JE! USIPOTIMIZA NADHIRI ZAKO ZOTE KWA BWANA. HAWEZI KUKUSAMEHE?

JE! USIPOTIMIZA NADHIRI ZAKO ZOTE KWA BWANA. HAWEZI KUKUSAMEHE?

Hili ni swali ambalo linaulizwa na wengi,  hususani watu ambao walimwekea Mungu nadhiri huko nyuma lakini mwisho wa siku wamejikuta hawawezi kuzitoa.

Sasa kabla ya kwenda kuona kama msamaha upo au haupo, Jambo la kwanza unalopaswa kufahamu kuhusu nadhiri ni kwamba lile ni  tendo la hiyari ambalo mtu anamwekea Mungu mwenyewe, na hapo ndipo Mungu anataka umakini sana kwasababu hakumlazimisha kufanya hivyo.

Biblia inasema ni heri, usiweke kabisa nadhiri kuliko kuiweka, halafu ukashindwa kuitoa,

Mhubiri 5: 4 “Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.

5 Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe”.

Unaona hapo? Mungu anasema yeye hawi radhi na wapumbavu. Ikiwa na maana kuwa nadhiri ambayo haitolewi kwa wakati, Ni haki ya Mungu kumwadhibu huyo mtu kwa jinsi atakavyo yeye.

Kwahiyo kabla hujatamka nadhiri yoyote kwa kinywa chako mbele za Mungu, hakikisha kwanza unaelewa unachokitamka, na una uwezo wa kukisimamia.Biblia inasema..

Mithali 20: 25 “Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari”.

Sasa tukirudi kwenye kiini cha somo, Je! Kutotimiza nadhiri zako, Mungu hawezi kukusamehe?

Tukumbuke katika biblia ni dhambi moja tu isiyosameheka kwa Mungu, na dhambi yenyewe ni “Kumkufuru Roho Mtakatifu”  Lakini hiyo haimaanishi kuwa adhabu za dhambi nyingine hazipo hapana.. Kuna dhambi ambazo Mungu atakusamehe bila adhabu, lakini pia zipo dhambi ambapo Mungu atakusamehe pamoja na adhabu. Kwa urefu wa somo hilo fungua hii link>>>>>> https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/dhambi-ya-mauti/

Sasa ikiwa mtu hajamtimizia Mungu nadhiri zake, anaweza akatubu na pengine Mungu akamsamehe kabisa na mbinguni akaenda, lakini adhabu ya kosa lake, bado akaitumikia hapa hapa duniani, adhabu inaweza ikawa pengine hata kifo,n.k.

Lakini bado tukirudi katika biblia tunaona wapo watu ambao walihalifu nadhiri zao, lakini hawakuadhibiwa na Mungu, mmojawapo ni Daudi wakati ule anataka kwenda kumuua Nabali, aliapa kwa Mungu kwamba kama hatamuua Nabali na nyumba yake yote, basi Mungu amfanyie yeye hivyo . Lakini tunaona hakumuua Nabali alipofika katika nyumba ile, na Mungu vilevile hakumuua Daudi na nyumba yake kwa kutotimiza nadhiri zake. Hizo ndizo zinazojulikana kama nadhiri wa wapumbavu.

1Samweli 25: 22 “Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi”.

Sehemu nyingine, utaona ni wakati Sauli anapigana na wafilisti naye pia aliweka nadhiri kuwa mtu yeyote asionje chochote mpaka atakapomaliza kupigana na wafilisti na kuwashinda, atakayeonja atauawa lakini mwanae Yonathani, hakusikia agizo hilo, yeye akala, na Sauli alipopata taarifa akataka kumwangamiza, lakini Israeli wakamzuia, kwasababu yeye ndiye aliyeleta wokovu katika taifa. Na baada ya hapo hatuoni kama Mungu alimwangamiza Sauli kwa kuhalifu agizo lile.(Soma 1Samweli 14)

Lakini tunaona pia kulikuwa na mwamuzi mwingine aliyeitwa Yeftha, yeye alimwekea Mungu nadhiri kuwa atakaporudi kutoka vitani na ushindi, basi chochote kitakachotokea cha kwanza mbele yake, atamtolea Mungu kama sadaka ya kuteketezwa. Hakufikiria kwamba anaweza kutokea mtu mbele yake..

Lakini kweli Mungu alipomfanikisha katika vita, kitu cha kwanza kutokea mbele yake, hakikuwa ng’ombe, au mbuzi, bali binti yake wa pekee. Hivyo ikambidi aende kumchinja mwanawe na kumtoa kafara kwa Mungu, japo ambalo ni kinyume kabisa na maagizo ya Mungu, na ni machukizo. Yeftha Alikuwa na uwezo wa kuizuia nadhiri yake ya kipumbavu, kama alivyofanya Daudi au Sauli, lakini alitimiza nadhiri isiyokuwa na maana yoyote mbele za Mungu.

Hivyo, Mungu anaweza akaadhibu au asiadhibu, yote yapo katika uwezo wake mwenyewe..

Lakini katika yote, Mungu tangu zamani kwa hekima yake alishaona kuwa wapo watu wake, ambao watakuja kutamka nadhiri zao bila hata ya kufikiria, na ili kuwaepusha na adhabu, akampa maagizo Musa, juu ya nadhiri za wapumbavu kama hizo akasema..

Walawi 5:4 “au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo;

5 kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa;

6 naye atamletea Bwana sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake”.

Umeona?, Mtu kama huyo ambaye alitamka tu maneno bila kufikiri hatma yake itakuwaje mbeleni, pengine mwingine alisema mimi sitaoa au kuolewa maisha yangu yote, bila kupiga gharama zake. Mungu alimwambia Musa, mtu huyo atubu, kisha sio kutubu tu, bali aambatanishe na sadaka yake ya makosa kama vile atakavyoelekezwa na kuhani.

Hii ikiwa na maana, hata sasa wapo watu waliotamka nadhiri zako mbele za Mungu, lakini sasa wameshindwa kuzitoa, jambo la kwanza wanalopaswa kulifanya  hapo ni kutubu kwa kumaanisha kabisa, sio kutubu kwa dakika mbili au tatu, hapana ni kulia kwa kumaanisha mbele za Mungu kwa kipindi fulani (ukikumbuka kuwa Mungu hawi radhi na wapumbavu, anaweza kukuondoa duniani kwa kosa hilo tu)..Kisha baadaye ukishamaliza maombi yako ya toba ya muda mrefu, andaa sehemu nono ya ulichonacho nacho (yaani sadaka), kisha kipeleke madhabahuni pa Mungu kwa ishara ya unyenyekevu kwa hofu nyingi.

Na baada ya hapo Mungu atakusamehe.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Suleiman mwahesa
Suleiman mwahesa
2 years ago

Nashukuru Mungu kwa watu wake mnao post masomo kwa ajiri yetu, Mungu awabariki