Bwana YESU KRISTO anatuombeaje kule juu mbinguni? (Warumi 8:34)

Bwana YESU KRISTO anatuombeaje kule juu mbinguni? (Warumi 8:34)

Swali: Maandiko yanasema KRISTO ameketi kutuombea, hata tufanyapo dhambi?


Jibu: Tafadhali soma taratibu na kwa umakini…

Warumi 8:34 “Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; TENA NDIYE ANAYETUOMBEA”.

Ni kweli Neno la Mungu linasema BWANA WETU YESU KRISTO, katika mstari huo na linazidi kututhibitishia tena katika 1Yohana 2:1.

1Yohana 2:1 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi TUNAYE MWOMBEZI KWA BABA, Yesu Kristo mwenye haki”

Lakini ni vizuri kuzijua lugha za kiroho na namna ya kuzitafsiri, vinginevyo itatuwia vigumu sana kuielewa biblia na hata wakati mwingine kujikuta tunaabudu sanamu kwa kushindwa kuzipambanua lugha za kiroho,

Kwamfano kuna mahali Bwana YESU alisema Mtu asipoula mwili wangu, na kuinywa damu yangu hana uzima ndani yake (soma Yohana 6:53), sasa tukiuchukua huo mstari kama ulivyo na kwenda kutafuta mwili wa Bwana kama nyama, na Damu yake kama ilivyo na kuinywa, tutakuwa tumeshindwa kutafsiri vyema lugha ya biblia, na hivyo tutakuwa tumefanana na waganga na wachawi walao nyama na kunywa damu!.

Lakini kama tukiweza kuelewa maana ya mwili wake Bwana Yesu na damu yake kuwa ni ule mkate na kile kikombe, sawasawa na (Mathayo 26:26-27) tutakuwa tumeenda sawasawa na Neno la Mungu.

SASA KWA MSINGI HUU, TUTAKUWA TAYARI KUJIFUNZA NI KWA NAMNA GANI KRISTO ANATUOMBEA KWA BABA.

Katika hiko kitabu cha Warumi mlango wa 8:34 tuliposoma kuwa KRISTO ndiye anayetuombea, hebu turudi mistari kadhaa nyuma mpaka ule mstari wa 26, tuone jambo..

 Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO MWENYEWE HUTUOMBEA KWA kuugua kusikoweza kutamkwa.

27  Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”

Angalia hapa; Katika ule mstari wa 34 tumesoma kuwa ni BWANA YESU ndiye anayetuombea, lakini tena katika mstari wa 26 ndani ya sura hiyo hiyo, tunasoma kuwa ni ROHO MTAKATIFU ndiye anayetuombea.. Sasa swali ni yupi kati ya hawa wawili anayetuombea kwa Baba?… ni Roho Mtakatifu au ni Bwana YESU??.

Sasa jibu la swali hili ni rahisi sana na ndio tunaelekea katika kiini cha mada hii.

Jibu la swali hili tunalipata katika kitabu kile cha 2Wakorintho 3:17, sikiliza Neno la Mungu linavyosema…

2Wakorintho 3:17  “Basi Bwana ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru”.

Hapo anasema lakini “Bwana” (yaani YESU)..ndiye “Roho”(yaani Roho Mtakatifu).. kumbuka hapo Roho imeanza kwa herufi kubwa kuwakilisha Roho Mtakatifu. (Popote pale Roho inapoanza kwa herufi kubwa inamaanisha Roho wa Mungu).

Hivyo kulingana na hayo maandiko, ni sahihi kabisa kusema BWANA YESU ndiye ROHO MTAKATIFU, na Roho mtakatifu ndiye Bwana YESU.. Kwahiyo mahali popote asemapo Roho Mtakatifu ni Bwana YESU ndiye kasema..

Ndio maana utaona katika kile kitabu cha Ufunuo Mlango wa 2 na wa 3 katika jumbe za yale makanisa saba, utaona ujumbe unaanza YESU ANASEMA, na unamaliza ROHO AYAAMBIA MAKANISA, ikiwa na maana kuwa Roho ndiye huyo huyo Bwana.

Vile vile Roho Mtakatifu akiomba ni  Bwana ameomba.

Sasa swali la mwisho ambalo litahitimisha Mada hii, ni je!, Kama Bwana YESU ndiye Roho Mtakatifu, je huyo Roho Mtakatifu anatuombeaje sawasawa na huo mstari wa 26?

Roho Mtakatifu (ambaye ndiye Bwana mwenyewe) hatuombei kama sisi tunavyoombeana!.. La! Yeye anaomba ndani yetu.. Maana yake tuombapo sisi, basi yale maombi yetu anayachukua na kuyapeleka mbele za Baba katika lugha nzuri Zaidi, katika maelezo mazuri Zaidi.

Lakini si kwamba tumelala au tunacheza, au tunafanya mambo yetu mengine basi wakati huo huo yeye kule anatuombea, hapana! Hiyo si tafsiri yake kabia..

Kwa urefu jinsi Roho Mtakatifu anavyotuombea fungua hapa utapata kuelewa vizuri sana >>ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba jinsi Bwana YESU anavyotuombea ni kwajinsi ya Roho Mtakatifu, na Roho Mtakatifu anachukua yale maombi yetu na kuyapeleka kwa Baba kwa lugha kamilifu Zaidi.. Hivyo kamwe usiwaze kuwa Bwana  YESU yupo mbinguni mbele za Baba, akisali kwaajili yetu, bali ni kwa njia ya Roho wake mtakatifu ndani yetu, ndipo anapotuombea.

Kwanini tunajifunza haya?.

Ni kwasababu zipo Imani zilizoanzishwa na ibilisi mwenyewe zisemazo kuwa “hatuna haja ya kuomba, kwasababu Bwana YESU yupo mbinguni anatuombea usiku na mchana”…

Kamwe usidanganyike na hayo mafundisho kwani ni mafundisho ya Adui, ibilisi… Tusipoomba na Roho Mtakatifu hawezi kuomba, na Roho Mtakatifu asipoomba ni Bwana hajaomba.. Lakini tuombapo, Roho Mtakatifu ni kipaza sauti chetu kwa Baba..kwahiyo maombi ni lazima… (Pitia tafadhali somo la jinsi Roho Mtakatifu anavyotuombea).

Na mwisho kabisa, hakuna mtakatifu yoyote aliyekufa au aliyenyakuliwa anayetuombea… NI YESU TU PEKE YAKE, kwa NJIA YA ROHO WAKE MTAKATIFU, ndiye anayetuombea.. Hivyo Mtakatifu Mariamu, hawezi kutuombea, wala Eliya, wala Musa, wala Henoko, wala mtu mwingine yoyote aliye hai wala aliyekufa…(Hawana na hatuna hivyo vigezo).

Kwahiyo lililo kubwa na la msingi sana, ni kutafuta Roho Mtakatifu kwasababu kwa kupitia huyo ndio maombi yetu yatafika na kukubaliwa, na tena mtu asiyekuwa na Roho Mtakatifu huyo si wake kulingana na biblia (Warumi 8:9)

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je! sheria ilikuwaje dhaifu kwasababu ya mwili? (Warumi 8:3)

NJIA/BARABARA YA WOKOVU NDANI YA KITABU CHA WARUMI.

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

Je Kauli ya Mungu katika Warumi 11:4 na 1Wafalme 19:18 inajichanganya?.

Roho Mtakatifu ni nani?.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments