MAUTI NA UZIMA HUWA KATIKA UWEZO WA ULIMI.

MAUTI NA UZIMA HUWA KATIKA UWEZO WA ULIMI.

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu lililo hai (Zab.119:105)

Je unaijua nguvu ya kinywa chako? Biblia inasema kuwa MAUTI na UZIMA huwa katika uwezo wa ULIMI. Na mtu awezaye kuutumia vizuri ulimi wake atakula matunda yake.

Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”.

Sasa ULIMI una matunda mawili tu!, ambayo ni “Uzima na Mauti”. Maana yake mtu anaweza kuutumia ulimi wake ukamletea UZIMA, lakini pia anaweza kuutumia na ukamletea MAUTI.

Yule kijana aliyempelekea Daudi habari za kifo cha Sauli, kinywa chake mwenyewe kilimletea “Mauti” (2Samweli 1:16) hali kadhalika Mfalme Yehoshafati alipokuwa katika hatari ya kufa, kwa kinywa chake mwenyewe alijiokoa. (2Nyakati 18:31).

Lakini leo nataka tuangalie faida za kutumia ULIMI katika eneo la  MAOMBI.

Wengi tumezoea kuomba kimoyomoyo, jambo ambalo ni zuri lakini si wakati wote linafaa!!.. kuna mazingira ni lazima utumie kinywa chako kutoa maneno dhahiri yanayosikika!..Kuna ngome zinahitaji kusikia sauti ndipo zitii!, Kuna ngome zinahitaji kuamrishwa na kukemewa ndipo zitii (Kuta za Yeriko zilihitaji kelele nyingi ili zianguke)….Hali kadhalika katika imani inahitajika sauti ya kinywa ili kuthibitisha wokovu mtu alioupata…

Warumi 10:9  “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

10  Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.

Kwa hiyo si kila wakati maombi ya ukimya yanafaa… Ni lazima ujifunze kubadili gear unapoingia katika maombi ya vita, hata motokaa haisafiri kwa gear moja tu, ikienda hivyo itakwamaa mahali Fulani.

Sasa biblia inatufundisha kuwa “Mauti na Uzima” huwa katika uwezo wa kinywa. Maana yake ni kwamba tukitumia vizuri ndimi zetu wakati wa kuomba tunauwezo wa kuvihuisha vitu vingi vilivyokufa, na pia kuviua baadhi ya vitu visivyofaa maishani mwetu.

Tunaviuaje vitu visivyofaa?.. Tunaviua kwa “kuvitamkia kifo” kwa mfano ule ule wa Bwana Yesu alivyoutamkia ule Mtini, na ukafa wakati ule ule.

Mathayo 21:18  “Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa.

19  Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; AKAUAMBIA, YASIPATIKANE MATUNDA KWAKO TANGU LEO HATA MILELE. MTINI UKANYAUKA MARA.

20  Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara?

21  Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka.

22  Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea”.

Mstari wa 19 unasema “..akauambia, yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele, mtini ukanyauka mara.” Hapo Bwana Yesu aliuua huo mtini kwa kutumia kinywa chake. (Aliutumia ulimi wake na akala matunda yake), na anatuambia tukiwa na Imani tunaweza kufanya kama hayo na hata Zaidi ya hayo.

Hivyo na sisi ni lazima tujifunze kutumia Ndimi zetu kuua baadhi ya vitu ambavyo shetani kavipanda katika maisha yetu.

Unapoamka kusali Ua kazi za giza katika siku yako, unapotembea zihukumu kazi za giza kwa kutumia kinywa chako.. kwasababu unapotamka na kuamini moyoni mwako basi fahamu kuwa ni lazima yatokee hayo uliyoyasema.

Zitamkie mauti kazi za shetani katika utumishi wako, katika familia yako, katika watoto wako, katika shughuli zako, katika vitu vyako unavyomiliki, Usiishie tu kuomba kimya kimya pasipo kutoa maneno yoyote.. Paza sauti kwasababu kuna nguvu Mungu kaiweka katika ulimi wa mwanadamu.

Wachawi na mawakala wote washetani wanajua nguvu iliyopo katika ulimi, ndio maana wanautumia kuleta madhara makubwa katika maisha ya watu.. sasa na watu waliookoka ni lazima kutumia ulimi kutangua maneno yote yaliyonenwa au yanayonenwa kinyume na maisha yetu ya kiroho na kimwili.

Vile vile ni lazima tutumie Ndimi zetu kutamka UZIMA wa vitu vilivyokufa katika maisha yetu. Nabii Ezekieli aliambiwa aitabirie mifupa mikavu ili iweze kuwa na uhai tena, na katika maono yale aliitabiria mifupa ile kwa kinywa chake na ikarudia uzima na likaamka jeshi kubwa sana (soma Ezekieli 37:1-8).

Sehemu zote Bwana Yesu alipoenda kuponya wagonjwa alitumia kinywa chake kutamka, na sisi ni lazima tutumie vinywa vyetu kutamka uzima juu ya vitu viliyokufa ndani yetu. Ikiwa ni huduma, ikiwa ni karama, ikiwa ni shughuli unayoifanya, ikiwa ni watoto, au kitu kingine chochote kilicho chema ni sharti kipate uzima kupitia kinywa chako!. Fanya hivyo daima, usiache hata siku moja hata kama unaona kwa nje ni pakavu, endelea kwasababu vita vya kiroho si vita vya kimwili, na ukiwa na bidii kufanya hivyo mwisho utakula matunda ya ulimi wako.

Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?

HIZO NDIZO ROHO ZA MASHETANI.

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

Tofuati kati ya kifo na mauti ni ipi?

Na ulimi laini huvunja mfupa.(Mithali 25:15)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments