Dhambi inafananishwa na mnyama mkali sana wa porini, kama vile simba au chui, au chatu. Utagundua tabia moja waliyonayo hawa wanyama pale wanapowinda ni kuwa hawana papara, Wanakuwa wavumilivu sana mbele ya kitoweo chao, hawakurupuki ovyo kwa kuanza kukikimbiza kutokea mbali, hapana, bali utaona wanajisogoza karibu navyo, taratibu na kwa upole sana, na kwa kuvizia,kana kwamba hawana habari navyo, kiasi kwamba yule anayewindwa, hawezi kugundua chochote.. Hadi pale anapokaribiwa sana, na kurukiwa, au kikimbizwa kwa ghafla ndipo anapogundua haa, kumbe adui yangu alikuwa karibu sana na mimi. Akiwa anajiandaa kukimbia tayari ameshakamatwa..
Na ndivyo ilivyo dhambi tabia yake, haina papara.. Wakati ule kabla Kaini hajamuua ndugu yake Habili, kuna maneno ambayo Mungu alimwambia, embu tusome..
Mwanzo 4:3 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana.
4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;
5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.
6 Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? USIPOTENDA VYEMA DHAMBI IKO, INAKUOTEA MLANGONI, NAYO INAKUTAMANI WEWE, WALAKINI YAPASA UISHINDE,
8 Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.”.
Unaona? Kumbe dhambi ilikuwa imeshamsogelea sana Kaini mlangoni kama chui, lakini yeye hakuiona, ilikuwa inasubiria tu afungue mlango Fulani katika maisha yake, kisha yenyewe imrukie kwa ghafla, na habari yake iwe imekwisha. Hivyo Mungu akamtahadharisha mapema lakini yeye hakusikia, Na kama tunavyosoma biblia, Kaini hakutubu na kugeuka kuachana na mahasira zake na wivu, badala yake, siku moja akamwambia ndugu yake twenda huko maporini, walipofika kule, alishangaa nguvu ya ajabu ya kuua imemwingia ndani yake kwa ghafla, na moja kwa moja, akachukua kisu akamchinja ndugu yake bila hata huruma.
Jiulize swali ni nani alimfundisha Kaini kuua?, hakuna aliyemfundisha bali ni ile dhambi iliyomnasa ndio ilitekeleza hayo yote. Unapoona mauaji ya kikatili yanatekelezwa na watu usidhani kuwa ni akili zao ziliwatuma hivyo,.Unapoona Yuda anakwenda kumsaliti Bwana wake, tena kwa kumbusu macho makavu, usidhani mwanadamu wa kawaida anaweza kufanya kitendo kama kile hapana, bali dhambi ikishakaba koo, huwezi kunasuka tena, ni sharti utimize mapenzi yake.
Ndugu yangu, leo hii, tabia ya dhambi bado ni ile ile.. Unapohubiriwa utubu dhambi, sio kwa faida ya mchungaji wako, au mwalimu wako, ni kwa faida yako mwenyewe. Kwasababu mimi na wewe sasa hivi tunawindwa vikali sana,..Na kama tutafungua milango yetu kuruhusu kila aina ya dhambi ituchezee tu, tufahamu kuwa mwisho wetu upo mlangoni.
Dhambi ina shinikizo kubwa sana, ikishafanikiwa kukuvaa kama Kaini, au Yuda, ujue hutoki tena, hutajali kifo, hutajali chochote. Kama unaendelea kutoka nje ya ndoa yako, kumbuka upo hatarini kufa, kama unazini zini ovyo, ujue dhambi imeshakuandalia mauti yako. Hatujui itakuwa ni kwa njia ya ukimwi, au kifo, au mapepo, lakini safari yako ipo ukingoni.
Hatupaswi kumwogopa shetani hata kidogo, lakini tunapaswa tuiogope dhambi kweli kweli. Kwasababu yeye ndio yule mnyama atuwindaye. Shetani kazi yake ni kututengenezea mazingira ya sisi kunaswa na dhambi, lakini yeye hana nguvu yoyote ya kukushinda.
Hivyo, tuwe makini, kama hujatubu, ni heri ukatubu sasa, na sio kesho. Hakuna wokovu wa kesho au ule wa “siku moja nitaokoka”. Wokovu wa namna hiyo haupo, wala hautakaa uje milele. Tubu mpendwa ukabatizwe, ukaoshwe dhambi zako, upokee na Roho Mtakatifu, hizi si zama za kutanga tanga na huu ulimwengu wa dhambi, mitandao inawaharibu watu wengi sana. Yesu alituambia, tumkumbuke mke wa Lutu. Tukitaka kuziponya nafsi zetu tutaziangamiza, na tukiziangamiza kwa ajili yake tutaziponya.
Acha mambo ya dunia yakupite, acha fashion zikupitie, acha anasa zikupite, ipoteze nafsi yako kwa Mungu, lakini mwisho wa siku utapona, kuliko kuupata ulimwengu mzima halafu baadaye unakwenda kuzimu milele itakusaidia nini?. Dhambi ni mnyama katili sana.
Bwana atusaidie sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine:
Mada Nyinginezo:
SI KWA UWEZA WALA KWA NGUVU BALI KWA ROHO YANGU, ASEMA BWANA.
NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.
Je aliyezungumza na Musa kule jangwani ni Mungu mwenyewe au malaika wake?
Je aliyezungumza na Musa kule jangwani ni Mungu mwenyewe au malaika wake?
UTAKUWA MTORO NA MTU ASIYE NA KIKAO DUNIANI.
HUDUMA YA UPATANISHO.
About the author