Ni lazima tujue namna mbalimbali za kupambana na adui yetu (Ibilisi). Tunajua yeye ni mpinzani wetu, na mpinzani sikuzote huwa si rahisi kukubali kushindwa kirahisi, ni lazima ataleta ukinzani. Na ndio hapo suala la Kukemea linakuja wala hatumbembelezi wala hatumsihi-sihi, bali tunamkemea.
Kukemea maana yake ni kukipinga/ kukifukuza kitu kwa nguvu, kwa mamlaka uliyonayo.
Tunaona sehemu nyingi Yesu akimkemea ibilisi Pamoja na mapepo yake, ambayo yalikuwa yanawatesa watu.
Mathayo 17:18 “Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile”.
Marko 8:33 Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu
Hivyo na sisi tumepewa mamlaka hiyo, ya kumkemea ibilisi na mapepo yake, na uovu, na magonjwa, na vitu vya asili kwa jina la Yesu na vikatii.
Lakini pia tuna majira si lazima tufanye hivyo, Tutatumia nguvu nyingi sana! Leo tutaona silaha nyingine za Malaika ambayo wanatumia kumshughulikia shetani.. Maandiko yanatuambia wanao uwezo mkuu kuliko sisi lakini hawatumii uwezo wao wakati wote, kufanya hivyo kila wanapokutana na adui yao shetani.
Kwamfano, Wakati Fulani Malaika Mikaeli alipokutana na shetani, wakiushindania mwili wa Musa, maandiko yanasema, hakutumia uwezo wake kumlaumu, bali alisema Bwana na akukemee!.
Yuda 1:9 “Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee”.
Utajiuliza ni kwanini afanye vile? Sio kwasababu alishindwa, lakini alitambua SILAHA kubwa Zaidi itamfutilia mbali adui yake. Kwa namna nyingine Mikaeli alikuwa anamchonganisha shetani kwa Mungu. Na ukikemewa na Mungu unatarajia nini? Kama sio kupotelea mbali kabisa moja kwa moja.
Hivyo shetani anaiogopa vita ya Mungu Zaidi ya ile ya malaika au wanadamu.
Utaona tena jambo kama hili hili alilitenda Malaika mwingine, wakati ule wa Yoshua kuhani mkuu alipokuwa amesimama mbele za Bwana kuomba, na shetani naye amesimama kumpinga. Yule Malaika alimwambia shetani “Bwana na akukemee”.
Zekaria 3:1 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. 2 Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?”
Umeona? Hivyo si kila wakati unapopishana na adui yako uso kwa uso, ufikirie kurusha makombora, kuvunja, kuharibu na kubomoa ngome, ndio yapo majira utasimama kuomba hivyo lakini pia tulia kwasababu maandiko yanasema VITA NI VYA BWANA. Mkabidhi Bwana yote. Kwamfano shetani amekuletea majaribu ya magonjwa sugu. Mwambie Bwana yaone mateso yangu, UMKEMEE SHETANI. Arudi nyuma yangu.
Sasa Maombi kama haya, usiyaombe juu juu tu,Fahamu kanuni, Ni maombi ya kumwita Mungu aingilie tatizo hilo, amwone mtesi wako, Ili pale anapopatumia kama mlango wa kukusumbua AMKEMEE atoke. Tatizo Lililokutesa kwa muda mrefu Bwana alifutilie mbali, kwa kulikemea.
Ni maombi aliyoyafanya Esta. Alipoona adui yake Hamani, amepanga vita dhidi yake na uzao wake na ndugu zake wauawe. Hakuhangaika, kushindana na Hamani adui yake. Aliona mambo yatakuwa mengi na kuumizana kichwa. Bali alikwenda moja kwa moja kwa mfalme. Akajinyenyekeza mbele zake, akamfanyia karamu kubwa sana, tena akamwomba katika karamu hiyo aje na yule adui yake, washiriki pamoja. ndipo mfalme akamuuliza haja yako ni nini, Lakini tunaona Esta bado hakumwambia tatizo lake kwa haraka,, akamfanyia tena na mara ya pili mfalme na adui yake karamu iliyo kubwa kama ile ya kwanza, akawaalika.. Ndipo Mfalme akamuuliza tena Esta haja yako ni nini?. Ndipo Esta sasa akaeleza akasema, ni HUYU ADUI YANGU HAMANI, amepanga kuniua mimi.
Akamwachia mfalme hukumu yote. Saa ileile Hamani akaenda kutundikwa msalabani, yeye na nyumba yake yote ikauliwa. Na Habari yake ikawa imeisha pale hadi hivi leo. Wala Esta hakuita kikosi, wala hakuchukua upanga, wala hakumwambia mfame muue, mvunje shingo, mchome moto Hamani. Hakusema hayo alichomwomba mfalme ni uhai wake tu (Esta 5).
Na ndivyo Mungu atakavyofanya kwa adui yetu Ibilisi na mapepo yake, pale ambapo tutataka Bwana ashughulike na matatizo yetu, zaidi ya sisi kushughulika nayo kuyakemea. Lakini ni sharti sisi tumkaribie yeye, kwa moyo wa upendo, tumfanyie karamu, ya Kupendeza ndipo tuzikabidhi changamoto zetu kwake.
Hivyo silaha hii ukiitumia vema itakusaidia sana. Jenga ukaribu wako na Mungu, Fanya ibada nyingi, mtolee Bwana sadaka, mwimbie sifa, mtukuze sana, ruka-ruka uweponi mwake, mpendeze moyo wake..( fanya hivi Zaidi ya kurusha makombora, na maombi ya vita) kisha mwishoni ndio mwambie Bwana amkemee adui yako. . Matokeo utayaona makubwa sana, haijalishi tatizo ulilonalo limekusumbua kwa muda mrefu kiasi gani, umepambana nalo kwa muda mrefu kiasi gani, limekuja na kujirudia rudia mara nyingi kiasi gani. Ugonjwa huo hautibiki kwa namna ipi, utakwenda tu.. Safari hii halitarudi kwako tena milele.
Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
Je Malaika Mikaeli ndiye Yesu mwenyewe?
USIRUHUSU INZI WATUE JUU YA ROHO YAKO.
Ni kwa namna gani, upendo husitiri wingi wa dhambi? (1Petro 4:8).
About the author