipo kuambiwa, wala kulazimishwa.

Bwana akubariki.

Kumbuka Kristo anarudi, na dalili zote zimeshatimia, hivyo kama hujampokea Yesu, ni vizuri ukafanya hivyo leo na wala si kesho!.

Luka 12:35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara”

Maran atha!.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho


Mada Nyinginezo:

NGUVU YA SADAKA.

MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Chamchela ni nini kwenye biblia?(Zaburi 58:9, Amosi 1:14)

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments