Jina la Bwana wetu Yesu, libarikiwe karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, ambalo ndio mwanga wa njia zetu na taa iongozayo miguu yetu. Leo tutajifunza vipindi VINNE ambavyo ni vigumu mtu kumkumbuka muumba wake.
Biblia inasema..
Mhubiri 12: 1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, KABLA HAZIJAJA SIKU ZILIZO MBAYA, WALA HAIJAKARIBIA MIAKA UTAKAPOSEMA, MIMI SINA FURAHA KATIKA HIYO.
2 KABLA JUA, NA NURU, NA MWEZI, NA NYOTA, HAVIJATIWA GIZA; KABLA YA KURUDI MAWINGU BAADA YA MVUA; ……
6 KABLA HAIJAKATIKA KAMBA YA FEDHA; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani”
7 NAYO MAVUMBI KUIRUDIA NCHI KAMA YALIVYOKUWA, NAYO ROHO KUMRUDIA MUNGU ALIYEITOA”
Biblia inaposema mkumbuke muumba wako “KABLA”. Maana yake ni kwamba kama hutamkumbuka katika hicho kipindi, basi utafika wakati itakuwa ni ngumu wewe kumkumbuka Muumba wako. Ikimaanisha kuwa kitendo cha mtu kumkumbuka Mungu, ni neema, na huwa hakidumu muda wote!, ni cha kitambo tu!..tofauti na wengi wanavyofikiri kuwa watakapofikia miaka fulani watamkumbuka Mungu, pasipo kujua kuwa nguvu ya mtu kuvutwa kwa Mungu inatoka kwa Mungu, na si kama mtu apendavyo yeye..
Yohana 6: 44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka;..”.
Ndio maana leo hii kuna idadi kubwa ya vijana na watoto wanaompokea Yesu, kuliko wazee!.
Sasa kufuatia hiyo mistari katika kitabu hicho cha Mhubiri, biblia imetupa vipindi 6 ambavyo tunapaswa tufanye maamuzi, maana yake ndani ya hivyo vipindi, tunatakiwa tuwe tumeshafanya maamuzi thabiti ya kumkumbuka muumba wetu na kumtumikia.
Mhubiri 12: 1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.
Nyakati za utoto na ujana, ni nyakati ambazo mtu anapokosa furaha, ni rahisi kumrudia Mungu, mtu anapopitia matatizo Fulani ndipo anapomkumbuka Mungu, kwasababu bado yupo katika miaka ya ujana, lakini sivyo atakavyokuwa mzee. Miaka ya uzee ni miaka ambayo mtu anapopitia matatizo au shida ndivyo anavyozidi kukaa mbali na Mungu. Ndio maana ni ngumu sana kumbadilisha mzee ampokee Yesu, hata akiwa katikati ya mateso na tabu!.. kwanini?..Ni kwasababu ile nguvu ya kumfanya amrudie muumba wako inakuwa haipo!.. Na mara nyingi ni kwasababu muda wa ujana, hakuutumia kumkumbuka muumba wake.
Lakini pia hapa biblia inatuonya kwamba tumkumbuke muumba kabla haijakaribia hiyo miaka!..sio haijafika!.. bali haijakaribia!!..maana yake hata kabla ya kuifikia hiyo miaka, bado kuna shughuli kumkumbuka Mungu..ikiwa na maana kuwa hii neema ya sisi kuvutwa kwa Mungu, haidumu juu yetu milele, inawahi kuondoka kabla hata ya sisi kufikia uzee. Ni wazee wachache sana, wanaopata neema ya kumpokea Yesu katika miaka ya uzee.. Na wengi wa hao ni kwasababu labda katika ujana, waliishi katika mazingira ambayo hawakufikiwa na injili sana.. Lakini wengi ambao wapo tangu ujana wao wanaisikia injili, lakini wanaipuuzia, katika uzee ni ngumu pia kumrudia Mungu.
Mhubiri 12:2 “Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua”
Kipindi ambacho Jua litatiwa giza kwa mtu, ni kipindi cha uzee.. Ni kipindi ambacho Mwili wako umeisha nguvu, macho yako hayana nguvu, miguu yako haina nguvu, mikono yako haina nguvu..
Bwana Yesu alimwambia Petro maneno haya..
Yohana 21:18 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka”
Kipindi hichi ni kipindi ambacho ni ngumu kumkumbuka muumba wako!.. ile kiu, hamu, au motisha ya kumtafuta Mungu inakuwa haipo, kadhalika uwezo wa kutafakari mambo ya Mungu unakuwa ni hafifu!.. kwahiyo Mungu anatupa tahadhari kuwa tumkumbuke yeye kabla hiyo miaka haijakaribia!..kwasababu itakapofika tofauti na tunavyofikiri kwamba tutakuwa na nguvu za kumkumbuka Mungu, kumbe la! Kinyume chake ndio tutakwenda mbali naye..
Na kipindi ambacho mawingu yatarudi baada ya mvua, ni kipindi hicho hicho ambacho, mvua ya neema imeisha juu ya mtu..hivyo mawingu yanarudi kama kawaida na kiangazi kinaanza.
Mhubiri 12:6 “kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani”
Kikawaida umri wa kukatika kamba ya fedha ni miaka 60, huo ndio umri wa kustaafu!…wengine wanastaafu kabla ya huo umri miaka 55, na wengine baada ya huo kidogo, miaka 65 na hapo anasema kukatika kamba ya fedha, na si kukatika fedha!..kamba ya fedha ni shughuli unayoifanya inayokuingizia kipato Fulani cha kila mwezi.. wengi!, kamba hiyo inakatika miaka 60.
Hivyo kabla ya hiyo miaka haijafika, Bwana Mungu anatupa tahadhari, tumkumbuke yeye kabla ya kuifikia hiyo miaka..kwasababu tusipomkumbuka na katika hiyo, na huku maisha yetu yote tumeisikia injili, baada ya miaka hiyo, hakutakuwa tena na nafasi ya sisi kumgeukia yeye.. kwasababu nguvu ya kuvutwa kwake haitokani na sisi, bali inatoka kwake.. hivyo hatupaswi kuipuuzia kipindi hichi cha ujana..
Hili ni neno la kuhitimisha. Kuwa tumkumbuke muumba kabla hatujamaliza maisha yetu hapa duniani. Baada ya kifo hakuna wokovu tena, biblia inasema “mti uangukiapo huko huko utalala Mhubiri 11:3”.
Hakuna nafasi ya pili baada ya kifo!. Bwana anasema tumkumbuke yeye kabla “roho zetu hazijamrudia yeye”. Kwasababu hakutakuwa na nafasi ya pili, kwamba tufufuliwe tutubu, ndipo tufe.. biblia inasema “tumewekewa kufa mara moja na baada ya kifo hukumu (Waebrania 9:27)”
Hivyo kwa hitimisho ni kwamba Bwana Mungu anatuonya kwamba tuutumie muda wetu vizuri tukiwa hapa duniani!.. Na yale mawazo adui aliyoyaweka katika vichwa vyetu kwamba tutakapokuwa wazee ndipo tutamrudia Mungu, hayo mawazo tuyakatae!, kwasababu ni ya adui.. kiufupi!, kwajinsi muda unavyozidi kwenda ndivyo ile njia ya wokovu inasonga!, na kuzidi kuwa nyembamba.. Ndio maana Bwana akatuambia..
2Wakorintho 6:2 “(Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa”
Tubu na kumpokea Kristo leo, usiseme ngoja nimalizie kuiba kidogo, au ngoja niendele kufanya ukahaba, au ngoja nimalizie kunywa pombe, baada ya kipindi Fulani nitaokoka!.. Ndugu hayo ni mahubiri ya shetani anayokuhubiria kichwani pako. Pia usiseme ngoja nitakapostaafu, nitapata muda mwingi wa kumtafuta Mungu..jambo hilo lifute kwenye akili yako kuanzia sasa, “mkumbuke muumba wako kabla kamba ya fedha haijakatika”.
Kwa kadiri muda unavyozidi kwenda ndivyo ile njia inavyozidi kusonga na kuwa nyembamba, wakati uliokubalika ndio huu!, saa ya wokovu ndio sasa. Kumbuka pia hujui siku yako ya kuondoka duniani ni lini!, na yeye anasema mkumbuke kabla roho yako haijamrudia yeye!.
Je upo tayari kumkumbuka leo!, na kusema siutaki tena ulimwengu na tamaa zake zote?.. Pengine umri wako ni mkubwa lakini bado unaisikia hii sauti ikikuambia tubu tubu!.. hiyo ni neema fahamu kuwa ndio upo kipindi cha kumalizia!… muda si mrefu hutaisikia tena! Kwasababu hatuamui sisi kipindi cha kumfuata Yesu, bali neema ya Mungu ndiyo inayoamua juu ya maisha yetu. Ikiisha hiyo, hata tufanyaje hatutaweza kumtafuta Mungu.
Kama upo tayari kumpokea Yesu leo, hapo ulipo jitenge kwa muda mchache, kisha tubu dhambi zako zote kwa Bwana Yesu, na dhamiria kuziacha, kama ni ulevi, uzinzi, wizi, uuaji, uvaaji mbaya, utukuanaji, kamari, na mambo mengine yote yasiyompendeza Mungu, unadhamiria kuacha yote, na baada ya kutubu kwa dhati kabisa, hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa, kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo kulingana na matendo 2:38, na Roho Mtakatifu ataingia ndani yako kukupa uwezo wa kushinda dhambi, na kukuongoza katika kweli yote.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine:
Mada Nyinginezo:
Biblia ituambia tusalimiane kwa busu takatifu. Hili busu ndio lipi?
About the author